TIMU ya Ukonga Kings imerejea katika Ligi Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), baada ya kuifumua Magone kwa mechi 2-0 katika nusu fainali ya Ligi Daraja la Kwanza, na hivyo kujihakikishia nafasi ya kucheza fainali huku ikijikatia tiketi ya kupanda daraja.
Itakumbukwa kwamba Ukonga Kings ilishuka daraja 2023, ambapo awali 2022 timu hiyo iliyolewa na JKT katika nafasi ya kutafuta mshindi wa tatu.
Jana, katika mchezo wa nusu fainali uliopangwa kuchezwa mara tatu kwa mfumo wa ‘best of three play-off’ ulipigwa kwenye Uwanja wa Donbosco, Upanga ukiishuhudia Ukonga Kings iliyoshinda kwa pointi 63-54 awali ikiibuka na ushindi wa pointi 54-48.
Kwa matokeo hayo, hivi sasa inasubiri mshindi kati ya KR One na Mlimani BC uliotarajiwa kuchezwa jana Jumanne usiku katika uwanja huo. Hata hivyo, licha ya timu hiyo kutinga fainali, imekuwa timu ya kwanza kutangulia kupata nafasi ya kucheza BDL mwaka huu.
Nafasi hiyo inatokana na Ukonga Kings kuwa moja kati ya timu tatu zinazotakiwa kucheza ligi hiyo mwaka huu kutoka Ligi ya Daraja la Kwanza. Timu mbili zitakazocheza fainali zinapata nafasi ya kucheza BDL, huku ile ya tatu ikitokana na matokeo ya mechi ya kutafuta mshindi wa tatu itakayozikutanisha timu zilizofungwa katika nusu fainali.
Akizungumzia jambo hilo, kocha wa Ukonga Kings, Achile Martin, amesema timu hiyo ilistahili kushinda dhidi ya Magone katika hatua ya nusu fainali.
“Sisi tulikuwa bora zaidi yao. Tulijipanga vizuri kushinda mchezo huo. Timu ya Magone haikuwa na uwezo wowote wa kutushinda,” alitamba Martin.
Fainali ya ligi hiyo imepangwa kuanza kuchezwa Jumamosi kwa michezo mitatu ya mfumo wa ‘best of three play-off’, ambapo timu tatu zitakazofanya vizuri zitacheza BDL mwaka huu.
