KOCHA wa Simba, Steve Barker, amesema matokeo ya sare ya mabao 2-2 dhidi ya Esperance de Tunis yameacha maumivu makubwa ndani ya kikosi baada ya kushindwa kulinda uongozi wa mabao mawili walioupata mapema katika mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Barker amesema ni jambo la kusikitisha kwa timu kushindwa kushinda mchezo ambao waliudhibiti kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha kwanza na sehemu ya mwanzo ya kipindi cha pili ambapo waliongoza kwa mabao 2-0.
Kocha huyo raia wa Afrika Kusini, alieleza kuwa Simba ilicheza kwa kiwango cha juu katika dakika 45 za kwanza, ikitekeleza kwa ufanisi mipango waliyojiwekea, hali iliyozaa mabao mawili ambayo yalifungwa na Shomary Kapombe na Yusuph Kagoma na kuwapa faida kubwa kabla ya mapumziko.
Ameongeza kuwa hata baada ya kurejea kipindi cha pili, timu yake ilionekana kuwa imetulia na kuumudu mchezo katika dakika za mwanzo, kabla ya kuruhusu bao la kwanza lililobadilisha mwelekeo wa mchezo.
Barker amesema bao hilo la Esperance lilisababisha mabadiliko ya kasi na presha, jambo lililoathiri mfumo wa uchezaji wa Simba.
Alifafanua kuwa, hali ilizidi kuwa ngumu baada ya timu kupata majeraha ya ghafla kwa baadhi ya wachezaji muhimu, hali iliyomlazimu kufanya mabadiliko ya lazima ambayo hayakuwa sehemu ya mipango ya awali.
Kocha huyo alitaja jeraha la kiungo Yusuph Kagoma kuwa lilikuwa ni pigo kubwa kwa timu, akisema kuondoka kwake kulipunguza uimara wa Simba katika eneo la kiungo.
“Kufungwa mabao mawili na kushindwa kushinda kutoka kwenye nafasi tuliyokuwa nayo ni jambo linaloumiza, hasa kwa sababu wachezaji walifanya kazi kubwa sana kipindi cha kwanza,” amesema Barker.
Aliongeza kuwa baadhi ya mambo ambayo benchi la ufundi limekuwa likiyafanyia kazi mazoezini yalianza kuonekana uwanjani, jambo lililompa matumaini juu ya mwelekeo wa timu.
Hata hivyo, Barker alikiri kuwa vijana wake wanatakiwa kujua namna bora ya kulinda matokeo, hususani katika kipindi cha pili, ili kuepuka kupoteza pointi muhimu.
Amesema wakati mwingine si rahisi kujiandaa kwa kila hali inayojitokeza ndani ya mchezo, lakini timu inapaswa kuwa na uwezo wa kudhibiti nyakati ngumu.
“Tutaendelea kufanya kazi kwa bidii, kupambana kwa ajili ya beji ya Simba na kuhakikisha timu inaendelea kukua na kuwa bora zaidi, natambua hali ambayo mashabiki wetu wanajisikia, lakini hiki ni kipindi cha mpito na niwahakikishie kuna nyakati nzuri za furaha zinakuja ni suala la muda tu,” amesema.
Kwa sasa Simba imesaliwa na mechi mbili katika hatua ya makundi kwa kucheza ugenini dhidi ya Petro Atletico huko Angola kabla ya kufunga pazia katika michuano hiyo kimataifa kwa kucheza dhidi ya vinara Stade Malien.