Mahakama yamruhusu mwalimu kufungua kesi kumpinga Rais

Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Musoma, imempa muda wa siku 30, aliyekuwa mwalimu, Kasoga Mangire, kufungua shauri la maombi ya mapitio kupinga uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuridhia kufukuzwa kwake kazi.

Uamuzi huo umetolewa Januari 30, 2026 na Jaji Marlin Komba baada ya kukubaliana na maombi ya Kasoga kuongezewa muda wa kufungua shauri hilo na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.

Katika maombi hayo, wajibu maombi ni Katibu Mkuu wa Tume ya Utumishi wa Walimu Tanzania (TSC), Rais pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mahakama imesema kuwa mwombaji ameibua hoja nzito za kisheria zinazostahili kusikilizwa katika shauri la mapitio ya Mahakama ambapo mwombaji huyo anaiomba Mahakama ibatilishe uamuzi wa kumfukuza kazini na kuamuru mamlaka husika kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria.

Jaji Komba amesema Mahakama imejiridhisha kuwa madai ya mwombaji, hususan kuhusu kunyimwa haki ya kusikilizwa, yana msingi wa kisheria unaohitaji uchunguzi wa kina, hivyo kuruhusu maombi hayo ya mapitio yafunguliwe tangu tarehe ya hukumu.

Kasoga, ambaye amekuwa mwalimu kwa miaka 25, alifukuzwa kazi kwa madai ya kughushi cheti cha kidato cha nne.

Mwombaji huyo alidai kufukuzwa kazi isivyo haki na TSC ambapo kulithibitishwa na mjibu maombi wa pili (Rais).

Chanzo cha mwalimu huyo kufukuzwa kazi ni madai kuwa alighushi cheti hicho ambapo alidaiwa kusoma Chuo cha Walimu cha Kasulu (mwaka 1994) na akaajiriwa, akifanya kazi kama mwalimu kwa miaka 25 ambapo pia alipewa vyeti vya kitaaluma kutoka shule na vyuo mbalimbali na alionekana kuwa mwalimu mwenye uwezo.

Januari 2022, alipewa notisi ya kinidhamu kutoka kwa TSC na kupewa muda wa siku 15 kujibu notisi hiyo.

Kimsingi, malalamiko ya mwombaji yanapatikana katika aya ya tano na sita ya kiapo kwamba hakupewa ruhusa ya kusikilizwa ipasavyo ambapo angeweza kuwasilisha ushahidi wake na hakupewa haki ya kumhoji shahidi yeyote.

Kumbukumbu za Mahakama zinaonyesha aliwasilisha cheti chake na uthibitisho kutoka Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) ila mjibu maombi wa kwanza na wa pili hawakuzingatia ushahidi wake.

Katika majibu ya wajibu maombi ambayo yaliwasilishwa chini ya hati moja ya kiapo, walieleza kuwa mwombaji alifukuzwa kazi kwa usahihi kwani alipatikana na vyeti viwili vya kidato cha nne vyenye namba sawa ila vikiwa na matokeo tofauti.

Aidha, walieleza Mahakama kuwa alisikilizwa kupitia TSC na alipewa muda wa kupinga madai hayo.

Katika maombi hayo yaliyosikilizwa kwa njia ya maandishi, mwombaji aliwakilishwa na Wakili Baraka Werema huku wajibu maombi wakiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Neema Mwaipyana.

Wakili wa mwombaji aliwasilisha kwamba ombi lililokusudiwa linaibua maswali muhimu ya kisheria kuhusu haki ya kusikilizwa katika kesi za kinidhamu na kupuuza ushahidi uliothibitishwa wa hati.

Alifafanua kwamba mwombaji hakupewa haki ya kusikilizwa kwa haki, pia alikataliwa kukabiliana na ushahidi uliotegemewa na kuhusu kosa la kughushi akieleza kuwa halikuthibitishwa kwa kiwango kinachohitajika kwani hakuna kesi iliyofanywa dhidi ya mwombaji kwa madai ya kughushi.

Alieleza Mahakama kuwa ombi liliwasilishwa ndani ya muda uliowekwa ambao ni miezi sita kuanzia tarehe ambayo msingi wa dai ulijitokeza mwanzoni.

Alieleza uamuzi wa mwisho wa Rais ulipokelewa na mwombaji Mei 9, 2024 ambapo maombi ya awali ya mapitio ya Mahakama yaliwasilishwa Septemba 23, 2024 ila Juni 17, 2025 yalionekana hayajakamilika kwani Rais hakuwa miongoni mwa wajibu maombi ambapo ilielekezwa Rais aongezwe katika orodha ya wajibu maombi.

Wakili aliieleza Mahakama kuwa sababu nyingine ya ombi hilo ni kwamba mwombaji aliyekuwa ameajiriwa Wilaya ya Bunda, alijaribu kupinga uamuzi huo kwa njia za kiutawala bila mafanikio lakini hakufanikiwa ambapo ili kuunga mkono hoja hiyo, alirejea uamuzi wa Mahakama ya Rufaa uliowahi kutolewa.

Jaji Komba amesema baada ya kupitia hoja za pande zote mbili, Mahakama imejielekeza kuangalia iwapo mwombaji amekidhi vigezo vya kisheria vya kupewa ruhusa ya kuwasilisha ombi la mapitio ya Mahakama.

Amesema Mahakama imeona kuwa malalamiko ya mwombaji kuhusu ukiukwaji wa haki ya kusikilizwa, haki ya kiutaratibu na kupuuzwa kwa ushahidi ni masuala mazito ya kisheria yanayostahili kufanyiwa uchunguzi wa kina katika ombi kuu.

Amesema pia Mahakama imejiridhisha kuwa mwombaji ana maslahi ya moja kwa moja katika suala hilo na kwamba ombi liliwasilishwa ndani ya muda wa kisheria hivyo kuruhusu maombi hayo.

“Kwa hiyo, Mahakama inatoa ruhusa kwa mwombaji kuwasilisha ombi la mapitio ya Mahakama, mwombaji anatakiwa kutumia ruhusa hiyo ndani ya siku 30 kuanzia tarehe ya uamuzi huu,” amesema Jaji.