Dodoma. Taasisi ya Aga Khan kwa kushirikiana na Ubalozi wa Ireland nchini kupitia mradi wa Tuamke Pamoja imepanga kutumia Sh7 bilioni kwa mitatu kuviwezesha vikundi vya kijamii 57 kwenye halmashauri sita za Mkoa wa Dodoma.
Vikundi hivyo kutoka halmashauri za Wilaya ya Kondoa Vijijini, Kondoa Mji, Bahi, Chamwino, Dodoma Mjini na Chemba, wanufaika wakubwa katika mradi huo ni wanawake, watu wenye ulemavu na vijana.
Wakizungumza jana Jumatatu, Februari 2, 2026 kwenye uzinduzi wa Mradi wa Tuinuke Pamoja uliofanyika wilayani Kondoa Mkoa wa Dodoma, wanufaika wa mradi huo wamesema maisha yao yamebadilika baada ya kufadhiliwa na Aga Khan Foundation.
Mweka Hazina wa Kikundi cha Tujikomboe Makamaka Women Group kutoka wilayani Chemba, Veronica Balie amesema kupitia ufadhili wa Aga Khan Foundation wamefanikiwa kuanzisha kilimo cha bustani za mboga mboga na kununua vyerehani kwa ajili ya shule ya ushonaji.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya jamii, jinsia wazee na watoto, Felister Mdemu (kushoto), akizungumza na wanawake wa Kikundi cha Tujikomboe Makamaka Women Group kutoka Wilayani Chemba kwenye uzinduzi wa mradi wa Tuinuke Pamoja uliofanyika Wilayani Kondoa mkoani Dodoma.
Amesema mpaka sasa wana wanafunzi watano ambao wamejiunga kwa ajili ya mafunzo ya kushona nguo mbalimbali.
”Aga Khan Foundation imetuwezesha Sh27.5 milioni ambazo zimetusaidia kuanzisha miradi mbalimbali ikiwamo ufugaji wa kuku wa kisasa na tuna mpango wa kujenga banda kubwa la kisasa lenye uwezo wa kuhifadhi kuku 2,000 kutoka 450 tulionao sasa, lakini kupitia fedha hizo tumefanikiwa kutengeneza pedi za kike ambazo tutazigawa kwa wanafunzi walioko shuleni,” amesema Balie.
Amesema awali kabla la ufadhili walikuwa wanafanya miradi mbalimbali lakini hawakuona faida yake, baada ya ufadhili wameanza kupata faida inayowawezesha kuboresha maisha yao.
Mwenyekiti wa Kikundi cha Amkeni Wanawake Viziwi kutoka Wilaya ya Bahi, Helena Banjilwa amesema kikundi hicho kinaundwa na wanawake watatu viziwi walioamua kujikita kwenye uzalishaji wa siagi ya karanga.
Amesema waliamua kujiunga kwenye kikundi kwa kuwa walikuwa wanapitia changamoto nyingi kutokana na ulemavu walionao ikiwamo unyanyapaa, hivyo ili kujikwamua walijiunga ili watumie fursa zilizopo ikiwamo ufadhili wa Aga Khan Foundation.
Amesema kupitia ufadhili huo, wamepewa elimu ya ujasiriamali, kujua fursa za kiuchumi, kijamii na kimaendeleo zilizopo kwenye maeneo yao ikiwamo haki za binadamu na haki za watu wenye ulemavu.
Balozi wa Ireland nchini, Nicola Brennan akiangalia kazi za wajasiriamali wanaofadhiliwa na Aga Khan Foundation Wilayani Kondoa mkoani Dodoma.
”Aga Khan Foundation imetuwezesha kusimama sisi wenyewe na sasa tunajiamini,” amesema Banjilwa.
Meneja miradi kutoka Aga Khan Foundation, Nestory Mhando amesema jumla ya vikundi 57 kutoka halmashauri sita za Mkoa wa Dodoma zimenufaika na mradi huo unaotekelezwa kwa miaka mitatu kwa Sh7 bilioni kwa kushirikiana na Ubalozi wa Ireland nchini.
Amesema wanufaika wa mradi huo ni vikundi vya kijamii vilivyoko ngazi ya vijiji, kata na vitongoji vilivyoundwa na wanawake pamoja na vikundi vya watu wenye ulemavu na vijana
Balozi wa Ireland nchini, Nicola Brennan (mwenye shati la kijani) akiwa amepanda kwenye pikipiki ya inayotumia umeme ambayo imetolewa kwa wahudumu wa Afya kwa ajili ya kuhudumia jamii Wilayani Kondoa. Picha na Rachel Chibwete
vilivyosajiliwa kwenye ngazi ya halmashauri, lengo likiwa ni kuwainua ili waweze kujitegemea kiuchumi.
Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Aga Khan Foundation, Atteeya Sumar amesema kwa kipindi cha nusu ya utekelezaji wa mradi huo wameona matokeo chanya kwa vikundi walivyovidhamini.
Amesema vikundi vimepewa mafunzo mbalimbali ya ujasiriamali, utunzaji wa fedha, elimu ya biashara, utunzaji wa mazingira na kupinga ukatili wa kijinsia kwenye jamii yao ikiwamo ukeketaji.
Amesema nusu ya kipindi cha mradi huo wamewafikia jumla ya wanufaika 10,969 wakiwamo wanawake 6,224 na wanaume 4,745 kwenye halmashauri zote zinazotekeleza mradi.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa Mradi wa Tuinuke Pamoja, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Felister Mdemu amewataka wanufaika wa mradi huo kuzitumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuimarisha uchumi wao.
Amesema Aga Khan Foundation imewaamini na kutenga fedha nyingi kwa ajili ya kuwawezesha, hivyo wasimwangushe.
