Dar es Salaam. Wakati matokeo ya kidato cha nne 2025 yakionyesha kuongezeka kwa ufaulu kufikia asilimia 94. 98, nusu ya watahiniwa hao wamepata daraja la nne na sifuri.
Kwa mujibu wa matokeo hayo yaliyotangazwa Januari 31, 2025 na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Profesa Said Mohamed watahiniwa takribani 271,216 sawa na asilimia 48.92 walipata daraja la nne.
Kati ya watahiniwa hao waliopata daraja la nne wasichana ni 158,380 sawa na asilimia 53.68 na wavulana wakiwa 112,836 sawa na asilimia 43.49.
Hata hivyo, idadi hiyo ni pungufu kidogo ukilinganisha na asilimia 49.41 ya mwaka 2024 kwa wahitimu waliopata daraja la nne.
Pia, katika matokeo hayo watahiniwa takribani 27,838 walipata daraja sifuri sawa na asilimia 5.02, kati ya hao wasichana ni 16,924 sawa na asilimia 5.74 na wavulana ni 10,914 sawa na asilimia 4.21.
Kwa idadi hiyo inafanya wanafunzi waliopata ufaulu wa daraja nne na sifuri kufikia asilimia 53.94. ambayo ni juu kidogo ya nusu ya watahiniwa.
Vilevile katika uchanganuzi wa matokeo hayo unaonyesha kuwa watahiniwa wa shule waliopata ubora wa ufaulu katika madaraja ya kwanza hadi tatu ni 255,404 sawa na asilimia 46.06.
“Mwaka 2024 watahiniwa waliopata ufaulu wa madaraja ya I- III walikuwa 221,953 sawa na asilimia 42.96. Hivyo, ubora wa ufaulu umeongezeka kwa asilimia 3.10 ikilinganishwa na mwaka 2024.” inaeleza taarifa hiyo.
Vilevile ubora wa ufaulu wa madaraja ya kwanza hadi tatu ni mzuri zaidi kwa wavulana ikilinganishwa na wasichana ambapo wavulana ni 135,676 sawa na asilimia 52.30 ya wavulana wote wenye matokeo.
Wasichana ni 119,728 sawa na asilimia 40.58 ya wasichana wote wenye matokeo.
Akitoa maoni yake kuhusu ufaulu huo, mtafiti wa elimu, Dk Muhanyi Nkoronko amesema ufaulu karibu ya nusu ya watahiniwa waliofaulu kupata daraja la nne kunasababishwa na masuala ya kimazingira, kimfumo na wanafunzi wenyewe husika.
Amesema baadhi ya wazazi kwa kipindi cha sasa wamepunguza ufuatiliaji na kutilia mkazo elimu ya watoto wao.
Amesema hiyo inachangia wanafunzi kutofaulu vizuri zaidi kutokana na kukosekana kwa ufuatiliaji wa wazazi.
Vilevile amesema mwenendo wa baadhi ya wahitimu kupendelea zaidi kwenda vyuo vya kati baada ya kuhitimu inachangia hilo.
Anasema hilo linachangia baadhi ya wanafunzi kupambana kupata ufaulu utakaowawezesha kudahiliwa katika vyuo hivyo kuliko ule wa kuwawezesha kwenda kidato cha tano.
“Baadhi yao wanapambana kupata D nne ambayo inaangukia katika ufaulu wa daraja la nne ili wapate vigezo vya kudahiliwa katika vyuo hivyo”amesema.
Pia, ameongeza kuwa licha ya hamasa kubwa iliyopo ndani ya jamii kuhakikisha watoto wa kike wanapata elimu, bado baadhi ya watu bado wana dhana potofu juu ya kumuelimisha mtoto wa kike.
Amesema baadhi yao wanaamini mtoto wa kike akipata elimu kidogo inamtosha, kwani hatakiwi kusoma sana kwa kuwa ataishia kuolewa.
