KUREJEA kikosini kwa kipa wa Simba, Yakoub Suleiman, aliyekuwa nje kuuguza majeraha baada ya kuumia akiwa na Taifa Stars wakati ikijiandaa dhidi Nigeria katika Fainali za AFCON 2025, kunakwenda kuongeza nguvu katika eneo hilo ambalo alibaki Mahamadou Tanja Djibrilla Kassali aliyesajiliwa katika dirisha dogo na Hussein Abel.
Yakoub aliwahi kufafanua majeraha yake akisema aliumia siku moja kabla ya mechi hiyo iliyokuwa imepigwa Desemba 23, 2025 nchini Morocco na Taifa Stars kufungwa 2-1.
Februari Mosi, 2026 Simba ilipocheza dhidi ya Esperance de tunis na kutoka sare ya mabao 2-2 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ndiyo siku Yakoub aliyoambiwa na daktari ajiunge na timu.
Chanzo cha ndani kutoka Simba kilisema kipa huyo alishajiunga na timu, ingawa hakufanya mazoezi na wenzake ambao walikuwa wanajiandaa na mechi dhidi ya Esperance de Tunis.
“Asingeweza kuwa sehemu ya mazoezi kwani hakuwa sehemu ya mpango wa mechi, atahitaji fitinesi akiwa anafanya mazoezi na wenzake kwani aliyokuwa akiyafanya wakati anauguza majeraha yalikuwa chini ya madaktari,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Kurejea kwake kutamuongezea nguvu kipa mpya Mahamadou Tanja Djibrilla Kassali katika mechi za Ligi Kuu Bara, ingawa za CAF itategemeana na uharaka wake wa kupata ufiti.”
Wakati huohuo, kuna taarifa zinazomzungumzia kipa Moussa Camara aliyeibuka kinara wa cleansheet msimu uliopita katika Ligi Kuu Bara akimaliza nazo 19 baada ya kuondolewa katika mfumo wa usajili, ataendelea kupokea mshahara wake kila mwezi kama kawaida hadi mkataba wake utakapomalizika mwisho wa msimu huu.
“Kama afya yake ikiimarika na kiwango chake kikirejea, anaweza akarejeshwa tena kikosini ingawa itategemeana na makubaliano, kwani anaweza akapata timu, hivyo lolote linaweza kutokea,” kilisema chanzo hicho.
Kocha wa zamani wa makipa wa Simba, Idd Pazi ambaye pia aliidakia timu hiyo, amesema Kassali kaja wakati mgumu, ila anamwamini ni bora na atafanya vizuri kwenye Ligi Kuu Bara, hivyo Yakoub afanye bidii ili kupata nafasi mbele yake.
“Ingawa bao la pili alilofungwa Kassali anapaswa namna ya kuelekezwa aina ya kuifuata mipira ya aina hiyo, lakini bao la aina hiyo alifungwa kipa wa Yanga, Djigui Diarra mechi dhidi ya Al Hilal, ila wakiboresha hilo ni mmoja wa makipa hodari,” amesema Pazi na kuongeza:
“Yakoub angekuwa na mshauri angerejea JKT Tanzania alikokuwa kipa namba moja na alikuwa anaitwa Taifa Stars, ila kwa sasa akikaa nje itakuwa ngumu kwake kuonekana, hilo ndilo alilolifanya Hussein Masalanga kwenda kujibana kwa Diarra na alijua kabisa hawezi kumuweka benchi.
“Tanzania One ilikuwa inaelea baada ya kuumia Aishi Manula ndiyo maana walikuwa wanaitwa kina Masalanga, Yakoub, Zuberi Foba wa Azam FC lakini endapo kama Manula atakuwa na mwendelezo wa kiwango alichokionyesha hivi karibuni basi anakwenda kurejesha heshima yake ya Tanzania One na yule ni king’ang’anizi atawaweka nje.”
Pazi amemalizia kwa kuwashauri Yakoub, Masalanga na Foba kufanya bidii na kuondoa mitazamo ya kuona wanastahili kuwa makipa namba mbili, wakiamini hakuna kocha atawaweka nje kama viwango vyao vitakuwa juu.