Dodoma. Wabunge wametaja kilimo cha umwagiliaji kuwa mkombozi kwenye mkakati wa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Mapema jana, Jumatatu Februari 2, 2026, Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, aliwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa 2050, ambao umegawanyika katika mapendekezo ya muda mfupi na yale ya mwaka mmoja.
Katika michango yao, wabunge wengi wameelezea namna Serikali inavyoweza kupata unafuu kwa kuwatumia vijana kwenye shughuli za kilimo.
Mbunge wa Tanganyika (CCM), Seleman Kakoso, amesema kilimo kinacholimwa sasa ni cha kujikimu, ambacho hakiwezi kuwavusha watu kwenda popote zaidi ya chakula.
“Ili tuweze kujikomboa, ni lazima tuwekeze katika kilimo cha umwagiliaji, nguvu kubwa ya vijana tuipeleke huko, lakini kilimo cha sasa ni cha kujikimu, hakiwezi kutuvusha,” amesema Kakoso.
Kwa mujibu wa Kakoso, mipango mingi inaweza kupangwa na kujadiriwa, lakini pasipokuwa na mkakati wa kuzalisha chakula na kuwa na malighafi za kulisha viwanda bado itakuwa kazi bure.
Mbunge wa Mbeya Mjini (CCM), Patrick Mwalunenge, ametaka mkazo zaidi uwekwe katika kilimo cha pamba, ikiwemo kuongeza ubora wa mazao ya matunda.
Mwalunenge amesema bodi ya pamba imekosa mtaji na Serikali haijapeleka msukumo wa kutosha huko, kama ambavyo iliwekeza kwenye zao la korosho, ambalo limeanza kutoa tija.
Mbunge huyo ametaja sababu ya kutokuwa na viwanda vya nguo inatokana na uzalishaji mdogo wa pamba na ukosefu wa ubora.
“Ili kuwa na kiwanda kikubwa cha nguo, ni lazima tuzalishe si chini ya tani milioni moja, lakini sisi tunazalisha chini ya tani 500,000, hapo ni ngumu kusema tutakuwa na viwanda vya nguo,” amesema Mwalunenge.
Kuhusu ubora wa matunda, mbunge huyo amelalamikia namna Tanzania inavyozalisha matunda kwa wingi, lakini hayana ubora kwa viwango vya kimataifa.
Ametolea mfano wa machungwa, ambayo alikuwa amepewa zabuni ya kupeleka Shanghai, China, lakini amepeleka majaribio machache yalionekana kutokuwa na ubora, sasa analazimika kuagiza Afrika Kusini.
Katika mchango wake, Japhael Lufungija, mbunge wa Ulyankulu, amesema mpango bila kuwekeza nguvu katika mashamba ni kazi bure na itakuwa vigumu kufikia malengo yanayotarajiwa.
Lufungija amesema jukumu zima la kufikia malengo hayo linapaswa kuwabebesha vijana, ambao ni lazima kwanza watengenezewe miundombinu ya mabwawa ya umwagiliaji.
Amesema mabwawa yakichimbwa yatasaidia kupeleka thamani ya kilimo, kwani ardhi bado ipo na nguvu kazi ipo ya kutosha.
Katika Kitabu cha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, suala la usimamizi madhubuti wa ardhi limetajwa.
“Ardhi ni rasilimali muhimu inayotoa fursa kwa ajili ya maendeleo ya kilimo, viwanda, makazi na shughuli nyingine za uchumi,” inasema sehemu ya mpango.
Wizara ya Uwekezaji inataja kuwa Tanzania ina takribani kilomita za mraba milioni moja za ardhi ambazo ni muhimu kwa maendeleo endelevu.