Mwili uliokatika vipande wakutwa juu ya reli, mashuhuda wasimulia

Tabora. Mwili wa mwanaume ambaye hajafahamika umekutwa juu ya reli huku ukiwa umekatika vipande katika eneo la Kombomasai, Kata ya Malolo, Manispaa ya Tabora, huku ikisadikiwa kuburuzwa na treni iliyopita usiku wa kuamkia leo.

Akizungumzia tukio hilo leo Februari mosi, 2026, Diwani wa Malolo, Naomi Kasanga, ameeleza kuwa akiwa nyumbani kwake saa 2 asubuhi alipata taarifa kutoka kwa wananchi wa mtaa huo kuwa kuna mwili juu ya reli, umekatika vipande na hajafahamika ni wa nani.

“Nimepokea taarifa ya tukio hili, lakini huyu mtu hajafahamika bado kwamba ni mkazi wa wapi, ila inaonekana pia kuwa amefariki usiku wa kuamkia leo,” amesema.

Kasanga ameliomba Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuongeza alama za hatari katika njia hiyo, kwa sababu inaonekana mtu huyo ameburuzwa na treni baada ya kugongwa.

Diwani wa kata ya Malolo manispaa ya Tabora akizungumzia ajali ya mwanaume kugonga Treni maeneo ya Malolo manispaa ya Tabora



“Kwenye reli hii zinapita treni kutoka Kigoma na Mpanda mkoani Katavi, lakini jana usiku inasemekana ilipita treni kutoka Kigoma saa 3 usiku wa kuamkia leo. Sasa ombi langu ni zile honi za treni tulizokuwa tunashuhudia zamani zirudi tena, maana mtu akisikia anakuwa na tahadhari na kukimbia mbali na reli,” amesisitiza diwani huyo.

Kaimu Mwenyekiti wa Mtaa wa Kombomasai, Moshi Ramadhani, amesema inasadikika marehemu huyo aligongwa na treni usiku ndipo ikamburura mwili wake na kukatika vipande, kama ilivyoshuhudiwa, huku akiwataka wananchi kuendelea kuwa makini wanapotembea au kuvuka maeneo yenye reli ili kuepusha ajali zinazoendelea kugharimu maisha ya watu.

“Tukio hili sasa ni la pili au la tatu mtu kupoteza maisha kwa kugongwa na treni. Sio jambo zuri. Niwaombe wenzetu wa reli warudishe tahadhari zilizokuwepo zamani kama vile honi kubwa, kwani hatukuwa tukishuhudia matukio haya mara kwa mara,” amesema.

Kwa upande wake, Joseph Deus, mkazi wa Kombomasai, amesema alisikia kuwa kuna mtu amefariki na mwili uko juu ya reli, na baada ya kusogea ndipo akaona mwili umekatikakatika na nguo zote zimechanika.

“Yaani kama hatutaongeza tahadhari, tutaisha, kwa sababu matukio haya yameanza kujirudia siku hizi,” amesema.

Kwa mujibu wa Ofisa Mnadhimu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Tabora, Omary Simba, amesema kulingana na mazingira ya mwili huo ni wazi kuwa marehemu amegongwa na treni na mwili wake umeburuzwa.

“Mwili huu umeburuzwa na treni, ndiyo maana umekatika vipande. Tunaupeleka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora, Kitete, kwa ajili ya uchunguzi zaidi na taratibu nyingine ziweze kufuata,” amesema ofisa huyo wa Zimamoto.