Dar es Salaam. Uamuzi wa Serikali kutangaza mpango wa kuuza sehemu ya akiba ya dhahabu umeibua mjadala mpana miongoni mwa wachumi, huku wakisisitiza kuwa hatua hiyo haina tatizo iwapo fedha zitakazopatikana zitaelekezwa kwenye miradi yenye tija kwa maendeleo ya Taifa na kulinda uthabiti wa uchumi.
Wataalamu hao wameeleza kuwa, katika mazingira ya mabadiliko ya uchumi wa dunia na kupungua kwa vyanzo vya nje vya fedha, matumizi ya akiba ya dhahabu au fedha za kigeni ni sehemu ya maamuzi ya sera, si jambo la dharura wala la hatari.
Mjadala huo umeibuka siku chache baada ya vyombo vya habari vya kimataifa kumnukuu Waziri wa Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, akisema Serikali ipo mbioni kuuza sehemu ya dhahabu zake ili kugharamia miradi ya maendeleo.
Hata hivyo, taarifa hiyo ilifafanuliwa baadaye na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ikieleza kuwa mpango wa kuuza dhahabu unafanyika kwa kuzingatia misingi ya sera ya usimamizi wa akiba ya Taifa, hasa ikizingatiwa kupungua kwa misaada ya maendeleo kutoka baadhi ya nchi za Magharibi.
Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha wa BoT, Emmanuel Akaro, amesema benki hiyo huweza kuuza sehemu ya dhahabu si kwa shinikizo, bali kama sehemu ya kubadilisha aina ya mali (asset rebalancing), ikiwemo kununua dola za Marekani.
“Ni kweli kuna mpango wa kuuza dhahabu, lakini tumefikia kiwango tulichokusudia kiwe kwenye mizania yetu, ambacho ni Dola za Marekani bilioni mbili kama kiwango elekezi. Tunapozidi kiwango hicho, kuna vihatarishi, hivyo tunalazimika kuuza kulingana na hali ya soko,” amesema Akaro.
Ufafanuzi mwingine ulitolewa bungeni na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, aliyesema BoT, kama msimamizi wa sera za fedha, wakati mwingine hutumia zana zake za kifedha kudhibiti mfumuko wa bei kwa kupunguza fedha zilizo kwenye mzunguko.
Amesema hatua za BoT katika ununuzi wa dhahabu zimewasaidia kwa kiasi kikubwa wachimbaji wadogo, huku akisisitiza kuwa mpango wa Serikali wa kuimarisha hifadhi ya dhahabu ni sehemu ya dira ya Rais Samia Suluhu Hassan.
“Haya ni maamuzi ya kisera. Tunataka kuendelea kununua dhahabu hata iwe nyingi ili tulingane na mataifa mengine. Haya si mambo ya mtaani, ni maamuzi ya kitaifa,” amesema Dk Mwigulu.
Akitoa mtazamo wake, mtaalamu wa uchumi, Dk Said Mzee, amesema kila nchi huwa na malengo maalumu katika kuhifadhi akiba ya dhahabu au dola, na inapofikia kiwango kilichopangwa, ziada inaweza kuuzwa kwa ajili ya maendeleo.
“Hakuna hasara kuuza, isipokuwa kama fedha zitakazopatikana zitapelekwa kwenye matumizi yasiyo na tija,” amesema Dk Mzee.
Ameongeza kuwa, kwa muda mrefu, dhahabu imekuwa ikionekana kuwa salama zaidi kuliko dola, kwa kuwa thamani ya dola hupanda na kushuka, ilhali dhahabu mara nyingi hudumisha thamani yake; ndiyo maana nchi zenye uchumi imara huweka akiba kubwa ya dhahabu.
Kwa upande wake, mchumi Oscar Mkude amesema lengo kuu la nchi kuhifadhi dhahabu au dola ni kulinda uthabiti wa thamani ya sarafu ya ndani.
Amesema Benki Kuu hutumia akiba hiyo kuongeza dola kwenye mzunguko pale inapobaini upungufu, ili kuzuia shilingi kushuka thamani dhidi ya dola.
“Dhahabu ni kinga ya uchumi. Ikitokea shilingi inaanza kuyumba, dhahabu hutumika kama ngao kwa sababu duniani kuna siasa za kuporomosha sarafu za baadhi ya nchi,” amesema.
Mkude ameongeza kuwa Serikali hutunza dhahabu pia kwa lengo la kulinda sekta ya madini, akieleza kuwa katika nyakati ambazo bei ya soko ni ndogo, Serikali inaweza kununua dhahabu kwa bei nzuri kwa wachimbaji wake, kisha kuiuza baadaye soko linapopanda.
Kwa nchi zinazoendelea, amesema ni busara zaidi kutumia akiba ya dhahabu badala ya kukopa, mradi hatua hiyo iwe ya muda na yenye mpango wa kurejesha akiba hiyo baadaye.
“Hatari ni pale ambapo dhahabu itauzwa bila mkakati wa kuirudisha. Hapo ndipo nchi inapoteza uwezo wa kujilinda siku zijazo,” amesema.
Naye Profesa Aurelia Kamuzora amesema kupunguza akiba ya dhahabu au fedha za kigeni kuna faida, akifananisha na namna familia inavyotunza na kutumia akiba yake.
“BoT inatunza fedha kwa niaba ya Watanzania. Tukizalisha zaidi tunatunza zaidi, tukipata changamoto tunatumia akiba ili kuendelea na shughuli zetu,” amesema.
Amesema iwapo dhahabu inauzwa kugharamia miradi ya maendeleo, faida yake itaonekana moja kwa moja kwa wananchi kupitia miundombinu bora, gharama ndogo za usafirishaji na ukuaji wa uchumi.
“Fedha zinatunzwa ili zije zitumike. Kama unazitunza nyumbani bila mpango wa kuwekeza, hazina faida,” amesema.
Akitoa mtazamo tofauti, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Godbless Lema, kupitia mtandao wake wa X, amehoji mantiki ya kuuza dhahabu wakati ambapo dunia inakabiliwa na misukosuko ya kisiasa na kiuchumi.
Amesema dhahabu si mali ya kufanyia biashara, bali ni kinga dhidi ya kuporomoka kwa thamani ya sarafu nyingine.
“Kuuza kwa sababu thamani imepanda ni sawa na kuuza bima/kinga kabla hatari haijatokea. ‘Central banks’ makini huongeza dhahabu inapopanda bei, si kuuza,” amesema.
Pia, aliyekuwa Waziri wa Ardhi zamani, Profesa Anna Tibaijuka, akizungumza na Crown TV, amesema dhahabu ni mtaji wa Taifa na uamuzi wa kuinunua kuanzia mwaka 2023 ulikuwa sahihi.
Amesema hoja si kuuza au kutouza dhahabu, bali ni namna Serikali inavyosimamia matokeo ya mauzo hayo.