Njiapanda: Udumavu washamiri Iringa licha ya kusheheni chakula -1

Iringa. Wakati kiwango cha udumavu nchini Tanzania kikiwa juu ya wastani wa dunia wa asilimia 22, Mkoa wa Iringa ni miongoni mwa mikoa yenye viwango vya juu zaidi, ikiwa na asilimia 56.9, licha ya kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa chakula nchini.

Kulea watoto maeneo ya kazi na kuwapa vileo walio chini ya umri wa miaka mitano kumechangia kuwepo kwa kiwango hiki kikubwa cha udumavu miongoni mwa watoto mkoani Iringa, uchunguzi wa Mwananchi umebaini.

Iringa ina idadi kubwa ya watoto waliodumaa chini ya umri wa miaka mitano, licha ya kuwa miongoni mwa mikoa inayozalisha chakula kwa wingi nchini Tanzania.

Watoto huchukuliwa kuwa wamedumaa iwapo urefu wao, kulingana na umri, uko chini kwa zaidi ya viwango viwili vya kawaida ikilinganishwa na wastani uliowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Sababu za udumavu ni lishe duni kabla na wakati wa ujauzito, katika hatua za awali za utoto, maambukizi ya mara kwa mara, pamoja na ukosefu wa msisimko wa kisaikolojia, hali inayoathiri ukuaji na maendeleo ya mtoto.

Takwimu za Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto Tanzania wa mwaka 2022 (TDHS-MIS) zinaonesha kuwa udumavu unaathiri asilimia 56.9 ya watoto chini ya miaka mitano mkoani Iringa, ukifuatiwa na Njombe kwa asilimia 50.4 na Rukwa kwa asilimia 49.8. Kati ya watoto waliodumaa Iringa, asilimia 17.3 wameainishwa kuwa na kiwango kikubwa cha udumavu.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi katika Manispaa ya Iringa, Wilaya ya Kilolo na Iringa Vijijini kati ya Oktoba na Desemba 2025 umebaini kuwa lishe si sababu pekee ya utapiamlo unaohusisha udumavu, kukonda na uzito mdogo.

Imebainika kuwa sababu nyingine ni jinsia ya mtoto, umri, uzito wa kuzaliwa na uwiano wa uzito na urefu wa mwili, mtindo wa unyonyeshaji, elimu ya mama, mahudhurio ya huduma stahiki za kliniki ya wajawazito, usafi na hali ya kiuchumi ya kaya.

Udumavu huwanyima watoto fursa tangu wakiwa wadogo hadi utu uzima, kwani baadhi hushindwa kufikia urefu au uwezo kamili wa kiakili.

 Mara nyingi watoto walioathiriwa na udumavu hukumbwa na changamoto za kushindwa kufikia malengo ya kitaaluma wawapo shuleni, hupata kipato kidogo wakiwa watu wazima, hushindwa kukabili vikwazo vya kijamii na kuwa katika hatari kubwa ya kupata magonjwa yasiyoambukiza.

Mbali na sababu za kisayansi zinazoainishwa, imebainika katika uchunguzi kuwa uelewa mdogo wa lishe miongoni mwa kinamama au walezi, pamoja na shinikizo la kiuchumi na kijamii, huzidisha tatizo la udumavu mkoani Iringa.

Kinamama na walezi wengi hujikuta njiapanda wanapotakiwa kuchagua ama kubaki nyumbani kulea watoto ili kuwapatia chakula chenye lishe kwa utaratibu unaokubalika au kujikita katika shughuli za kuwaingizia kipato.

Kwa kuzingatia umuhimu wa yote mawili, imebainika katika uchunguzi kuwa wengi huchagua kulea watoto maeneo yao ya kazi, ambako hushindwa kuwapatia lishe sahihi inayopendekezwa kwa muda husika, hali inayochochea kukithiri kwa udumavu.

Hali hii inakiuka Kifungu cha 17 na 20 cha Sheria ya Mtoto (Sura ya 13), Kifungu cha 3 na 4 cha Sheria ya Chakula na Lishe Tanzania (Sura ya 109), pamoja na Mpango Jumuishi wa Pili wa Taifa wa Lishe (2021/22–2025/26).

Sheria na mpango huo vinawataka maofisa lishe na ustawi wa jamii kuhakikisha watoto wanalelewa ipasavyo na kupata mlo unaochochea ukuaji na ustawi.

Vilevile, maofisa hao wanaelekezwa kutekeleza afua za chakula na lishe zilizobainishwa katika mipango ya maendeleo ya taifa na kushirikiana na wadau wengine kulinda ubora wa chakula.

Hatua hizi zinalenga kuhakikisha ukuaji bora wa mtoto, kumsaidia kufikia uwezo kamili na kukuza programu endelevu za lishe zinazochangia ustawi wa mtu binafsi na maendeleo ya Taifa.

