MASHABIKI wa Yanga wamekuwa wanyonge baada ya kutoka sare nyumbani dhidi ya Al Ahly ya Misri na baadaye usiku wakaumizwa zaidi na ushindi wa AS Far Rabat lakini kocha wao, Pedro Goncalves amewatuliza huku akisema mchezo wao dhidi ya Wamorocco hao ni sawa na fainali.
Yanga imepata sare ya bao 1-1 dhidi ya Ahly kisha Far Rabat ikashinda nyumbani kwa bao 1-0 dhidi ya JS Kabylie, matokeo ambayo yameifanya Yanga kushuka mpaka nafasi ya tatu huku Wamorocco hao wakipanda nafasi ya pili kwa faida ya tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Akizungumza na Mwanaspoti kocha wa Yanga, Pedro amesema bado hesabu zao hazijaharibika kwenda robo fainali ingawa walitaka kushinda mbele ya Ahly.
Pedro amesema hawakuwa na bahati kupata matokeo ya ushindi na kwamba wachezaji wake walipambana vyema na sasa wanaanza hesabu za kuwafuata Far Rabat.
“Tulikwenda kutafuta ushindi hata maandalizi yetu yalilenga huko, lakini bahati mbaya tumepata pointi moja, hatuna chaguo zaidi ya kuyapokea matokeo hayo, tulikutana na timu kubwa Afrika lazima tuheshimu hilo,” amesema Pedro.
“Tunatakiwa tuchukue funzo la mchezo wa jana (juzi) na kubadilika haraka na kuanza kufikiria mchezo ujao, kundi letu ni gumu kama ambavyo nilisema kabla lakini nafasi yetu bado ipo kuweza kusonga mbele.
“Tuna kazi ya kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye mechi zetu mbili zijazo tukianza na Far Rabat, wameshinda jana (juzi) bahati nzuri kwao mechi hizi mbili watacheza wakiwa nyumbani tunatakiwa kwenda na akili ya ushindi hukohuko.
“Mchezo huo dhidi ya FAR Rabat ni sawa na kwamba tunakwenda kucheza fainali kuamua safari yetu ya kwenda hatua inayofuata, tukijua kwamba tukishinda tutafuzu.
Yanga jana asubuhi ilifanya mazoezi yake Zanzibar kisha ratiba hiyo itaendelea leo kabla ya kuanza safari ya kuwafuata FAR Rabat kwenye mchezo huo utakaopigwa Februari 7.
“Tuna safari ngumu tutakayotumia siku mbili mpaka kufika ndio maana unaona mazoezi yetu yameanza haraka, nafurahia kuona morali ya kutaka kushinda ilianza jana (juzi) kwa wachezaji wenyewe ambao waliumizwa na matokeo yale.
“Nimewaambia njia rahisi ya kuwapa nguvu mashabiki wetu wanaosafiri kokote tunakokwenda ni kuwatafutia ushindi wa pili kule Morocco kwangu mimi hili linawezekana.”