JK KWA MFALME MSWATI III KUJADILI UPATIKANAJI WA FEDHA ZA MIRADI YA AFYA KWA NCHI WANACHAMA WA ECSA



Mfalme Mswati III akikutana na Washiriki wa Mkutano wa 67 wa Mawaziri wa Afya wakiongozwa na Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete

Dkt. Kikwete akihutubia Washiriki katika Mkutano huo

Dkt. Kikwete akiwa na Bw. Mduduzi Matsebula, Waziri wa Afya wa Eswatini (kushoto kwake) na Dkt. Ntuli Kapologwe, Mkurugenzi Mkuu wa ECSA-HC

Mfalme Mswati III akiwa katika picha ya pamoja na Washiriki wa Mkutano wa 67 wa Mawaziri wa Afya

Ezulwini, Ufalme wa Eswatini – Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi Jakaya Mrisho Kikwete Foundation (JMKF) ameshiriki Mkutano wa 67 wa Mawaziri wa Afya kutoka nchi 9 wanachama za Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika (ECSA-HC) unaofanyika Ezulwini, Ufalme wa Eswatini tarehe 2-3 Februari, 2026.

Pamoja na mambo mengine, Mkutano huo umejadili mikakati ya kuimarisha mifumo ya afya ya nchi wanachama wa ECSA-HC, hususan kwa kuzingatia mabadiliko yanayoendelea duniani kote yaliyopelekea kupungua au kusitishwa kabisa kwa upatikanaji wa fedha za kufadhili miradi ya afya kutoka kwa wafadhili waliozoeleka.

Katika hotuba akifungua Kikao cha Makatibu Wakuu na Maafisa Waandamizi wa ECSA-HC, Dkt. Kikwete alitoa rai kwa nchi hizo kuwa wabunifu katika kubuni na kutafuta vyanzo mbadala vya rasilimali za kifedha ili kuhakikisha kuwa miradi iliyokwishaanza kutekelezwa haitetereki au kufa kutokana na kukoma kwa fedha za wafadhili.


 “Kama Serikali huwezi kuwaambia wananchi kuwa tunasitisha huduma za afya kwa sababu wafadhili wameacha kutoa fedha. Hapana. Ni wajibu wenu kama watunga Sera kuumiza vichwa na kufanya juu chini kutafuta vyanzo mbadala vya fedha ili wananchi waendelee kupata huduma wanazostahili”, alieleza Dkt. Kikwete.

Alitumia pia fursa hiyo kutoa uzoefu wake jinsi walivyowahi kukabiliana na changamoto za aina hiyo wakati wa uongozi wake ambapo moja ya mbinu walizobuni ni kuimarisha ushirikiano wa kikanda baina ya nchi za Afrika ili kuongeza uhimilivu wa mifumo ya afya, ikiwemo uamuzi wa nchi za ukanda huu kufanya manunuzi ya pamoja ya jumla kwa bei nafuu (bulk-procurement) ya dawa, vifaa tisa na vitendanishi badala ya kila nchi kununua vifaa hivyo kivyake.

Rais Mstaafu Dkt. Kikwete alitumia pia fursa hiyo kueleza washiriki hao hatua kubwa za mafanikio zilizopigwa na Tanzania chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sekta ya afya. Akitoa mfano, alieleza namna ushirikiano wa karibu kati ya Serikali ya Tanzania na wadau wa mashirika yasiyo ya kiserikali, ikiwemo Taasisi ya JMKF, ulivyoweza kushusha kiwango cha vifo vya wakinamama wanaojufungua kutoka vifo 560 kwa kila kinamama 100,000 wanaojifungua hadi kufikia vifo 104 na kuifanya Tanzania kuwa nchi inayoongoza barani Afrika katika kutimiza lengo la Umoja wa Mataifa la SDG 3.1 linalozitaka nchi zote duniani kushusha kiwango hicho hadi kufikia vifo 70 ifikapo mwaka 2030.

Akitoa mfano wa umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali mashirika binafsi katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya katika ngazi ya jamii, Dkt. Kikwete alieleza namna JMKF inavyotoa huduma za kliniki inayotembea (mobile outreach) kwa kinamama wajawazito wanaoishi maeneo ya mbali na vituo vya afya na magumu kufikika katika Wilaya za Uyui na Sikonge, Mkoani Tabora.

Kwa mujibu wa Taasisi ya JMKF, Mradi huo unaojulikana kama Jamii Salama umechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga mkoani Tabora ambapo hadi sasa umewagusa zaidi ya wakina mama 1,500 kwa kuwapatia huduma za kliniki, ikiwemo huduma ya ultrasound, tiba ya malaria, pamoja na kuwafikia watoto wa shule zaidi ya 3,200 kwa elimu ya afya ya kinywa na malaria.

Kwa upande mwingine, Rais Mstaafu Dkt. Kikwete aliongoza washiriki wa Mkutano huo kuonana na Mfalme Mswati III wa Eswatini ambaye aliahidi kupokea ripoti itakayotokana na majadiliano ya Mkutano huo na kuifikisha kwa Viongozi wenzake wa nchi wanachana wa ECSA-HC na Jumuiya nyingine za Kikanda.