Morogoro. Baada ya Tanzania kuorodheshwa kuwa miongoni mwa nchi 10 duniani zinazoongoza kwa vifo vinavyotokana na ugonjwa wa malaria, Shirika la Amplify Health & Development in Africa limeanzisha mpango maalumu wa kuwaandaa wahudumu wa afya ngazi ya jamii na vijana 160.
Wahudumu hao watatumika kutoa elimu na hamasa kwa wananchi kuhusu kinga, utambuzi wa mapema na udhibiti wa ugonjwa wa malaria pamoja na magonjwa mengine yasiyopewa kipaumbele.
Akizungumza kwenye mafunzo hayo leo Februari 3, 2026, katika kikao kazi cha wataalamu wa afya kilichofanyika mjini Morogoro, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Amplify Health & Development in Africa, Aloyce Urassa, amesema ripoti ya malaria ya mwaka 2025 ya Shirika la Afya Duniani (WHO) imeitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa vifo vitokanavyo na ugonjwa huo.
Urassa amesema hali hiyo inaonesha bado kuna changamoto kubwa katika mapambano dhidi ya malaria, licha ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali pamoja na wadau wa afya.
Amesisitiza kuwa hali hiyo inahitaji juhudi za pamoja kati ya Serikali, wadau wa maendeleo na jamii ili kupunguza maambukizi na vifo vinavyotokana na ugonjwa huo.
Urassa amesema mpango ulioanzishwa na shirika hilo unalenga kuimarisha uelewa wa jamii, hususan katika maeneo yenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya malaria na magonjwa mengine yasiyopewa kipaumbele.
Ameongeza kuwa mpango huo utatumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii na vijana kama chachu ya kutoa elimu, hamasa na taarifa sahihi za afya kwa wananchi baada ya kukamilika kwa kikao kazi hicho.
“Ripoti ya malaria ya mwaka 2025 inaonesha wazi kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa vifo vitokanavyo na ugonjwa huu duniani. Hali hii inaonesha kuwa bado kuna changamoto kubwa katika kinga na uzuiaji wa maambukizi licha ya jitihada mbalimbali zinazofanywa,” amesema Urassa.
Ameongeza kuwa,kuendelea kwa Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 10 zinazoongoza kwa vifo vitokanavyo na malaria ni ishara kuwa kuna haja ya kuongeza nguvu katika utoaji wa elimu na hamasa kwa wananchi.
Urassa amesisitiza kuwa, njia bora ya kupambana na malaria na magonjwa yasiyopewa kipaumbele ni kuijengea jamii uelewa wa namna ya kujikinga, kutambua dalili mapema na kufuata matibabu sahihi.
Mratibu wa Huduma za Afya Ngazi ya Jamii kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Tamisemi, Dk May Alexander amesema kikao hicho ni sehemu ya maandalizi ya utekelezaji wa Mradi wa Jamii Shupavu.
Amesema mradi huo unalenga kutumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii na vijana kama wasimamizi wa huduma za afya katika maeneo yao.
Dk May amesema mradi huo utatekelezwa katika halmashauri nne za Tanzania Bara ambazo ni Ulanga (Morogoro), Nzega (Tabora), Pangani (Tanga) na Kiteto (Manyara).
Amefafanua kuwa, Halmashauri ya Ulanga wananchi wanakabiliwa zaidi na ugonjwa wa usubi, Kiteto ugonjwa wa vikope, Pangani magonjwa ya matende na mabusha, huku Nzega ikitajwa kuwa miongoni mwa halmashauri zenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya malaria nchini.
