MSHAMBULIAJI mpya wa Geita Gold, Raymond Lulendi, amesema licha ya ushindani mkubwa uliopo katika eneo la kikosi hicho msimu huu ila hana hofu, kwa sababu atapambana kadri ya uwezo wake atakavyopewa nafasi na benchi la ufundi la timu hiyo.
Nyota huyo amejiunga na Geita Gold katika dirisha dogo lililofungwa Januari 30, 2026, baada ya kuachana na kikosi cha Songea United kinachoshiriki pia Ligi ya Championship, alichojiunga nacho mwanzoni mwa msimu akitokea JKU ya Zanzibar.
“Ushindani ni mkubwa kwa sababu wapo washambuliaji wengi na wazuri niliowakuta na wanafanya vizuri, kusajiliwa kwangu ni ishara tosha ya kuonyesha benchi la ufundi kuna kitu kikubwa ilichokiona hivyo, nipo tayari kupambana,” amesema Lulendi.
Mshambuliaji huyo aliyewahi kuichezea pia Fountain Gate kabla ya kutua JKU, amesema licha ya ushindani uliopo hadi sasa, ila anaamini Geita ni sehemu nzuri kwake ya kutimiza malengo yake ikiwemo kuirejesha Ligi Kuu na kuibuka mfungaji bora.
Nyota huyo ameenda kuongeza nguvu katika eneo la ushambuliaji la Geita Gold linaloongozwa na Maulid Shaban aliyeifungia timu hiyo mabao saba, ikiwa ni idadi sawa na aliyofunga Raymond Lulendi, wakati akiwa na kikosi hicho cha Songea United.