SAFARI ZA SGR KUSITISHWA PALE USALAMA UNAPOKUWA HATARINI

::::::::::

Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amewahakikishia Watanzania kuwa Serikali haitafanya mchezo na usalama wa abiria wanaotumia Reli ya Kisasa (SGR), huku akisisitiza kuwa uamuzi wa kusitisha safari nyakati za changamoto za kibiashara au kimazingira unalenga kulinda maisha ya watu.

Akizungumza na waandishi wa habari katika mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma, February mosi,2026 Prof. Mbarawa amesema reli hiyo imejengwa kwa viwango vya juu vya kimataifa, ikihusisha miundombinu imara ikiwemo madaraja yenye kina kirefu kwenda chini.

Waziri Mbarawa amebainisha kuwa, licha ya ubora wa reli hiyo, taratibu za kiusalama zinataka operesheni kusitishwa mara moja pindi kunapojitokeza viashiria vya hatari kama mvua kubwa au upepo mkali.

“Usalama wa Watanzania na mali zao ndio kipaumbele chetu cha kwanza (first priority). Tukiona kuna changamoto yoyote, ni lazima tusimamishe safari ili kuhakikisha usalama wa abiria wetu,” alisema Prof. Mbarawa.

Katika hatua nyingine, Waziri Mbarawa ameipongeza Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa kuendelea kusimamia miundombinu hiyo kwa umakini na kuwataka wasilegeze kamba katika kuhakikisha reli hiyo inabaki kuwa salama wakati wote.

SGR ya Tanzania inatajwa kuwa moja ya miradi mikubwa ya kimkakati inayolenga kuleta mapinduzi ya kiuchumi na usafirishaji nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.