Arusha/Dar. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ameonya tabia ya vijana kujibizana na kuwakejeli wazee, akisema vitendo hivyo vinavunja heshima na ni hatari kwa maadili katika jamii.
Mtendaji mkuu huyo wa Serikali ambaye, kwa nafasi yake, ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), amesisitiza ni jambo la hatari kwa Taifa unapofika wakati vijana wanapata ujasiri wa kuwavunjia heshima wazee au viongozi wa kiroho.
Kauli ya Dk Mwigulu inakuja wakati ambao kumeshuhudiwa matukio mbalimbali ya vijana, hususan wa kisiasa na wanaharakati, kujibizana na wazee, wakati mwingine hata kutoleana lugha chafu.
Desemba 27, 2025, kundi la vijana lilijitokeza kumjibu Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Juda Ruwa’ichi, wakisema ametumia maneno machafu dhidi yao, kinyume na kile walichokiita mafundisho ya Yesu Kristo.
Majibu ya kundi hilo la vijana yalitokana na kauli ya Askofu Ruwa’ichi, aliyewataka vijana hao wapuuzwe kwa kuwa ni Wakatoliki bandia.
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba akisali katika Ibada ya Jumapili kwenye Kanisa Kuu la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati, Usharika wa Arusha Mjini, Februari 1, 2026. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
Sababu ya kiongozi huyo wa kiroho kusema hayo ni vijana hao kuandamana kwenda kumshitaki Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima, katika Ubalozi wa Vatican.
Vijana hao waliandamana kumpinga Padri Kitima wakisema haenendi vema katika uongozi wake ndani ya baraza hilo, kwa kuwa anatoa kauli zinazofarakanisha badala ya kuunganisha.
Mbali na hilo, Januari 17, 2026, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenan Kihongosi, alimjibu Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, akimtaka asiwe na chuki kwa viongozi waliopo.
“Warioba amekutana na Rais siku nne hazijapita, yupo tena mtandaoni. Sasa inasikitisha kidogo, lakini tunachomuomba ni kwamba astaafu vizuri, aendelee kupumzika lakini asiwe na chuki kwa viongozi waliopo, kwa sababu ana uwezo wa kushauri na kufika katika mamlaka husika na kuweza kuishauri kwa hekima kuliko kwenda kulalamika kwenye mitandao,” alisema Kihongosi.
Majibu ya Kihongosi yalitokana na swali aliloulizwa na mwandishi wa habari, likimtaka atoe msimamo wa CCM kuhusu kilichozungumzwa awali na Jaji Warioba. Kauli ya Warioba iliishutumu Serikali kuwa imechangia vurugu zilizotokea wakati wa uchaguzi mkuu, Oktoba 29 na anavyoona ni kama viongozi wamewaacha polisi watawale.
Julai 2019, akiwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ali Hapi, ambaye sasa ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, aliahidi kuwajibu wazee kila watakapotoa kauli dhidi ya Rais wa wakati huo, hayati John Magufuli.
“Bingwa wa kuendesha shughuli za Serikali ni mwanasiasa aliyestaafu akachunga ulimi wake. Wakae kimya zama zao zimepita, mazuri waliyofanya kwa nchi yetu tunawashukuru, wasituharibie nchi yetu. Popote watakapojitokeza tutawatwanga, hatutawaacha hivi hivi kamwe,” alisema.
Hao ni wachache kati ya wengi waliowahi kujibizana na wazee kupitia majukwaa ya kisiasa na imani za dini.
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba akizungumza katika Ibada ya Jumapili kwenye Kanisa Kuu la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati, Usharika wa Arusha Mjini, Februari 1, 2026. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
Leo, Jumapili Februari Mosi, 2026, Dk Mwigulu ametoa kauli hiyo alipozungumza wakati wa ibada iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, Usharika wa Arusha Mjini, Kanisa Kuu (Cathedral).
Amesema tabia hiyo ya vijana kuingiliana na kujibizana na wazee kwa misingi ya imani za kidini ni hatari na inavunja heshima.
“Ni jambo la hatari kwenye Taifa watu wakiwa na ujasiri wa kufanya kitu ambacho kinavunja heshima dhidi ya Askofu, watu wakakejeli mpaka viongozi wa dini, Sheikh au Mufti. Ni jambo la hatari. Mzee anatokea, mzee mtu mzima, mstaafu au ambaye kwa rika hulingani naye amesema jambo, unajibu kama ni mwanarika mwenzako,” amesema.
Amewataka vijana hao wasitumie kigezo cha siasa kuwajibu wazee hao akisema: “Anatokea tu mzee amefanikiwa katika shughuli zake, tena halazimiki kusema alifanyaje. Naweza nikatoa hata mfano kwa sababu siyo jambo baya kutolea mfano mzee tunayemheshimu.”
Amemtolea mfano Mwenyekiti wa Kampuni ya Azam, Said Salim Bakhresa, akisema anaeleza alikopita kwa kuuza bidhaa mbalimbali ndogo hadi kufikia kuwa mwekezaji, lakini anatokea kijana anaandika kukejeli.
Dk Mwigulu amesema wengine wanaandika vitu hata wasivyovijua, baadhi wanawajibu hata wataalamu wa mambo kama sheria, ilhali wao hawana taaluma hizo.
