Arusha. Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imemuongezea adhabu Pius Ernest kutoka kifungo cha miaka 30 jela hadi kifungo cha maisha jela, baada ya kubaini kuwa adhabu ya awali ilikuwa kinyume cha matakwa ya sheria.
Awali, Pius alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumlawiti mtoto wa mwajiri wake mwenye umri wa miaka saba.
Kwa kawaida, mkata rufaa hulenga kupunguziwa adhabu au kuachiwa huru, hata hivyo hali imekuwa tofauti kwa Pius, ambaye rufaa yake imesababisha kuongezewa adhabu hadi kifungo cha maisha jela.
Uamuzi huo ulitolewa Januari 30, 2026 na Jaji Awamu Mbagwa, ambaye alisema Mahakama Kuu imejiridhisha kuwa kosa lililotendwa lilimhusu mtoto aliye chini ya umri wa miaka 18, hivyo adhabu iliyotolewa awali haikulingana na matakwa ya kisheria.
Jaji Mbagwa amesema kifungu cha 154(2) cha Kanuni ya Adhabu kinaelekeza kuwa endapo kosa la kufanya mapenzi kinyume na maumbile litafanywa dhidi ya mtoto aliye chini ya umri wa miaka 18, adhabu yake ni kifungo cha maisha jela.
“Hukumu ya kifungo cha maisha ni ya lazima kwa mujibu wa sheria. Kwa hiyo, ninaondoa adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela na kuibadilisha kuwa kifungo cha maisha jela,” amesema Jaji Mbagwa.
Kwa mujibu wa kumbukumbu za Mahakama, Pius alishtakiwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam kwa kosa la kumlawiti mtoto wa miaka minane kinyume na Kifungu cha 154(1)(a) na (2) cha Kanuni ya Adhabu.
Ilidaiwa kuwa alitenda kosa hilo Mei 29, 2022, eneo la Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam.
Mahakama ilielezwa kuwa siku ya tukio, mama wa mtoto alikuwa ameondoka kwenda kazini Kariakoo na kumwacha mtoto nyumbani. Mrufani alitumia fursa hiyo kumwita jikoni kwa kisingizio cha kumpa matunda kabla ya kumfanyia kitendo hicho cha kikatili.
Ilidaiwa kuwa mama wa mtoto aliporejea nyumbani na kufanya ukaguzi wa kawaida wa usalama usiku huo, alibaini mwenendo usio wa kawaida kwa mtoto wake. Baada ya kumuhoji, alimweleza kuwa alikuwa amelawitiwa na mshtakiwa siku hiyo na siku nyingine zilizotangulia.
Kutokana na tuhuma hizo, tukio liliripotiwa kwa viongozi wa eneo husika na baadaye Polisi Kituo cha Kawe, ambako mrufani alikamatwa na kufikishwa mahakamani.
Upande wa mashtaka uliita mashahidi watano akiwemo mama wa mtoto, mwathirika mwenyewe, askari polisi pamoja na daktari aliyemfanyia mtoto uchunguzi wa kitabibu.
Daktari huyo aliieleza Mahakama kuwa alibaini dalili za wazi za ukatili wa kingono, ikiwemo kulegea kwa misuli ya sehemu ya haja kubwa, hali iliyoendana na maelezo ya tukio yaliyotolewa na mtoto.
Kwa upande wake, mshtakiwa alikanusha mashtaka hayo akidai kuwa alitungiwa kesi na mama wa mtoto, lakini alishindwa kueleza sababu yoyote ya msingi inayoweza kuhalalisha madai hayo.
Baada ya kusikiliza ushahidi wote, Mahakama ya Wilaya iliridhika kuwa mashtaka yalithibitishwa bila kuacha shaka yoyote na hivyo ikamhukumu mshtakiwa kifungo cha miaka 30 jela.
Akiwa hajaridhika na hukumu hiyo, Pius alikata rufaa katika Mahakama Kuu akipinga hatia na adhabu, akidai kuwa ushahidi wa mtoto ulipokelewa kinyume na sheria kwa kuwa hakukuwa na uchunguzi wa awali kuthibitisha uwezo wa mtoto kuelewa kiapo na wajibu wa kusema ukweli.
Pia, alidai kuwa kulikuwa na utata katika ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka, hususan kuhusu tarehe ya uchunguzi wa kitabibu, pamoja na ucheleweshaji katika kumfikisha mahakamani.
Hata hivyo, upande wa Jamhuri ulieleza kuwa hoja hizo hazikuwa na mashiko na hazikuathiri haki ya mshtakiwa kupata haki.
Katika uamuzi wake, Mahakama Kuu ilisisitiza kuwa ushahidi wa mtoto uliungwa mkono na ushahidi wa kitabibu pamoja na ushahidi wa mama wa mtoto, na kwamba mrufani alishindwa kuupinga kwa namna yoyote yenye nguvu.
Mahakama pia ilibainisha kuwa adhabu ya miaka 30 jela iliyotolewa awali ilikuwa kinyume cha sheria, hivyo ikaibatilisha na kumuhukumu mrufani kifungo cha maisha jela, huku rufaa yake ikitupiliwa mbali.