Suluhisho kukabiliana na udumavu Iringa -3

Iringa. Wadau wa lishe wanapendekeza hatua mahususi za kukabiliana na viwango vya udumavu wa watoto mkoani Iringa, wakionya kuwa sheria na sera zilizopo hazitafsiriwi ipasavyo wala kutekelezwa katika ngazi ya kaya na jamii.

Licha ya Iringa kuwa miongoni mwa mikoa mikuu ya uzalishaji wa chakula, bado inaongoza kwa viwango vya juu vya udumavu miongoni mwa watoto walio chini ya miaka mitano.

Takwimu za Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto Tanzania wa mwaka 2022 (TDHS-MIS) zinaonesha kuwa udumavu unaathiri asilimia 56.9 ya watoto walio chini ya miaka mitano mkoani Iringa, ukifuatiwa na Njombe kwa asilimia 50.4 na Rukwa kwa asilimia 49.8. Kati ya watoto waliodumaa Iringa, asilimia 17.3 wameainishwa kuwa na kiwango kikubwa cha udumavu.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi katika Manispaa ya Iringa, Wilaya ya Kilolo na Iringa Vijijini kati ya Oktoba na Desemba 2025 umebaini kuwa lishe si sababu pekee ya utapiamlo unaohusisha udumavu, kukonda na uzito mdogo, bali pia kulea watoto katika maeneo ya kazi na kuwapa vileo watoto walio chini ya umri wa miaka mitano kumechangia kuwapo kwa hali hiyo.

Hali hii inakiuka Kifungu cha 17 na 20 cha Sheria ya Mtoto (Sura ya 13), Kifungu cha 3 na 4 cha Sheria ya Chakula na Lishe Tanzania (Sura ya 109), pamoja na Mpango Jumuishi wa Pili wa Taifa wa Lishe (NMNAP II – 2021/22–2025/26). Vilevile, inakiuka Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Mtoto, ambao Tanzania imeridhia.

Sheria na mpango huo vinawataka maofisa lishe na ustawi wa jamii kuhakikisha watoto wanalelewa ipasavyo na kupata mlo unaochochea ukuaji na ustawi wao.

Pia, maofisa hao wanaelekezwa kutekeleza afua za chakula na lishe zilizobainishwa katika mipango ya maendeleo ya Taifa na kushirikiana na wadau wengine kulinda ubora wa chakula.

Hatua hizi zinalenga kuhakikisha ukuaji bora wa mtoto, kumsaidia kufikia uwezo wake kamili na kukuza programu endelevu za lishe zinazochangia ustawi wa mtu binafsi na maendeleo ya Taifa.

Walezi, maofisa lishe, mashirika ya kiraia na wataalamu wa afya katika Manispaa ya Iringa, Wilaya ya Kilolo na Iringa Vijijini, ambako uchunguzi wa Mwananchi umefanyika, wanaeleza kuwa matatizo ya ukuaji wa watoto mara nyingi hugundulika kwa kuchelewa, ushauri wa kliniki hukosa uwazi kwa wazazi, na kwamba hakuna juhudi za kutosha na zenye mwendelezo kusaidia familia nje ya vituo vya afya.

Kutokana na hayo, wanapendekeza hatua ambazo wanaamini zikitekelezwa ipasavyo na kwa kuzingatia sheria na sera zilizopo, zitapunguza kwa kiasi kikubwa udumavu mkoani Iringa.

Wanabainisha kuwapo kwa uchelewaji wa kutolewa elimu ya lishe, wakieleza kuwa jitihada kwa sasa zinajikita zaidi katika kipindi cha ujauzito na baada ya kujifungua, badala ya kujenga maarifa mapema zaidi.

“Tunasubiri hadi mwanamke awe mjamzito au mtoto awe na uzito mdogo ndipo tuanze kuzungumzia kwa uzito suala la lishe,” anasema Ritha Paul, mama wa watoto wanne na kiongozi wa nyumba kumi katika Mtaa wa Mkimbizi, Manispaa ya Iringa.