“Dhana hiyo inaweza kuathiri hata ujifunzaji wa mwanafunzi husika kufanya juhudi ya kufaulu zaidi ili kuendelea na ngazi za juu katika elimu,” amesema.
Naye mchambuzi wa Elimu, Mussa John amesema takribani ya nusu ya watahiniwa waliofaulu kuangukia daraja la nne, kunaonesha uelewa wa wanafunzi haujaimarika kutokana na wanafunzi kukariri ili wapatikane kwenye madaraja ya ufaulu.
Mdau wa Elimu na Mkuu wa Shule ya Sekondari Kosiryamu, Clinton Weston amesema ili wanafunzi wengi waweze kufaulu katika madaraja ya juu zaidi yaani daraja la kwanza hadi la tatu, ni muhimu mwanafunzi kuendelea kutengenezewa mazingira wezeshi ya ujifunzaji.
Anasema mazingira hayo ni pamoja na uwepo wa madarasa ya kutosha, walimu, maktaba pamoja na maabara yenye vifaa vyote muhimu.
“Vilevile ni muhimu kuwasaidia wanafunzi hawa wasitembee umbali mrefu kwenda shuleni na kurudi nyumbani kwani hili pia linachangia wanafunzi kutofanya vizuri.
“Shule ambazo ziko mbali kidogo na makazi ya watu ni vyema zikajengewa mabweni ambayo yatawasaidia wanafunzi wanaotoka mbali kuwa karibu na shule,” amesema.
Pia, amesema wazazi pamoja na walimu wana jukumu la kuhakikisha wanamwezesha mtoto kujitambua na kufahamu umuhimu wa elimu katika maisha yake.
Amesema hiyo itamsaidia mwanafunzi kuweka malengo na kufanya juhudi ya kusoma kwa bidii ili aweze kufikia ndoto zake.
Vilevile amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wazazi pamoja na walimu ili kumwezesha mwanafunzi kufaulu vizuri.
Hisabati na biolojia bado changamoto
Ingawa kiwango cha ufaulu wa jumla kimeimarika, ufaulu katika masomo ya msingi kama vile hisabati bado umeendelea kuwa changamoto.
Mwaka 2025, ni asilimia 26.45 pekee ya watahiniwa waliopata ufaulu huku katika somo la biolojia kiwango cha ufaulu kilishuka hadi asilimia 65.68 kutoka asilimia 74.15 mwaka 2024, huku ni asilimia 24.92 pekee ya watahiniwa waliopata madaraja ya ubora (A hadi C), ikishuka kutoka asilimia 40.04 mwaka uliotangulia.
“Mwelekeo huu unatia wasiwasi,” alisema mtaalamu wa elimu ya sayansi, Profesa Joseph Mwakalobo na kuongeza: “Hisabati ni msingi wa ujifunzaji katika fizikia, kemia, biolojia na teknolojia.
Amesema kutofanya vizuri katika somo la hesabu hupunguza uwezo wa wanafunzi kufanya vizuri katika maeneo mengine.
“Vivyo hivyo, kushuka kwa biolojia kunaonesha upungufu katika uelewa wa dhana ambazo zinaweza kuathiri sekta za afya, kilimo na sayansi huko baadaye,” amesema.
Matokeo pia yanaonesha kile kinachowezekana pale mazingira ya ufundishaji, rasilimali na ujifunzaji wa vitendo vinapokuwepo.
Wataalamu wanasema kuziba mapengo haya kunahitaji zaidi ya kuzingatia mitihani pekee.
“Tunahitaji uwekezaji endelevu katika mafunzo ya walimu, vifaa bora vya kufundishia na muda zaidi kwa ujifunzaji wa vitendo na marejeo ya ziada.
“Ushirikiano wa jamii, programu za uhamasishaji na hatua maalumu kwa wasichana ni muhimu pia kufunga pengo linaloendelea kuwepo.”amesema Johnson.