Dar es Salaam. Zikiwa zimesalia siku 11 kabla Rais Samia Suluhu Hassan kutimiza siku 100 madarakani tangu kuapishwa kwake Novemba 5, 2025, Tanzania inajaribu kufanya uponyaji wa kisiasa na migawanyiko iliyojitokeza huku ajenda ya maridhiano ikijitokeza kama ahadi.
Pia, mchakato wa maridhiano unaibua mjadala mpana kufuatia uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 uliotikisa hali ya kisiasa.
Wakati na baada ya uchaguzi mkuu mwaka jana, kuliibuka maandamano yaliyozaa vurugu katika maeneo mbalimbali nchini na kusababisha vifo vya watu, majeruhi na uharibifu wa mali za umma na watu binafsi, hali iliyotia doa sifa ya muda mrefu ya Tanzania kama kisiwa cha amani katika ukanda unaokabiliwa na misukosuko ya kisiasa.
Baada ya uchaguzi huo, Rais Samia amekuwa akisisitiza maridhiano, umoja, na uthabiti wa kiuchumi kama nguzo zisizotenganishwa katika safari ya kurejesha taifa, huku wakosoaji wakisisitiza kuwa uponyaji wa kweli unahitaji uwajibikaji, ukweli, na mageuzi ya kina.
Kuanzia kauli za Rais na mijadala bungeni, hadi mashaka ya upinzani, madai ya asasi za kiraia na wito wa viongozi wa dini, siku 100 za kwanza zinaonesha mafanikio fulani pamoja na mipasuko katika safari ya Tanzania kuelekea maridhiano ya kitaifa.
Katika kampeni za uchaguzi mkuu, Samia aliahidi katika siku 100 za kwanza, angeanza mchakato wa maridhiano ili kulileta taifa pamoja kutokana na makovu yatokanayo na uchaguzi.
Baada ya kuingia madarakani, kufuatia vurugu zilizotokea siku ya uchaguzi, Rais Samia ameunda tume ya kuchunguza matukio ya wakati na baada ya uchaguzi mkuu ambayo alisema ndiyo itasafisha njia kuelekea kwenye maridhiano.
Vilevile, Rais Samia amekuwa akitumia hotuba zake mbalimbali, hususan hotuba yake bungeni na mikutano ya kikazi, akisisitiza umoja kama msingi wa mustakabali wa kisiasa na kiuchumi wa Tanzania.
Katika hotuba yake ya mwisho wa mwaka, alitangaza maandalizi ya kuunda Tume ya Maridhiano ya Kitaifa kwa lengo la kuponya majeraha yaliyojitokeza wakati wa uchaguzi.
Ameonya mara kwa mara dhidi ya kuruhusu tofauti za kiitikadi na kisiasa kuvuruga maendeleo, akisema amani na mshikamano ni sharti la maendeleo ya kiuchumi.
Maridhiano yamefungamanishwa moja kwa moja na imani ya wawekezaji, utulivu wa kijamii, na malengo ya muda mrefu ya maendeleo ya Tanzania, ikiwamo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Vyama vya upinzani bado vina mashaka, vikihoji muda na dhati ya mpango wa maridhiano.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), John Heche, anaeleza mchakato huo kuwa “maridhiano ya hadaa,” akisema hayawezi kufanyika kwa maana halisi ilhali madai ya muda mrefu ya mageuzi ya mfumo wa uchaguzi bado hayajashughulikiwa.
“Ni dharau kuita haya maridhiano wakati Serikali ilipuuza makusudi wananchi, vyama vya siasa, na wadau wa demokrasia kuhusu haja ya mageuzi ya uchaguzi,” anasema.
Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, anasema maridhiano hayawezi kusonga mbele wakati bado kuna mahabusu wa kisiasa na uwajibikaji unaonekana kuchaguliwa.
“Hatuwezi kuingia kwenye maridhiano wakati bado kuna wafungwa wa kisiasa, wala hatuwezi kuendesha mchakato unaolenga kutafuta mbuzi wa kafara,” anasema.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Magdalena Sakaya, anataka uchunguzi huru wa mauaji yanayodaiwa kuhusishwa na vurugu za baada ya uchaguzi, akisema machungu bado yapo kwa kuwa mamlaka hazijakiri rasmi makosa.
Makamu Mwenyekiti wa NCCR–Mageuzi, Joseph Selasini, anahoji maridhiano yasiyoanzia kwenye ukweli:
“Maridhiano lazima yaanze kwa ukweli wa kilichotokea na baina ya nani na nani yanahitajika,” anasema.
