KIUNGO wa Barberian FC, Muhsin Mlaga, amesema licha ya dili lake la kwenda Simba kushindwa kukamilika dakika za mwisho, ila, jambo la kuhusishwa na kikosi hicho kwake imempa motisha kubwa ya kuamini kila kitu kinawezekana ukionyesha juhudi.
Nyota huyo anayemudu kucheza kiungo mkabaji na ushambuliaji kwa ufasaha, alifanya mazungumzo ya kujiunga na Simba katika dirisha dogo la Januari 2026, ingawa dili hilo lilikwama dakika za mwisho na kushindwa kukamilika kwa wakati uliotakiwa.
“Ni fahari kuona timu kubwa ya Simba inafanya mazungumzo na menejimenti yangu kunihitaji, hii imenipa morali ya kuzidi kupambana na kuonyesha kipaji changu, licha tu ya dili hilo kushindwa kufanikiwa ila ni heshima kwangu,” amesema Mlaga.
Msimamizi wa mchezaji huyo ambaye kitaaluma ni Wakili, James Rukeha, amesema licha tu ya mazungumzo chanya na uongozi wa Simba ila, usajili huo haukufanikiwa mwishoni, kutokana na sababu mbalimbali ambazo asingependa kuziweka wazi kwa sasa.
Nyota huyo kabla ya kutua Barberian, aliichezea pia Ndanda, huku akianzia katika kituo cha Michezo cha Kapteni (Captain Sports Centre), ambacho ni cha aliyekuwa kocha na mchezaji wa Majimaji, Yanga, Mtibwa Sugar na KenGold, Omary Kapilima.