Anaeleza kuwa kufikia wakati huo, tabia nyingi huwa tayari zimejengeka: “Elimu ya lishe inapaswa kufundishwa shuleni kuanzia ngazi ya msingi ili watoto wakue wakiwa na uelewa wa kutosha kuhusu chakula, afya na malezi.”

Anasema awali masomo ya sayansikimu na uchumi wa nyumbani yalikuwa sehemu ya mitaala ya shule za msingi, ambako wanafunzi walifundishwa kuanzia darasa la tano.

“Tulijifunza shuleni stadi za msingi za maisha kama kupika, maandalizi ya chakula na namna ya kutunza miili na familia zetu. Elimu ya lishe inapaswa kuanzia shuleni, siyo kliniki,” anasema.

Maoni hayo yanaungwa mkono na baadhi ya maofisa lishe, waliotaka kurejeshwa kwa elimu ya stadi za maisha shuleni, ikiwamo maandalizi ya chakula, mlo kamili na malezi ya msingi ya watoto.

Kwa mtazamo wao, elimu hiyo ingewapa wazazi wa baadaye maarifa ya vitendo, tena kwa muda mrefu kabla hawajaingia katika majukumu ya malezi.

Katika vituo vya afya, wadau wanasisitiza umuhimu wa mwongozo wa kliniki ulio wazi na wa vitendo zaidi, wakisema ushauri kama “ongeza lishe” au “ongeza ulaji” pasipo kufafanua namna ya kutekeleza huwa mgumu kufanyiwa kazi majumbani.

“Mama anahitaji kujua kwa usahihi ni vyakula gani aandae, amlishe mtoto mara ngapi ili atekeleze hayo kwa kiasi cha fedha alichonacho,” anasema Samwel Paul, aliyekuwa ofisa lishe katika Mtaa wa Tumaini, Kata ya Kihesa, Manispaa ya Iringa.

Paul, aliyewahi kuhudumu kama ofisa lishe wa jamii kwa watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU) katika shirika lisilo la kiserikali la Care International, anasema kama mwongozo si wa vitendo, huwa mgumu kuzingatiwa.

Kwa upande wake, Paulo Brasili, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Call Africa, anasema ufuatiliaji hafifu na maelekezo yanayokatisha tamaa katika kliniki huwa na madhara ya muda mrefu.

“Wazazi wengi wa watoto wenye utapiamlo hapa Iringa hukata tamaa mapema na huacha kuhudhuria kliniki, wakati mwingine hata kukosa chanjo za kawaida,” anasema na kuongeza:

“Hali inapofikia hatua mbaya, mara nyingi huwa vigumu kurekebisha madhara yaliyojitokeza.”

Call Africa, shirika lenye makao yake mkoani Iringa, linajishughulisha na kupambana na umaskini na ukosefu wa haki za kijamii, na kwa sasa linaendesha programu tatu mkoani humo.

Programu hizo ni kituo cha malezi kinachotoa huduma kwa watoto wenye ulemavu, kituo cha lishe kwa watoto wenye utapiamlo, na mpango wa lishe shuleni unaosaidia shule saba za msingi za umma.

Brasili anasema elimu endelevu na ufuatiliaji ni muhimu, akisisitiza kuwa: “Elimu ya lishe lazima izifikie familia majumbani mwao kupitia viongozi wa serikali za mitaa na watoa huduma za afya.”

“Kinamama wanahitaji kuelewa umuhimu wa kurejea kliniki na kukamilisha matibabu ya lishe kwa watoto wao. Wakati huohuo, watoa huduma wanapaswa kuwafuatilia kwa karibu watoto wenye utapiamlo na walezi wanaoacha kuhudhuria kliniki,” anasema.

Anaeleza kuwa mtoto anapoondolewa kwenye mpango wa lishe, kunapaswa kuwa na ufuatiliaji hata kama familia imehama.

“Hivi sasa wanapotoweka kliniki, mfumo mara nyingi hushindwa kuwafuatilia na mara nyingi hupotea,” anasema.

