Kipaumbele cha Wandiba Gunners FC

KOCHA mpya wa Gunners FC ya jijini Dodoma, Mathias Wandiba, amesema malengo makubwa aliyopewa na uongozi wa kikosi hicho ni kuhakikisha timu hiyo inabakia Ligi ya Championship, licha ya ushindani mkubwa uliopo na mwenendo pia usioridhisha.

Akizungumza na Mwanaspoti, Wandiba, amesema anaijua vyema Ligi ya Championship kwa sababu sio mara ya kwanza kufundisha, ingawa, ili kufikia malengo ya kuendelea kukibakisha kikosi hicho msimu ujao anahitaji ushirikiano wa pamoja kikosini.

“Nafasi tuliyopo sio mbaya wala nzuri sana kwa sababu ya ushindani uliopo, naamini bado tuna uwezo wa kufanya vizuri kwa mechi za raundi ya pili, jambo kubwa ni kuhakikisha hatudondoshi pointi kizembe ili tuyafikie malengo,” amesema Wandiba.

Wandiba aliyewahi kuzifundisha Geita Gold, Pamba Jiji, Mbeya City, Singida United na Alliance FC, amejiunga na timu hiyo baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Juma Ikaba kusitishiwa mkataba kwa makubaliano ya pande mbili kutokana na mwenendo mbaya.

Ikaba aliyefundisha timu za Gwasa, Usalama na Baobab Queens, aliiongoza Gunners tangu ikiwa Ligi ya Mkoa (RCL) hadi Ligi ya Championship, ambapo inashika nafasi ya 11 na pointi 17, baada ya kushinda mechi nne tu, sare tano na kupoteza saba.

Gunners imepanda Ligi ya Championship msimu huu baada ya kuibuka mabingwa wa First League msimu wa 2024-2025, kufuatia kuongoza kundi B na pointi 35, ikiungana na kikosi cha Hausung kutoka Njombe iliyoongoza ikitokea kundi A na pointi 25.