Dar es Salaam. Pendekezo la hoja iliyowasilishwa bungeni la kutaka itungwe sheria itakayowalazimisha watoto kuwatunza wazazi wao wasiojiweza, limeibua mjadala wengi wakihoji ni vipi sheria hiyo itakuwa na utekelezaji, na wengine wakitaka sheria hiyo iwe ya Serikali kuwatunza wazee na si kuwalazimisha watoto.
Mtazamo huo umekuja siku tatu tangu Mbunge wa Kinondoni, Abbas Tarimba kuchangia hoja bungeni kwamba Serikali haioni haja ya kuweka sharti la kisheria la watoto wakubwa kuwatunza wazazi wao wasiojiweza.
Hoja kama hiyo iliwahi kuibuka kwenye Bunge la 12, ambapo aliyekuwa Mbunge wa Kahama Mjini (CCM), Jumanne Kishimba kutaka itungwe sheria kwa ajili ya kuwabana watoto wawatunze wazazi.
Hoja hiyo imeibua mijadala kama huo ni wajibu wa kimaadili au liwe takwa kisheria? Huku baadhi wakihoji ni vipi itatekelezeka.
Baadhi yao wametolea mifano ya baadhi ya nchi ambazo zina sheria hiyo, ingawa utekelezaji wake umekuwa na changamoto za migogoro ya kifamilia na ugumu wa kuthibitisha uwezo wa kifedha wa mtoto.
Hapa nchini baadhi ya wazazi na watoto wamekuwa na mitazamo tofauti, watoto wakisema hakuna haja ya sheria wakiamini ni wajibu wa mtoto kumtunza mzazi anapokuwa na kazi na kipato.
“Wala hakuna haja ya sheria, kwa mtoto ambaye ana kazi na hataki kumtunza mzazi wake aliyemlea na kuhangaika naye, Mungu ndiye atatoa adhabu dhidi yake,” amesema Jerome Mathias kijana wa miaka 37.
Neema Shayo (25) amesema ikiwapo sheria itawabana wale wenye vipato kuwahudumia wazazi wao, lakini akihoji ni kwa nini mtoto alazimishwe kumuhudumia mzazi na jambo hilo lisifanyike kwa upendo na utashi wa mtoto?
Wakati Anna Nelson mzee wa miaka 65 yeye anaamini watoto wengi hasa wa kiume huwa hawaoni umuhimu wa kuwatunza wazazi wao pale wanapokuwa wakubwa na kuanzisha familia zao.
Nelson katika hoja hiyo, anasema ikiwepo sheria wale wenye vipato itasaidia kama ambavyo kuna sheria ya baba kumtunza mtoto wake mdogo.
“Iwe lazima kama ambavyo baba mwenye kazi anakatwa mshahara wake na kumtunza mtoto, basi na kijana mwenye kazi sheria imlazimishe akatwe mshahara na pesa imtunze mzazi wake ambaye hana kipato na ni mzee,” amesema.
Akifafanua hilo kwa muktadha wa kijamii, Askofu Msaidizi mstaafu wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini amesema sheria itakayotungwa kwenye hoja hiyo ni Serikali kuwa na mfuko wa kutunza wazee na si vinginevyo.
“Watoto kuwatunza wazee hiyo ni amri ya Mwenyezi Mungu tu, wakiwa na hofu ya Mungu watafanya lakini kwa kuwatungia sheria si rahisi na itakuwa na ugumu kutekelezeka,” amesema na kufafanua.
“Badala ya kuweka sheria ya watoto kuwatunza wazee, tuweke sheria ya pensheni ya kutunza wazee, ifanyike kama ambavyo tumekwenda kwenye bima ya afya kwa wote.”
Amesema kukiwa na mfuko wa kuhudumia wazee ili wazee wasiojiweza wakatunzwe kwenye nyumba za wazee na wale wanaojiweza wajitunze wenyewe.
“Serikali iwe na sheria na fungu la kutunza wazee wasiojiweza kuanzia umri fulani kama ambavyo Ulaya wanafanya, japo huko kuwatunza sio shida lakini nako wanakuwa na upweke watoto wao hawaonekani.
“Hili suala linahitaji utaratibu mzuri, kuna wazee inafika mahali hawajiwezi tena, anaishi maisha ya upweke, japo aliweza kulea watoto 10 ambao wote wameshindwa kumlea, sheria ya kuwalazimisha watoto kuwatunza wazazi inaweza kuwekwa lakini ikawa ngumu kutekelezeka,” amesema.
Mmoja wa majaji nchini ambaye aliomba hifadhi ya jina, amesema sheria yoyote inayotungwa ni kwa sababu ya matakwa ya jamii ili kuongeza ustawi wake.
“Sheria zetu zimegawanyika zipo za private law na public law, hivyo kwenye hoja ya mtoto kumuhudumia mzazi kama imetokea utafiti ukafanyika na jamii ikataka mtoto kumhudumia mzazi, lazima tuongozwe na matakwa ya jamii, japo nchi yetu haijafika huko,” amesema.
Naye wakili wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Fulgence Massawe amesema mfumo wa hifadhi ya jamii ndiyo unapaswa kuwatunza wazee.
“Japo katika utamaduni wa kwetu watoto kuwatunza wazazi ni kawaida, japokuwa jukumu hilo siyo takwa la kisheria, mfumo unataka hifadhi ya jamii ndiyo iwatunze wazee,” amesema.
Katika hoja hiyo, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Watoto, Maryprisca Mahundi alisema Serikali inatambua umuhimu wa familia na jamii kuchukua jukumu la kulea wazee.
“Jukumu hilo ni msingi unaojengwa katika hatua za awali za malezi na makuzi ya watoto,” alisema Mahundi akifafanua kwamba Serikali imetunga sera ya wazee iliyoweka msisitizo wa kuimarisha mfumo wa kisheria kulinda wazee.
Mtaalamu wa malezi ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Christian Bwaya amesema kuwalaumu watoto kwa kutokuwahudumia wazazi na kufikiri sheria ndio itawalazimisha ni kuonesha jamii haielewi tatizo liko wapi.
“Sheria haiwezi kubadili jambo hili lenye mzizi mrefu kwenye malezi.
“Fikiria mtoto ambaye tangu anazaliwa hajawahi kujisikia kusikika, kueleweka na kuthaminika, mzazi anazaa mtoto hana muda naye. Unategemea nini,” amesema.
Bwaya amesema mtu huwa anachuma alichopanda akishauri mahali pa kuanzia ni kuwakumbusha wazazi wajibu wao kwa watoto.
“Kama kuna sheria inahitajika basi iwe hiyo ya kurudisha heshima ya mahusiano ya familia na kuelewa kuwa tabia zetu zinajengwa kwenye miaka ya mwanzo ya maisha yetu.
“Lea mtoto kwa maana halisi ya kulea. Jenga ukaribu na mtoto. Heshimu hisia zake, penye kuwajibisha fanya hivyo kwa upendo. Hutohitaji sheria kulazimisha kupata matunda ya mbegu ambayo hukuipanda,” amesema.