Mahakama kutumia teknolojia kuendesha kesi Zanzibar

Unguja. Mahakama Kuu ya Zanzibar inatarajia kuzindua mfumo wa kisasa wa usikilizaji wa kesi na usimamizi wa mashauri kwa njia ya kielektroniki, hatua inayolenga kuimarisha utoaji wa haki kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

Uzinduzi wa mfumo huo unatarajiwa kufanyika Februari 9, 2026 katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi kisiwani Pemba, ikiwa ni kilele cha maadhimisho ya wiki ya sheria Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jaji Mkuu wa Zanzibar, Khamis Ramadhan Abdulla, mfumo huo unatarajiwa kuzinduliwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.

Jaji Ramadhani, amesema kuanzishwa kwa mfumo huo wa kielektroniki kutasaidia kesi zote kusikilizwa kwa kutumia teknolojia, jambo litakalopunguza changamoto za ucheleweshaji wa mashauri na kuongeza uwazi katika utoaji wa haki.

“Mfumo huo utawezesha usimamizi bora wa mashauri kuanzia usajili wa kesi, upangaji wa tarehe za kusikilizwa, hadi ufuatiliaji wa maamuzi kwa njia ya kidijitali,” amesema.

Amefafanua matumizi ya teknolojia katika mahakama yataongeza ufanisi wa kazi, kupunguza gharama kwa wananchi na taasisi za haki, pamoja na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kimahakama.

Kwa mujibu wa Jaji mkuu huyo, hatua hiyo ni sehemu ya mageuzi makubwa yanayofanywa na Mahakama ya Zanzibar ili kuendana na maendeleo ya sayansi na teknolojia pamoja na mahitaji ya jamii ya sasa.

Maadhimisho ya wiki ya Sheria Zanzibar yanalenga kuhimiza matumizi ya Tehama katika utoaji wa haki, kuimarisha huduma kwa wananchi na kujenga mfumo wa mahakama wenye ufanisi na uwajibikaji.

Ameongeza kuwa maadhimisho hayo ni jukwaa muhimu la kuwakutanisha wadau wa haki ili kujadili masuala mbalimbali yanayohusu utawala wa sheria na kubadilishana uzoefu wa kitaaluma.

Wiki ya sheria ni tukio muhimu linalolenga kuimarisha utawala wa sheria, haki, uwajibikaji na uwazi katika utoaji wa huduma za kimahakama nchini.

Jaji Ramadhan, amesema kupitia maadhimisho hayo, Mahakama hupata fursa ya kutathmini mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizopo pamoja na kuweka mikakati ya kuboresha huduma za haki kwa wananchi.

Maadhimisho ya Wiki ya Sheria kwa mwaka huu yanafanyika chini ya kaulimbiu isemayo “Matumizi ya Tehama ni chachu ya upatikanaji wa haki.”

Kwa mujibu wa Jaji Ramadhan, kaulimbiu hiyo inaakisi dhamira ya serikali katika kuimarisha mifumo ya haki kwa kutumia teknolojia.

Hata hivyo, amesema katika kipindi cha maadhimisho hayo, kutakuwa na shughuli mbalimbali ikiwemo makongamano ya kitaaluma yanayowakutanisha wataalamu wa sheria na wadau wa sekta ya haki.

Shughuli nyingine zitakazofanyika ni utoaji wa elimu ya haki kwa jamii, lengo likiwa ni kuwawezesha wananchi kufahamu haki zao za msingi na taratibu za kisheria, pia kutakuwa na maonyesho ya huduma za kimahakama pamoja na ushiriki wa taasisi mbalimbali za haki zitakazowasilisha upatikanaji wa taarifa kwa wananchi.

Baadhi ya wadau wa sheria wamesema kuanzishwa kwa mfumo wa usikilizaji wa kesi kwa kutumia teknolojia kutaongeza uwazi, kupunguza gharama na kurahisisha usikilizaji wa kesi.

“Tulikuwa tumechelewa sana kuanzisha huu mfumo, lakini hata kwa hatua hii utasaidia kwa kiasi kikubwa masuala ya uwazi na kupunguza hata msongamano mahakamani, amesema mdau wa mahakama Laylat Haji.