Inapendekezwa pia kuwapo kwa ratiba za kliniki na vipindi vya lishe vinavyowalenga kinamama wafanyakazi, badala ya mihadhara mirefu.

“Tuligundua kwa kiasi kikubwa tulikuwa tunazungumza sisi kwa sisi,” anasema ofisa lishe wa Kata za Ilala na Mkwawa katika Manispaa ya Iringa, Sizo Nzogere.

Anasema juhudi za awali za kuandaa semina za lishe katika ofisi za kata hazikutoa matokeo yaliyotarajiwa.

“Tulipobadili mkakati na kuhamia kwenye uhamasishaji wa kijamii, tuliwafikia watu wengi zaidi,” anasema.

Inapendekezwa umuhimu wa majukwaa ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kama njia bora za kutoa elimu ya lishe.

Vipindi vya redio, taasisi za kidini, matukio ya michezo na mikutano ya vijiji vinatajwa kama maeneo yanayoaminika ambako ujumbe unaweza kutolewa na kufikia kaya nzima.

“Sasa tunafanya kazi na viongozi wa dini kwa sababu wanawafikia watu wengi kila wiki. Tulitambua kuwa inasaidia kupeleka ujumbe wa lishe nje ya kliniki,” anasema Nzogere.

Wadau pia walibainisha hitaji la dharura la huduma za malezi ya watoto zinazotegemea jamii, hususan kwa kinamama wanaofanya kazi kwa saa nyingi sokoni, shambani au waliojiajiri katika sekta isiyo rasmi.

Walionya kuwa bila njia mbadala za malezi salama na za kuaminika, watoto wadogo wako katika hatari kubwa ya kukosa au kuchelewa kula.

Kwa mujibu wa maofisa lishe, changamoto hiyo inaanza kushughulikiwa. Katika hilo, ofisa ustawi wa jamii wa Manispaa ya Iringa, Tiniel Mbaga, anasema manispaa kwa kushirikiana na asasi ya BRAC wanafanya utambuzi wa majengo yanayofaa kutumika kama vituo vya malezi ya watoto vya gharama nafuu.

Hata hivyo, anasema utekelezaji bado haujaanza, hali inayowaacha kinamama wengi wanaofanya kazi bila msaada wa kutosha.

Kwa ujumla, wadau wanakubaliana kuwa kupunguza udumavu Iringa hakuhitaji sheria mpya bali mabadiliko ya mtazamo, elimu inayoanza mapema, inayofikia kaya kwa ufanisi zaidi na inayoendana na namna familia zinavyoishi na kufanya kazi.

“Kinga, uwazi na ufuatiliaji ni mambo muhimu. Tukipeleka elimu ya lishe karibu na familia na kuwaunga mkono kina mama badala ya kuwalaumu, tunaweza kuvunja mzunguko wa utapiamlo na udumavu mkoani Iringa,” anasema Brasili.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe, amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika tafiti ili kuboresha afua za lishe nchini.

Amesema Tamisemi, kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, wanaandaa mpango mkakati unaoelekeza namna bora ya kutekeleza NMNAP II ili kuleta matokeo yanayoonekana katika lishe na maendeleo ya watoto.

Alitoa kauli hiyo jijini Dodoma Januari 22, 2026, wakati wa mkutano wa tisa wa kutathmini utekelezaji wa Mkataba wa Lishe wa Kitaifa uliosainiwa Septemba 2022. Katika tathmini hiyo, wadau walitoa mapendekezo ya hatua za kuboresha lishe nchini.

Amesema kwa takwimu zilizopo, ni asilimia 47 pekee ya watoto walio chini ya miaka mitano walio kwenye ukuaji unaoridhisha, wakati asilimia 53 wako kwenye ukuaji hafifu.

“Lishe ni mojawapo ya viashiria muhimu vinavyotumika kupima ukuaji na maendeleo ya mtoto, hivyo inapaswa kupewa kipaumbele cha juu,” amesema.