“Jambo la kiuchumi yeye yuko tu pale anamjibu Gavana wa Benki Kuu, Profesa wa uchumi. Huu uharaka wa kuandika kila kitu unakuta neno limetolewa na kiongozi wa kiroho anajibu kama anamuongelea mwizi wa mtaani. Haya si mambo mazuri kwa uelekeo wa Taifa letu,” amesema.
Amesema ni hatari vijana wanapojibizana na viongozi wa kiroho kwa sababu wanaheshimiwa na wengine, hivyo ni muhimu kuwa na tahadhari.
“Kama una maoni mazuri sana, kaongelee kuhusu imani yako chumbani kwenye kikao chenu. Ongeeni hapo kama mnavyopanga kuhusu jengo, mnaweza kukaa kama kamati ya ujenzi mkazungumza, lakini usiguse imani ya mwenzako anayoiamini,” amesema.
Amesema watu wakizidi kuingiliana kwenye imani, hapatakuwa na mshindi kwa sababu kila mtu jambo moja analoapa kulifia ni lile la kumpeleka mbinguni.
Aidha, kiongozi huyo ameziomba taasisi za dini, viongozi wa rika na jamii kuwekeza katika malezi ya vijana na watoto, akisema matokeo hasi yameanza kuonekana kwenye malezi ya vijana hao.
Amesema zamani malezi yaliyokuwa yakitolewa kwa vijana na watoto yamesaidia hadi sasa Taifa lina watu wanaoheshimiana, hawabaguani kwa kabila, dini au vipato.
“Hili ulilosema baba Askofu liwe roho kwa taasisi za dini kuwaasa vijana wa Tanzania, kuwaasa Watanzania kuwekeza katika malezi ya watoto wetu na vijana wetu. Kuna mahali tumelegea kwenye malezi ya watoto na vijana wetu, na tumeanza kuona matokeo hasi yakitokea,” amesema.
Katika hatua nyingine, akiwasilisha salamu za Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu ujenzi wa kanisa hilo, Dk Mwigulu amesema amechangia Sh50 milioni huku yeye mwenyewe akichangia Sh20 milioni kwa ajili ya ujenzi huo.
Washiriki wa Ibada ya Jumapili kwenye Kanisa Kuu la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati, Usharika wa Arusha Mjini, wakimsikiliza Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba alipozungumza, Februari 1, 2026. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
Alichokisema Askofu Mollel
Awali, Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dk Godson Mollel, amewataka Watanzania kutambua kuwa kila mamlaka imewekwa na Mungu, hivyo ni vyema kuziheshimu na pale kunapokuwa na hoja ni vyema ikawasilishwa kwa staha na heshima.
“Nimesema mara nyingi na leo nasema tena, tuheshimu mamlaka. Neno la Mungu linatufundisha hivyo. Nimefundisha vijana zaidi ya mara 10, narudia tena, tuheshimu mamlaka na kama una hoja, toa kwa staha na heshima ili iwe na matokeo. Tuombe pia kwa mamlaka, wamebeba mzigo mkubwa sana,” amesema.
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba akiwa katika picha ya pamoja na Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Kati ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dkt. Godson Abel Mollel na viongozi wa Mkoa wa Arusha baada ya kushiriki Ibada ya Jumapili kwenye Kanisa Kuu la KKKT Usharika wa Arusha Mjini, Februari 1, 2026. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
Akizungumzia kauli hiyo ya Dk Mwigulu, mchambuzi wa siasa, Profesa Abel Kinyondo, amesema inaashiria mchanganyiko, kwanza kusaidia kurejesha maadili ya vijana kutowajibu wazee, kwa kuwa upo usemi usemao wazee hawakosei.
Amesema kauli ya Dk Mwigulu ikiangaliwa kwa undani, inaibua shida, kwani anazungumza baada ya nani kusemwa, kwa kuwa vijana walimsema Jaji Warioba.
Amesema waliomsema Jaji Warioba walikuwa upande wa CCM na wengine walimsema Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Julius Nyerere, Joseph Butiku.
Profesa Kinyondo amesema baada ya Jaji Warioba kusemwa hakuna kauli yoyote iliyotolewa, lakini sasa baada ya Butiku kuzungumza na mazungumzo yake kukosolewa ndipo tamko hilo linaibuka, na linazua maswali ni aina gani ya wazee wanapaswa kusikilizwa.
“Inakuwa ni jambo zuri akisema waheshimuni wazee, lakini kama ni kwa ujumla tu kwamba waheshimuni wazee, anapaswa kumtetea Warioba, maana alianza kuongea akatukanwa pande zote na hakutetewa.
“Mzee aliyeongea hivi karibuni ni Butiku, na anaonekana ndiyo aina ya wazee anaowazungumzia Waziri Mkuu. Kama ndicho anachofanya, analeta mkanganyiko. Ingekuwa vizuri wazee wakiongea ni utamaduni wetu kuwaheshimu wazee wote, hata wanachozungumza tukiona kipo sawa au hakipo sawa,” amesema.
Kwa upande wa Mwalimu Samson Sombi, amesema tamko hilo ni la Serikali na Watanzania hawana utamaduni wa kuwajibu vibaya wazee, bali hata kuwasahihisha kuna utaratibu.
“Lazima tuangalie haijalishi kama mzee amekosea, tuwe na utamaduni wa Kitanzania. Mtu akitoa maoni yake tofauti na wengine wanavyofikiri, aendelee kuheshimiwa. Tusipende kuwatolea maneno makali ya kuwavunjia heshima,” amesema.