Uchunguzi umebaini wanawake wengi wamekuwa wakifanya kazi shambani, sokoni, vilabu vya pombe za kienyeji, ulinzi, mama lishe, kufua nguo, biashara ya nguo na kazi nyinginezo. Baadhi yao wameeleza huamka mapema kuandaa uji unaotokana na ulezi, mahindi na ndizi kabla ya kwenda kazini.

Kwa mujibu wa baadhi ya kinamama, hunyonyesha mara kwa mara, lakini wakati mwingine huwapa watoto vyakula wanavyonunua kwa mama lishe, hasa wanapoishiwa kilichoandaliwa nyumbani, licha ya kuwa huandaliwa kwa ajili ya watu wazima na hakikidhi mahitaji ya lishe ya mtoto.

Katika Soko la Mlandege, Manispaa ya Iringa, mfanyabiashara ambaye hakutaka jina lake litajwe anasema hunyonyesha mwanaye wa miezi minane baada ya kuamka, na kuna wakati hushindwa kufanya hivyo anapozidiwa na wateja.

“Hakuna mtu wa kubaki na mtoto, nikikaa nyumbani sitafanya biashara, hivyo nitashindwa kuilisha familia yangu,” anasema, akieleza humpa mtoto uji kama chakula cha ziada.

Beatrice (si jina halisi) anasema hana ndugu wa kubaki na mtoto, huku mumewe akifanya kazi katika kampuni ya ujenzi.

 “Sina kipato cha kuajiri mfanyakazi wa ndani. Kwa hiyo, nalazimika kumchukua mwanangu ninapokuja kwenye shughuli zangu. Huwa namnyonyesha na kumpa chakula cha ziada ninachokiandaa nyumbani,” anasema Beatrice, anayefanya kazi ya ulinzi katika shule ya msingi iliyopo Mtaa wa Mkimbizi.

Anasema amekuwa akienda kazini na mtoto wake tangu alipokuwa na miezi mitatu, wakati ambao anatakiwa kunyonya maziwa ya mama pekee. Anaeleza huamka alfajiri na kuandaa uji anaoubeba kwenye chupa, ambao humywesha.

Mfanyabiashara katika Soko la Kihesa, Christina Chatanda, ambaye ni mama wa watoto wawili, anasema uwezo wake ni kununua sembe na mbogamboga anazouza sokoni, lakini hawezi kununua mayai, nyama wala maziwa. “Nilipata mafunzo kliniki wakati wa ujauzito. Kujua ninachopaswa kumpa mwanangu na uwezo wa kununua ni mambo mawili tofauti,” anasema.

“Mlezi anaweza kutumia Sh2,000 kununua maandazi ili watoto washibe, badala ya kununua mayai kwa gharama hiyo hiyo,” anaunga mkono mfanyabiashara mwenzake, Mzee Anthony.

Anasema: “Familia nyingi huuza vyakula vyenye lishe, lakini hushindwa kuzipa familia zao vyakula vya namna hiyo. Badala yake huishia kuzipa vyakula vya bei ndogo, wakitanguliza kushibisha na biashara kuliko lishe bora.”

Kwa mujibu wa kina mama na walezi, wanapozidiwa na kazi, watoto huchelewa kula au hukosa mlo kwa wakati uliopangwa, ikiwamo kunyonya, hali inayowaweka katika hatari kubwa kiafya na katika maendeleo ya ukuaji wao.

Uchunguzi wa Mwananchi pia umebaini kuwa klabu za pombe za kienyeji si salama kwa malezi ya watoto, kwani huwaweka katika mazingira hatarishi katika umri mdogo. Mbali na mazingira yenye uchafu, wadudu, vumbi na moshi, baadhi ya watoto hunyweshwa pombe.

“Baadhi ya kinamama huwapa watoto pombe ya kienyeji (ulanzi) ili walale kwa muda mrefu zaidi wakati wao wakishughulika na kazi au biashara zao,” anasema ofisa afya wa kata ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Imebainika pia kuwa ukosefu wa muda wa kutosha huwazuia kinamama kuandaa milo yenye mchanganyiko wa virutubisho vinavyotakiwa, hivyo kusababisha upungufu katika ukuaji wa mtoto. Ratiba zisizozingatia matakwa ya ulaji na ukosefu wa aina mbalimbali za vyakula vinavyoainishwa kiafya huongeza hatari ya udumavu na ukuaji hafifu wa watoto.

Kwa Watanzania wengi, mlo bado hauna mchanganyiko wa kutosha, huku asilimia 71 ya nishati ya chakula ikitokana na vyakula vikuu, hususan sembe, na kiasi kidogo cha virutubisho vingine.

