Nafasi ya mzazi kung’amua vipaji vya mtoto

Dar es Salaam. Kila mtoto huzaliwa na kipaji fulani ndani yake. Hiki ni kile kitu cha kipekee anachokifanya kwa urahisi, kwa ustadi, na kwa furaha.

Ni sehemu ya asili ya mtoto ambayo humtofautisha na wengine. Hata hivyo, kipaji hicho, kisipotambuliwa mapema na kuendelezwa ipasavyo, hubakia kikiwa kimelala au hata kufa kabisa.

Dunia imejaa watu wazima waliowahi kuwa watoto wenye vipaji vikubwa, lakini hawakuwahi kupewa nafasi ya kuvikuza.

Matokeo yake, jamii inapoteza wasanii, wanamichezo, wanasayansi, wabunifu, na hata viongozi waliokuwa na uwezo mkubwa lakini waliishia katika maisha ya kawaida kwa sababu hakuna aliyewasaidia kung’amua kipaji chao.

Katika karne ya 21, ambapo ubunifu na vipaji vina nafasi kubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii, mzazi au mlezi hawezi tena kulichukulia  suala hili kibahati nasibu.

Namaanisha mzazi anakaa akisubiri kile kitakachomtokea mwanawe. Huko siko kuwajibika kama mzazi makini.

Ni wajibu wa kila mzazi kuchukua jukumu la kutambua mapema kipaji cha mtoto wake, na zaidi ya hapo, kuhakikisha anakipatia mazingira ya kukua na kuendelezwa.

Lakini kipaji ni nini hasa? Kipaji ni uwezo wa kipekee wa asili ambao mtu anazaliwa nao. Hii inaweza kuwa uwezo wa kuimba, kuchora, kucheza michezo, kuongoza, kuzungumza mbele ya watu, kufanya hesabu, au hata kuwa mbunifu wa vitu vipya.

Kipaji kinaweza kujitokeza mtoto akiwa na umri mdogo sana. Kwa mfano, mtoto anayependa kuimba kila mara, au anayependa kuchora hata ukuta wa nyumba, anaweza kuwa na kipaji cha sanaa.

Tatizo ni kwamba mara nyingi, watu wazima huchukulia tabia hizo kama michezo au ulevi wa utoto, badala ya kuwa ishara ya kipaji.

Mzazi mwenye maono huangalia zaidi ya alichonacho mtoto darasani. Huchunguza kile anachopenda kufanya, kile kinachomvutia, na kile anachokiendea kwa hiari yake.

Hii ndiyo njia rahisi ya kutambua kipaji. Kwa mfano, kama mtoto kila mara anapenda kushika vifaa vya umeme, kufungua vitu, kuviunganisha, au kuuliza maswali ya kina kuhusu jinsi vitu vinavyofanya kazi,  huenda ana kipaji cha uhandisi.

Mzazi makini ataanza kumwelekeza katika shughuli zinazohusiana na taaluma hiyo, hata kabla ya mtoto kuingia ngazi za juu za elimu.

Kuna makosa makubwa yanayofanywa na baadhi ya wazazi na hata walimu  kutaka kila mtoto awe bora katika masomo ya darasani tu. Mfumo wa elimu umekuwa ukipima mafanikio ya mtoto kwa karatasi na namba, bila kuangalia vipaji vingine visivyoonekana moja kwa moja darasani.

Hii imewakatisha tamaa watoto wengi ambao si lazima wawe bora kwenye hisabati au sayansi, lakini wana uwezo mkubwa katika maeneo mengine.

Mzazi au mwalimu anayelazimisha mtoto kufaulu katika eneo ambalo si nguvu yake ya asili, humchosha mtoto huyo na wakati mwingine humkatisha tamaa kabisa katika maisha.

Hapa namkumbuka mwalimu wangu wa maadili na mwanasafu mwenzangu katika gazeti hili, Profesa Raymond Mosha ambaye siku zote anakemea tabia ya kutaka mtoto afanye asichotaka kielimu.

Kuwekeza kwenye kipaji cha mtoto ni kama kupanda mbegu nzuri ardhini. Mbegu hiyo itahitaji mbolea, maji, mwanga wa jua na matunzo ya kila siku. Kipaji cha mtoto ni hivyo hivyo. Baada ya kukitambua, mzazi anapaswa kuhakikisha mtoto anapata mafunzo sahihi, mazingira ya mazoezi, na zaidi ya yote motisha na msaada wa  kisaikolojia.

Mzazi mwelevu pia anapaswa kuwa mvumilivu. Kipaji hakijengwi kwa siku moja. Kuna nyakati mtoto atakata tamaa, atavunjika moyo, au hata kuchoka. Ni jukumu la mzazi kuhakikisha mtoto anaendelea kuamini katika uwezo wake.

Ni muhimu pia kuelewa kuwa kila kipaji kina nafasi yake katika dunia ya sasa. Dunia ya sasa inahitaji wabunifu, wasanii, wanamichezo, waigizaji, na wataalamu katika nyanja mbalimbali.

Mtoto wako anaweza kuja kuwa mtu mashuhuri kupitia kipaji chake cha uchezaji, uimbaji, ubunifu wa programu za kompyuta, au hata kupika.

Si lazima kila mtoto awe daktari au mwanasheria ili aitwe amefanikiwa. Mafanikio ni kufanya kile unachopenda kwa bidii na kukifikia kwa ubora wa hali ya juu.

Mzazi asiyethamini kipaji cha mtoto wake ni sawa na mkulima anayekataa kumwagilia mmea unaoota vizuri shambani mwake. Dunia hii haimsubiri mtu yeyote. Watoto wanaozaliwa leo wanakua kwenye ulimwengu wa kasi, wa ushindani mkali, na wa mabadiliko ya kila wakati.

Ili mtoto aweze kusimama imara kesho, kipaji chake kinapaswa kupewa nafasi leo. Kipaji ni kama taa ndani ya giza, kinapopewa nafasi huangaza njia ya mtoto bila kumchosha.

Katika jamii yetu, bado kuna hitaji kubwa la elimu kuhusu vipaji. Shuleni na majumbani, kunahitajika mabadiliko ya fikra.

Walimu na wazazi wanapaswa kushirikiana katika kuwasaidia watoto wao kutambua vipaji vyao na kuvikuza. Serikali pia inaweza kushiriki kwa kuanzisha vituo vya kukuza vipaji na kuweka sera zinazotambua umuhimu wa vipaji katika mfumo wa elimu. Tusipofanya hivi sasa, tutajikuta tuna kizazi cha vijana wasioelewa nafasi yao katika dunia hii.

Tambua kipaji cha mtoto wako leo. Kikuze, kitunze. Kiwekee mazingira ya kukua. Msaidie mtoto wako kutambua kuwa kile anachokifanya kwa urahisi si mchezo, bali  ni ishara ya mwelekeo wake wa maisha. Na siku moja, utaweza kusema kwa fahari, “Niliona kipaji ndani ya mtoto wangu, nikakilea, na sasa dunia nzima inakiona.”