Shinyanga. Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amezindua ndege ya kisasa ya utafiti wa kijiolojia wa anga, itakayosaidia shughuli za utafutaji wa madini kwa kutumia teknolojia ya juu.
Ndege hiyo itakayoruka mita 30 kutoka usawa wa uso wa ardhi, mali ya kampuni ya Barrick, itaongeza usahihi wa upatikanaji wa miamba iliyo chini ya ardhi, kupunguza athari za kimazingira na kuboresha ufanisi wa shughuli za utafutaji wa madini nchini.
Waziri Mavunde amezindua ndege hiyo leo Februari Mosi, 2026 katika eneo maalumu la uwekezaji la Buzwagi, Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga kuashiria kuanza rasmi kwa utafiti utakaofanywa na kampuni ya Barrick kwa ajili ya uanzishwaji wa mgodi mpya.
Amesema utafiti huo utakaofanywa na Barrick utahusisha helikopta kuruka katika maeneo ya Msalala, Nzega, Igunga, Mbogwe na Nyangh’wale kwa lengo la kupata taarifa zitakazosaidia uanzishwaji wa mgodi huo.
Waziri huyo amesema kwa maeneo ambayo Barrick itafanya utafiti na kubaini kuwa hayakidhi vigezo vya uchimbaji mkubwa, yatagawiwa kwa wachimbaji wadogo ili kuwaongoza na kuondokana na uchimbaji wa kubahatisha.
Waziri wa madini Anthony Mavunde akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa ndege ya utafiti wa kina wa kijiolojia wa anga, leo februari 1, 2026 wilayani Kahama mkoani Shinyanga.
Amesema Serikali katika kuhakikisha inaongeza ukubwa wa eneo la utafiti, katika mwaka huu wa fedha 2025/26 na mwaka ujao 2026/27, itarusha ndege itakayofikia eneo la kilomita 165,874, sawa na asilimia 18 ya Tanzania nzima, kwa ushirikiano na Umoja wa Ulaya.
“Pamoja na kazi inayofanywa na Barrick hapa, Serikali katika mwaka 2025/26 na 2026/27 tutarusha ndege itakayofikia eneo la kilomita za mraba 165,874 sawa na asilimia 18 ya nchi yetu ya Tanzania. Huu ni mradi tutakaofanya kwa pamoja na wenzetu wa umoja wa Ulaya,” amesema.
Ameongeza kuwa: “Lakini hatua ya pili ya kuhakikisha tunaongeza eneo kubwa zaidi la utafiti, Rais Samia Suluhu Hassan amesharidhia, tuko katika mchakato wa hatua za kukamilika ununuzi wa helikopta itakayokuwa chini ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST), itakayosaidia kufanya utafiti wa kina na kuongeza maeneo mengi zaidi.”
Awali, Meneja Mkazi wa Kampuni ya Barrick Tanzania, Dk Melkiory Ngido amebainisha kwamba tangu ianze shughuli zake hapa nchini mwaka 2020, imewekeza zaidi ya Sh100 bilioni kwenye utafiti wa kina wa madini, ambapo kupitia migodi mitatu inayoiendesha imeweza kuzalisha zaidi ya Sh14 trilioni kwenye mzunguko wa uchumi wa ndani.
“Tangu Barrick ilipoanza uzalishaji mwaka 2020, kampuni yetu imewekeza zaidi ya Sh100 bilioni, zote zimeenda kwenye utafiti wa kina kwenye migodi ya Barrick iliyopo na maeneo ya nje ya migodi. Ni jukumu letu kushirikiana na Serikali ili kutafuta sehemu nyingine tutakayojenga mgodi mpya.”
Ndege ya utafiti wa kina wa kijiolojia wa anga iliyozinduliwa leo februari 1, 2026 wilayani Kahama mkoani Shinyanga na waziri wa madini Anthony Mavunde, ikifanya jaribio la kuruka.
Mbunge wa Kahama Mjini, Benjamin Ngayiwa pamoja na mwenzake wa Msalala, Mabula Magangila wameishukuru Serikali kwa namna inavyowezesha uwekezaji wilayani Kahama na kwamba matarajio ya wananchi ni kupata ajira na kuwainua kiuchumi, kupitia miradi itakayokwenda kuanzishwa kwenye maeneo yao.
Hii ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa Serikali kuhakikisha inafikia lengo la kuongeza eneo la utafiti kufikia asilimia 50 ifikapo 2030.