AKU kuwaunganisha wanafunzi na fursa za kibiashara

Dar es Salaam. Chuo Kikuu cha Aga Khan nchini (AKU), kimezindua klabu ya ujasiriamali ili kuwawezesha na kuwaunganisha wanafunzi wa chuo hicho na fursa za kibiashara.

Kwa mujibu wa chuo hicho, hatua hiyo pia, itawasaidia wanafunzi kusoma kwa vitendo kuhusu ujasiriamali badala ya nadharia pekee wakiwa chuoni hapo.

Uzinduzi huo umefanyika leo, Februari 3, 2026 katika chuo hicho kilichopo Upanga jijini Dar es Salaam.

AKU imebobea zaidi katika kutoa kozi za afya hasa fani za udaktari, ukunga na uuguzi, elimu (ualimu) na ujasiriamali.

Mhadhiri wa AKU, Profesa Tumbwene Mwansisya ambaye ni mtaalamu wa afya na ujasiriamali amesema eneo la afya kuna fursa ya kibiashara, lakini bado watu hawajaligundua.

“Tunatamani wanafunzi wakimaliza chuo kuwa na uwezo wa kujiajiri na kuajiri wengine, ili kufikia azma, lazima wawe na ujuzi wa kuzitengeneza hizo ajira.

“Pamoja na wanafunzi kusoma masomo ya afya na ualimu, hapa chuoni kuna kozi ya ujasiriamali. Tumefikia kama wanasoma ujasiriamali kwa nadharia haitakuwa na maana, badala yake wasome kwa vitendo tena wakiwa hapa hapa chuo,” amesema.

Mkuu wa AKU, Profesa Eunice Pallangyo amesema klabu hiyo imeanzishwa na wanafunzi wa chuo ili kutumia fursa ya duka walilolianzisha kwa ajili ya ubunifu wa bidhaa mbalimbali zitakazouzwa kwa wafanyakazi chuoni hapo.

“Tulichokifanya AKU ni kuwapa nafasi na kuwashika mkono kidogo ili kutimiza jukumu lao. Wanatengeneza juisi ambayo ndani yake ina tiba mbalimbali mwilini,” amesema Profesa Pallangyo.

Profesa Pallangyo amesema katika chuo hicho wanafunzi hao wameanzisha bustani ndogo iliyopandwa mazao mbalimbali yatakayotumika kwa ajili ya klabu ya ujasiriamali.

Amefafanua kuwa kupitia klabu inawawezesha wanafunzi kukutana pamoja na kuumiza vichwa kwa kufikiria ikiwamo kuingiza sayansi ndani yake.

“Tunataka mtu akitoka hapa amepata alama A ya kemia, iwe na msaada kweli kweli ambayo itaweza kutafsiri mambo. Tunatamani kutengeneza wahitimu watakaokuwa majibu ya changamoto kwenye jamii,”

Mkuu wa Chuo cha Udaktari cha Aga Khan, Profesa Paschal Ruggajo ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo, amesema somo la ujasirimali linafundishwa ili kuwaanda wahitimu na maisha baada ya chuo.

“Serikali inajitahidi kuboresha fursa za ajira, lakini siku zote hazijawahi kutosheleza, hivyo wanafunzi wetu wanapohitimu na stadi mbalimbali ikiwamo ubunifu wa kujiajiri wenyewe wanasaidia soko la ajira,” amesema Profesa Ruggajo.

Mmoja wa wanafunzi wanaounda klabu hiyo, Elfraha Masawe amesema hatua hiyo itawezesha kujiajiri au kuwaajiri vijana wengine kutokana na ubunifu walioufanya.

“Tumeangalia mazingira na changamoto mbalimbali ambazo tumezigeuza kuwa fursa kwa kuandaa kitu kama hiki. Duka hili litawezesha wafanyakazi wa ndani kupata huduma ndani si lazima kutoka nje ya chuo,” amesema Masawe.