Kwa jumla, vyama vya upinzani vinakubaliana kuwa maridhiano yanapaswa kuanzia kwenye haki ya uchaguzi, uwajibikaji, na mageuzi, badala ya kuwa ishara ya kisiasa isiyo na mizizi.
Wito wa amani, busara, maadili
Viongozi wa dini wameendelea kutoa wito wa utulivu, umoja, na uongozi wa kimaadili bila kuingiza siasa. Rais Samia amekiri mara kwa mara mchango wa viongozi wa dini katika kulinda amani na kuwataka kuhubiri umoja.
Ameonya pia dhidi ya kuingiza siasa katika dini, akisisitiza kuwa imani inalenga kuunganisha jamii.
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Lindi, Wolfgang Pisa, anatoa wito wa umoja wa kitaifa na tahadhari:
“Tuombe Bikira Maria atuombee ili taifa letu liwe na umoja na kila jambo lifanyike kwa manufaa ya nchi,” anasema, akionya misimamo mikali inaweza kudhoofisha umoja.
Viongozi wa kiislamu kupitia Baraza la Maimamu wamesisitiza kuwa maridhiano lazima yajengwe juu ya ukweli, uadilifu, na uwajibikaji. Katibu Mkuu, Sheikh Issa Ponda, anasema dosari za uchaguzi zinaonyesha haja ya haraka ya mageuzi na mazungumzo ya wazi.
“Jitihada za kujenga umoja wa kitaifa lazima zijengwe juu ya ukweli, uadilifu, na uwajibikaji wa mamlaka zote zilizohusika katika mchakato wa uchaguzi,” anasema, akionya kuwa bila mageuzi maridhiano yatabaki dhaifu.
Kwa ujumla, sauti za madhehebu mbalimbali zinakubaliana kuwa amani ni nyeti na inahitaji kulindwa kupitia uongozi wenye kuwajibika, maadili mema, na kuheshimu utu wa binadamu.
Asasi za kiraia na uwajibikaji
Asasi za kiraia (CSOs) zinasisitiza kuwa uponyaji wa kweli unahitaji uwajibikaji, heshima ya haki za binadamu, na ushiriki wa wananchi. Baada ya vurugu za uchaguzi, makundi ya haki za binadamu yameonya kuwa maridhiano yanaweza kuwa ya juu juu kama hayataegemezwa kwenye haki na ukweli.
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) wametaka hatua za kurejesha imani ya umma, zikiwamo kusitisha kukamatwa kiholela, uvamizi wa nyumba, na matumizi mabaya ya sheria za ugaidi. Pia, zilitaka maelezo ya watu wanaoripotiwa kupotea.
“Uhuru na haki si fadhila kutoka kwa walio madarakani; ni haki ya kila raia. Kuzilinda ni msingi wa utulivu wa taifa na amani ya kudumu,” zinasema taasisi hizo.
LHRC) kimesisitiza kuundwa kwa tume huru ya kimahakama kuchunguza vurugu za baada ya uchaguzi, kikisema uwajibikaji ni muhimu katika uponyaji. Tamwa pia ilisisitiza kuwa amani ya kudumu inahitaji kuheshimiwa kwa haki na uhuru wa kujieleza.
Mchambuzi wa siasa, Dk Paul Loisulie wa Chuo Kikuu cha Dodoma, anasema maridhiano yanapaswa kuwa ya taasisi, jumuishi, na yenye muundo, yakihusisha vyama vya siasa, viongozi wa dini, asasi za kiraia, na wataalamu. Anasema kuyatenga makundi muhimu, hususan vijana, kunadhoofisha uhalali wake.
“Maridhiano lazima yashughulikie udhaifu uliopo katika mfumo wa uchaguzi na kuhakikisha ushiriki mpana ili yalete utulivu wa kudumu,” anasema.
Mwanazuoni, Dk Onesmo Kyauke kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anasema ukweli ni msingi wa maridhiano na anatahadharisha kuhusu kutafuta mbuzi wa kafara:
“Maridhiano ya maana yanawezekana pale tu pande zote zinapokubali uwajibikaji na kuweka ukweli mbele kuliko lawama,” anasema, akibainisha kuwa maridhiano yanahitaji maelewano.
Profesa Makame Ali Ussi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) anaona maridhiano kama uwekezaji muhimu kwa amani ya muda mrefu, akionya kuwa malalamiko yasiyotatuliwa yanaweza kuharibu mshikamano wa kijamii:
“Maridhiano si ishara ya udhaifu; ni utambuzi kwamba utulivu wa taifa unahitaji mazungumzo, imani, na taasisi zenye kuaminika,” anasema.