Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imefanya mazungumzo na viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya (EU) jijini Brussels nchini Ubelgiji, hatua inayotafsiriwa kuwa mwelekeo mpya wa diplomasia.
Katika mazungumzo hayo, ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, ulijadiliana na viongozi wa EU, kuhusu kuimarisha ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na kiusalama.
Hayo yamefanyika leo, Jumapili Februari 1, 2026 Balozi Kombo alipokutana na Makamu wa Rais wa Tume ya Ulaya na Mwakilishi Mkuu wa EU katika Sera za Mambo ya Nje na Usalama, Kaja Kallas nchini Ubelgiji.
Balozi Kombo amesema kuna umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa vitendo unaojengwa katika misingi ya heshima ya mamlaka ya kitaifa, biashara inayozingatia utawala wa sheria, uwekezaji unaotabirika na mifumo ya ushirikiano inayotekelezeka.
Ujumbe huo, uliomhusisha Waziri wa Nchi kutoka Ofisi ya Rais, Profesa Palamagamba Kabudi, ulikutana pia na Kamati ya Kisiasa na Usalama ya EU (PSC), chombo chenye ushawishi mkubwa kinachoundwa na mabalozi wa nchi 27 wanachama wa umoja huo.
Kupitia kikao hicho, Tanzania iliwasilisha msimamo wake moja kwa moja kwa EU, huku ikithibitisha nafasi yake kama mshirika wa kuaminika katika masuala ya amani, usalama na uthabiti wa ukanda wa Afrika Mashariki.
Katika ngazi ya bunge, Waziri Kombo alifanya mazungumzo katika Bunge la Ulaya, ikiwemo kukutana na Makamu wa Rais wa Bunge hilo, Younous Omarjee.
Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha diplomasia ya kibunge kama nguzo ya uhusiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na EU, hususan katika biashara, utawala bora na uhusiano wa watu kwa watu.
Katika ziara hiyo pia, Ujumbe wa Tanzania ulikutana na kufanya mazungumzo na Kamishna wa EU wa Ushirikiano wa Kimataifa, Jozef Síkela.
Katika kikao hicho, Tanzania ilieleza wazi vipaumbele vyake vya ushirikiano unaozalisha ajira, kukuza ujuzi, kuongeza thamani ya mazao na kuimarisha miundombinu himilivu na mabadiliko ya kiuchumi.
Ujumbe wa Tanzania uliambatana na Balozi Swahiba Mndeme, Mkurugenzi wa Ulaya, Balozi Jestas Abuok Nyamanga, Mwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Ulaya na maofisa wengine waandamizi.
Tanzania inafanya ziara hiyo, ukiwa umepita mwezi mmoja tangu Bunge la EU Novemba 29, mwaka jana lisitishe msaada wa Euro milioni 150 (zaidi ya Sh461.53 bilioni), zilizopaswa kuletwa nchini Januari mwaka huu, kupitia mfuko wa NDICI-Global Europe.
Hatua hiyo ya Bunge la EU, ilitokana na kile ilichoeleza, kukithiri vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini vinavyohusisha utekaji wa raia, ukandamizwaji wa wanasiasa wa upinzani na kuminywa kwa uhuru wa kuongea.
Hayo yaliibuka, baada ya vurugu ya Oktoba 29, mwaka jana na kusababisha kuuawa kwa raia, uharibifu wa mali za umma na zile za watu binafsi.
Hata hivyo, uamuzi wa bunge hilo, ulijibiwa na Serikali ya Tanzania, ikisema haijatendewa haki, kwa kuwa wakati inajadiliwa haikupewa nafasi ya kusikilizwa kwa upande wake.
Tanzania ilisisitiza kwa kuwa ni Taifa huru halipaswi kupangiwa mambo ya kufanya.