Dar es Salaam. Zana duni za kilimo zinazosababisha ugumu wa kazi pamoja na ukosefu wa teknolojia za kisasa ni miongoni mwa sababu za sekta ya kilimo kukabiliwa na uhaba wa nguvukazi hasa vijana.
Imeelezwa vijana wameamua kuchana na aina hiyo ya kilimo cha jadi chenye tija kidogo huku kukiwa hakuna teknolojia rafiki, wanawake ndio wanaendelea kubeba mzigo huo hali inayozidisha utofauti wa kijinsia.
Hayo yote yamebainishwa leo Jumanne Februari 3, 2026 na Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba wakati akifungua mkutano wa kwanza kufanyika Afrika unaohusu zana endelevu za kilimo (Africa Sustainable Agricultural Mechanization) unaofanyika hapa Dar es Salaam kupitia Wizara ya Kilimo kwa ushirikiano na Shirika la chakula na kilimo duniani, (FAO).
Mkutano huo wa siku tatu ambao utaenda sambamba na uzinduzi wa mkakakti wa Taifa wa zana za kilimo awamu ya pili kuanzia 2025/26 hadi 2036 unajadili namna ya kuwatoa wananchi katika umaskini ambao zaidi ya asilimia 80 wanategemea kilimo.
Dk Nchemba amesema vijana barani Afrika wanasita kuwekeza sekta ya kilimo hasa ukilinganisha kipindi hiki cha mabadiliko ya tabianchi, hivyo ongezeko la ushindani wa matumizi ya ardhi huwezi kuwekeza kwa vijana kujikita kwenye kilimo na zana za kizamani.
Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba, wakati akifungua Mkutano wa Kwanza wa Kikanda wa Afrika wa Matumizi Endelevu ya Zana za Kilimo, uliofanyika katika Hotel ya Johari Rotana, Dar es Salaam, leo Jumanne, Februari 3, 2026. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu.
“Hali ya uwekezaji katika zana za kilimo barani Afrika, haijaendana na mahitaji halisi ya wakulima wadogo pamoja na mifumo dhaifu ya huduma, ukosefu wa mitaji, ukosefu wa ujuzi wa kiufundi, kukwama kwa minyororo ya thamani ya maendeleo, upotevu wa mazao baada ya mavuno.
“Sababu hizi zinafanya vijana kutowekeza nguvu kubwa katika sekta hii na mifugo, hivyo mtakachojadili kwenye mkutano huu kitaenda kutafuta suluhisho tuondokane na matatizo ya aina hii,” amesema.
Katika kukabiliana na hilo, Waziri huyo Mkuu amesema Serikali imeongeza uwekezaji katika huduma za zana za kilimo, utafiiti na uendelezaji wa ujuzi hasa kwa vijana kwa kushirikiana na FAO ambapo imeandaa mkakati wa Taifa wa zana za kilimo unaolenga kuimarisha matumizi ya uzalishaji usimamizi na uratibu wa teknolojia za kilimo katika minyororo wa thamani.
“Serikali imepanga kununua matrekta 10,000 pamoja na kuanzishwa kwa vituo jumuishi 1,000 vya huduma za zana za kilimo katika ngazi ya kata, hatua inayoongeza tija na kupunguza gharama sambamba na kuwapa wakulima muda wa kufanya shughuli zingine,” amesema.
Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba, akifungua Mkutano wa Kwanza wa Kikanda wa Afrika wa Matumizi Endelevu ya Zana za Kilimo uliofanyika katika Hotel ya Johari Rotana, Dar es Salaam, leo Jumanne, Februari 3, 2026. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mbali ya changamoto zinazokabili sekta hiyo, amesema ni muhimu kuimarisha uwekezaji katika zana za kilimo rafiki kwa mazingira na zinazozingatia mabadiliko ya tabianchi, zana hizo zinapaswa kupunguza uzito wa kazi kuongeza tija, kulinda mazingira kwa kutumia teknolojia na kupunguza upotevu wa mazao.
“Tunapaswa kuhakikisha ushiriki mkubwa wa sekta binafsi katika uzalishaji, usambazaji na utoaji wa huduma za zana pamoja na zana za kilimo, Serikali zinapaswa kuweka mazingira wezeshi ya sera, sheria na vivutio vya uwekezaji ili sekta hizo zishiriki kikamilifu kupunguza gharama kwa wakulima,” amesema.
Aidha, kuwawezesha vijana na wanawake ili washiriki kikamilifu katika biashara na ubunifu kwakuwa ndio kundi lenye nguvu linaloweza kuleta matokeo katika uzalishaji na soko kwa kuwa ni msingi wa maendeleo endelevu.
Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo amesema mkakati wa Taifa za zana za kilimo uliozinduliwa leo unahusu matumizi endelevu pamoja na usimamizi wa teknolojia ili kurahisisha kazi katika minyororo wa uzalishaji sekta ya kilimo ikiwa ni kufanikisha utekelezaji wa dira ya maendeleo pamoja na sera ya kilimo.
Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba, akikagua baadhi ya Zana za Kilimo katika Mkutano wa Kwanza wa Kikanda wa Afrika wa Matumizi Endelevu ya Zana za Kilimo uliofanyika katika Hotel ya Johari Rotana, Dar es Salaam, leo Jumanne, Februari 3, 2026. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Msaidizi wa Mkurugenzi Mkuu wa FAO na Mwakilishi wa Kikanda ya Afrika, Abebe Gabriel ameishukuru Tanzania kwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo mkubwa uliokutanisha wadau kutoka nje ya Bara la Afrika.
Amesema suala la uvumbuzi, mitambo ya kisasa na matumizi ya kiteknolojia mambo hayo yanasaidia katika kuendeleza shughuli za FAO hapa barani Afrika.
Charles Spillane, Mwanasayansi Mkuu wa FAO amesema lazima kuachana na kilimo cha mazoea, inapaswa kutambua matumizi ya mashine za kisasa za kilimo, yanahitaji kubuniwa katika mchakato ambao kwa mabadiliko ya thamani inahitaji kubadilisha matokeo.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema mkoa huo hauna kilimo kikubwa bali ni soko kubwa kwa bidhaa za kilimo kutokana mikoa ya Tanzania huku akiomba uwekezaji zaidi.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Bashiru Ally amesema kubadilisha nyenzo za uzalishaji soko na uhifadhi mazao umeleta matokeo chanya na mabadiliko katika sekta hiyo hasa ufugaji na uvuvi.
