Zaidi ya watu 200 wapoteza maisha, mgodi ukiporomoka DRC

Dar es Salaam. Zaidi ya watu 200 wameuawa kufuatia kuporomoka kwa mgodi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), mamlaka za waasi zimesema.

Ajali hiyo ilitokea Jumatano katika mji wa Rubaya, baada ya mgodi huo kutitia kutokana na mvua kubwa, kwa mujibu wa Lumumba Kambere Muyisa, msemaji wa gavana wa waasi wa jimbo la Kivu Kaskazini.  

Kwa mujibu wa BBC, wanawake na watoto walikuwa miongoni mwa waliokuwa wakichimba madini ya koltani, ambayo yanatumika kutengeneza vifaa vya kielektroniki kama simu janja na kompyuta.

Aliyekuwa msimamizi wa mgodi huo amesema eneo hilo halikuwa likitunzwa ipasavyo, hali iliyoongeza uwezekano wa ajali na pia kuathiri juhudi za uokoaji pindi ajali zinapotokea. Ameongeza kuwa udongo dhaifu wa eneo hilo uliifanya hali kuwa mbaya zaidi.

Wanawake, watoto na wachimbaji wadogo wasioajiriwa rasmi na kampuni za uchimbaji ni miongoni mwa waliopoteza maisha. Takribani manusura 20 wameripotiwa kuwa wanapatiwa matibabu hospitalini.

Mtu mmoja aliyepoteza binamu yake katika ajali hiyo, amesema tukio hilo ni pigo kubwa kwa familia na jamii. “Sikufikiria angefariki katika mazingira kama hayo,” amesema mtu huyo aliyetaka jina lake lihifadhiwe, akimwelezea marehemu kuwa mtu jasiri na mwenye ndoto, aliyekuwa akijitahidi kuwatunza mkewe na watoto wawili.

“Niliendelea kuwa na matumaini kwa kuwa uchunguzi ulikuwa unaendelea na mwili wake haukuonekana mara moja. Lakini kwa masikitiko, baada ya saa kadhaa, mwili wake ulipatikana,” kiliongeza chanzo hicho cha habari.

Gavana Erasto Musanga, aliyeteuliwa na waasi wa M23 baada ya kuchukua maeneo makubwa ya Kivu Kaskazini, amewatembelea manusura wa tukio hilo Ijumaa.

Rubaya ni miongoni mwa miji kadhaa ya Kivu Kaskazini iliyo chini ya udhibiti wa M23.

Migodi ya Rubaya inakadiriwa kuwa na takribani asilimia 15 ya akiba yote ya koltani duniani na nusu ya hifadhi ya madini hayo nchini DRC. Madini hayo yana tantalum, inayotumika kutengeneza vifaa vya kielektroniki vyenye uwezo mkubwa, hivyo kuwa na mahitaji makubwa duniani.

Timu ya BBC ilipotembelea eneo hilo Julai 2025, ilishuhudia wachimbaji wakichimba kwa mikono kutafuta madini hayo ya thamani. Hali ya kazi mgodini humo ilielezwa kuwa mbaya, huku mashimo hatarishi yakitapakaa katika eneo kubwa.

Tangu mwaka 2024, waasi wa M23 wamekuwa wakidhibiti migodi hiyo. Umoja wa Mataifa umeituhumu kundi hilo kwa kutoza kodi katika sekta ya madini kwa manufaa yao binafsi.

BBC imesema imewasiliana na Serikali ya DRC mjini Kinshasa ili kupata maoni yao kuhusu tukio hilo.