Kwa sheria za Tanzania, ustawi wa mama na mtoto ni jukumu la umma linalosimamiwa na mamlaka za serikali za mitaa na Serikali Kuu.

 Ofisa Lishe wa Manispaa ya Iringa, Anzaeli Msigwa, anasema mafunzo ya chakula na lishe hutolewa katika vituo vya afya, ofisi za kata, mikutano ya hadhara na kwa kuwatembelea wahusika nyumba kwa nyumba.

“Tunalitoa mafunzo haya mara nne kwa mwaka, sambamba na semina kwa wajawazito, kinamama wenye watoto chini ya miaka mitano na umma wa wananchi wengine kwa ujumla,” anasema.

Mama Millen, mkazi wa Mtaa wa Magari Mabovu, anaunga mkono kauli hiyo akisema: “Huwa tunapatiwa mafunzo ya mama na mtoto pamoja na elimu kuhusu lishe. Wakati mwingine tunalazimika kujifunza kwa vitendo kwa kupika vyakula wakati wa vikao. Hata hivyo, mwaka huu (2025) hakuna mafunzo yaliyofanyika hapa.”

Ofisa kutoka Ofisi ya Lishe Wilaya ya Kilolo, aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina, anakiri imekuwa ngumu kuwakusanya kinamama na watoto wao kwa ajili ya mafunzo kutokana na kutingwa na shughuli zao za kujipatia kipato.

“Programu zetu zinajikita zaidi kwenye kliniki na kutembelea wanufaika wa mafunzo katika kaya zao. Mahudhurio ya mikutano ya uhamasishaji ni madogo kwa sababu kina mama huwa shambani, sokoni, shuleni au kwenye vilabu vya pombe za kienyeji wakijikita katika shughuli za kujiingizia kipato,” anasema.

Ofisa mwingine kutoka Ofisi ya Lishe Manispaa ya Iringa anasema uhaba wa watumishi unasababisha utekelezaji hafifu na kufifisha ufuatiliaji wa mara kwa mara.

Hata hivyo, uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa uhaba wa chakula una nafasi ndogo ya kuchochea udumavu, bali shinikizo la kiuchumi kwa kinamama na jamii kwa ujumla ndilo linalozuia utolewaji wa lishe sahihi na kwa wakati, pamoja na ufuatiliaji sahihi wa ukuaji wa watoto.

Ingawa Mpango Jumuishi wa Pili wa Taifa wa Lishe (NMNAP II) unasisitiza uratibu wa sekta nyingi kushughulikia vichocheo vya utapiamlo, hasa udumavu, mianya katika utekelezaji ni mingi. Sera, mikakati na sheria za lishe zilizopo hazijatekelezwa kikamilifu ili kutoa suluhisho zinazozingatiwa na jamii.

Ofisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Iringa, Tiniel Mbaga, anasema hana ufahamu wa kina kuhusu NMNAP II, lakini anasisitiza kuwa wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Mpango Jumuishi wa Taifa wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) ili kuhakikisha afya na maendeleo bora ya mtoto mkoani Iringa.

Anasema mpango huo unatambua lishe kama moja ya maeneo matano muhimu ya maendeleo ya mtoto. Mengine ni afya, ujifunzaji wa awali, usalama na malezi yenye mwitikio chanya.

“Mpango huu unatukutanisha wadau wote, lakini kila mmoja ana wajibu katika eneo lake. Tusipotekeleza mpango endelevu wa malezi, makuzi na maendeleo ya awali, watoto wanaweza kushindwa kufikia uwezo wao kamili wa ukuaji,” anasema.

Anaeleza changamoto katika ngazi ya jamii ni kubwa, kwani kinamama wengi wanalazimika kuwapeleka watoto walio chini ya miaka mitano katika sehemu zao za kazi kutokana na kukosekana kwa mtu wa kuwalea nyumbani.

“Hii ndiyo sababu tunaendelea kuwasisitiza wazazi kuwapeleka watoto katika vituo vya kulelea watoto mchana,” anasema.

Anasema manispaa, kwa kushirikiana na sekta binafsi, imebainisha majengo 20 yatakayotumika kama vituo vya kulelea watoto vya gharama nafuu. Hata hivyo, anabainisha kuwa utekelezaji bado haujakamilika.

Mbaga anasema kata za Kihesa, Mkwawa na Ruaha zimetambuliwa kama maeneo yenye uhitaji mkubwa kutokana na kukosekana kwa huduma hiyo.

Mbali na hayo, anasema Kata ya Kihesa ina msongamano mkubwa wa klabu za pombe za kienyeji, hivyo kuongeza wasiwasi kuhusu usalama na uangalizi wa watoto.