MBEYA City imeendelea kuhaha Ligi Kuu Bara baada ya leo kuambulia tena sare dhidi ya Dodoma Jiji, huku Kocha Mkuu wa timu hiyo Mecky Maxime akitaja kinachowaangusha akitoa matumaini mapya kwa ajili ya mechi zijazo.
Wakati Maxime akitoa kilio kwa kukosa matokeo ya ushindi mfululizo, Dodoma Jiji wao wamechekelea pointi moja kwenye Uwanja wa Sokoine, huku Kocha Mkuu Aman Josiah akiwapongeza wachezaji wake.
Maxime ameiongoza Mbeya City mchezo wa tatu leo akiambulia sare ya pili baada ya ile dhidi ya Pamba Jiji huku akipoteza mmoja mbele ya Mtibwa Sugar na kuwa nafasi ya 13 kwa pointi 10 baada ya mechi 13.
Dodoma Jiji baada ya mchezo huo wamepanda nafasi ya nane kwa pointi 14, michezo sawa na wapinzani hao na sasa wanarejea nyumbani kuwakaribisha KMC kwenye mwendelezo wa ligi hiyo.
Katika mchezo huo uliopigwa saa 8 mchana kwenye uwanja wa Sokoine, Dodoma Jiji ndio walitangulia kupata bao dakika ya 10 kupitia kwa WillIam Edagar, kabla ya Eliud Ambokile kuisawazishia Mbeya City dakika ya 26.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Maxime amesema pamoja na wachezaji kuonesha ubora na kumiliki mpira, lakini bado tatizo kubwa ni kufunga mabao ya udhindi, akitaja saikolojia kuwaathiri.
Amesema bado anayo matumaini kwa timu hiyo kufanya vizuri, akiahidi kuwa watakapoanza kushinda, kuna mtu atakula nyingi bila kujali ugenini au nyumbani akiwatuliza mashabiki kutokata tamaa.
“Ninao uzoefu wa ligi kuu kuanzia kucheza hadi kufundisha, nitafanyia kazi tatizo la mchezaji mmoja mmoja haswa, kisaikolojia hawako sawa kufuatia mwendelezo wa kukosa ushindi,” amesema Maxime.
“Naamini tutakapoanza kushinda kuna timu itakula nyingi yakipungua basi matatu, vijana wanapambana kwa kuwa wanamiliki mpira na wanatengeneza nafasi, tatizo ushindi tu.”
Kwa upande wake, Josiah amesema matokeo hayo siyo mabaya kwao kwa kuwa walitaka ushindi, lakini pointi moja nayo si haba kwa kuwa ligi ni ngumu na haina ugenini wala nyumbani.
“Pointi nne katika mechi tatu za ugenini siyo mbaya niwapongeze wachezaji kwa kujituma. Kukutana na timu zilizopo nafasi za chini huwa ushindani ni mkali, lakini wamepambana na tunaenda kujipanga tena,” amesema kocha huyo.