KOCHA Mkuu wa Transit Camp, Shadrack Nsajigwa, amesema kuondoka kwa aliyekuwa mshambuliaji wa kikosi hicho, Adam Uledi ni pengo kubwa kutokana na ubora wake, ingawa usajili wa nyota, Abrahaman Mussa anaamini utaleta pia mabadiliko chanya.
Uledi aliyeifungia Transit Camp mabao 11 msimu huu katika Ligi ya Championship, amekamilisha usajili wake wa kujiunga na KMC inayoshiriki Ligi Kuu Bara, huku Abrahaman Mussa akirithi nafasi yake baada ya kuondoka Gunners FC ya jijini Dodoma.
“Ni pigo kubwa kwetu kwa sababu alikuwa ni mchezaji muhimu tunayemtegemea msimu huu, lakini ni fursa pia nzuri kwake ya kuzidi kujitengenezea jina lake, ubora wa Abrahaman utakuwa ni chachu ya mabadiliko chanya kikosini,” amesema Nsajigwa.
Aidha, Nsajigwa amesema mabao manane aliyofunga mshambuliaji, Abrahaman Mussa msimu huu akiwa na kikosi cha Gunners FC, ni kuonyesha wazi ubora wa nyota huyo kutokana na uzoefu wake, hivyo hana shaka kuhusu kuziba nafasi hiyo ya Adam Uledi.
Abrahaman anakumbukwa zaidi kwa msimu wa 2016-2017, akiwa na Ruvu Shooting ambapo alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara baada ya kufunga mabao 14, sawa na Simon Msuva aliyekuwa anaichezea Yanga japo kwa sasa anaichezea Al-Talaba SC ya Iraq.