Clara, Masaka waitwa kukiwasha WAFCON 2026

KOCHA wa timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania maarufu Twiga Stars, Bakari Shime ametangaza kikosi cha awali kitakachojiandaa na michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2026, itakayofanyika Machi 17, 2026 hadi Aprili 3, 2026 nchini Morocco.

Kikosi hicho kinajumuisha wachezaji 30 kutoka klabu mbalimbali za ndani na nje ya Tanzania wakiwamo Clara Luvanga anayecheza Saudi Arabia na Aisha Masaka wa Brighton ya England. Mbali na hilo, nyota kutoka JKT Queens wameitwa kwa wingi wakichomoza mara 12.

Katika droo ya WAFCON 2026, Twiga Stars imepangwa Kundi B na itachuana na Afrika Kusini, Ivory Coast na Burkina Faso.

Kundi hilo linatajwa kuwa gumu, lakini Kocha Shime ameonyesha imani kikosi chake kinaweza kufanya vizuri iwapo maandalizi yatakuwa bora na wachezaji kuonyesha nidhamu na kujituma.

Wachezaji wa JKT Queens walioitwa katika kikosi hicho ni Najiath Abbas, Lidya Maximilian, Donisia Minja, Christer Bahera, Anastazia Katunzi, Ester Maseke, Janeth Christopher, Joyce Lema, Elizabeth Chenge, Stumai Abdallah, Winfrida Gerald na Jamila Rajabu.

Simba Queens wapo wawili ambao ni Asha Omary na Aisha Juma, huku Yanga Princess walioitwa ni watatu Diana Mnaly, Maimuna Kaimu na Neema Shau.

Timu zingine zilizotoa wachezaji wengi ni Juarez ya Mexico ambao Enekia Kasonga na Juletha Singano. Pia FC Masar ya Misri wapo Vaileth Nicholaus na Hasnath Ubamba.

Nyota wengine walioitwa ni Asha Mrisho (Mashujaa Queens), Nusrat Jafar (Fountain Gate), Husna Mtunda (Alliance Girls),

Suzan Adam (Tausi FC), Noela Luhala (MFA Žalgiris ya Lithuania), Opah Clement (SD Eibar ya Hispania), Clara Luvanga (Al Nassr ya Saudi Arabia), Aisha Masaka (Brighton & Hove Albion ya England) na Diana Lucas (Trabzonspor ya Ururuki).