SHABIKI wa Yanga ambaye unaona timu yako haikucheza vizuri soma hii aliyosema kocha wa Al Ahly ya Misri kwamba wenyeji wao wana timu imara sana na wachezaji bora kisha akawataja baadhi.
Kocha wa Al Ahly Jesse Thorup ameliambia Mwanaspoti kuwa haikuwa rahisi kwao kupata pointi moja ingawa walitengeneza nafasi, lakini ubora wa Yanga uliwapa changamoto ngumu juzi.
Thorup amesema kuwa kama soka lingeweza kuangalia usawa basi wao na Yanga wanastahili kwenda robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kutokana na namna walivyocheza vizuri.
Kocha huyo raia wa Denmark amesema hatua ya Yanga kushika nafasi ya pili mpaka mzunguko wa nne wa hatua ya makundi, inahitaji kuheshimiwa kwamba mabingwa hao wa soka Tanzania wana timu imara.
“Nafahamu hesabu za soka, wakati ratiba inatoka ilikuwa inaonekana hili ni kundi gumu sana, lakini leo (juzi) tumepata sare hapa, tulikutana na timu inayocheza vizuri wakitupa changamoto nzuri,” amesema Thorup.
“Kwa muda mrefu kundi letu tumekuwa tukifukuzana nao kwa karibu mpaka huu mzunguko wa nne, kama ingekuwa anayekwenda makundi inaangaliwa kwa namna ulivyojituma, hizi timu mbili zilizocheza leo hapa nadhani zilistahili kusonga mbele.
Aidha, Thorup amesema amevutiwa na viwango vya winga mpya wa Yanga, Allan Okello, Pacome Zouzoua na beki Bakari Mwamnyeto ambao walikuwa kwenye kiwango bora katika mchezo huo.
“Kuanzia mchezo wa kwanza nyumbani niliona namna yule mchezaji namba 20 (Okello) ni mchezaji mbunifu sana, yule namba 10 (Zouzoua) tulikuwa na taarifa zake kwa muda mrefu, lakini bado alicheza vizuri na kule kwenye ulinzi nahodha wao alifanya kazi kubwa sana.
“Kiujumla wana wachezaji wengi wazuri sana wenye njaa ya mafanikio wanajituma sana wanaweza kufika mbali zaidi kama watajitunza na kuendelea kucheza kwa ubora huu.”