Pigo sekta ya usafirishaji abiria ikipoteza vigogo wawili siku moja

Dar es Salaam. Sekta ya usafirishaji wa abiria nchini imetikiswa baada ya kuwapoteza wakongwe wake wawili ndani ya siku moja, huku wadau wakisema ni pigo kubwa kutokana na mchango wao wa zaidi ya robo karne.

Wawili hao waliofariki dunia ni mwanzilishi na mmiliki wa kampuni ya mabasi ya NBS mkoani Tabora, Nassor Hamdani, na Mohamed Hood, mmiliki na mwanzilishi wa kampuni ya mabasi ya Hood mkoani Morogoro.

Hamdani alifariki dunia alipokuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, jijini Dar es Salaam, huku Hood akifariki dunia akiwa nyumbani kwake mtaa wa Mlapakoro, Kata ya Mji Mkuu Manispaa ya Morogoro. Wote walifariki jana, Jumatatu, Februari 2, 2026.

Ni wakongwe katika sekta ya usafirishaji wa abiria kwa kuwa Hamdani na Hood ni miongoni mwa wawekezaji wa mwanzo katika biashara ya mabasi ya mikoani, kabla ya kuibuka kwa kampuni nyingine nyingi zinazoonekana sasa.

Si hivyo tu, Hood ni miongoni mwa waasisi na ndiye Mwenyekiti wa kwanza wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), aliyetumikia nafasi hiyo kwa zaidi ya miaka 10, kabla ya baadaye kuachia ngazi kwa hiari.

Wadau wa sekta ya usafiri wamesema vifo vyao ni pigo kubwa kwa tasnia hiyo kutokana na mchango wao katika kuimarisha huduma za usafiri wa abiria, kutoa ajira kwa Watanzania na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Wamesema kupitia uwekezaji wao, maelfu ya ajira zilitolewa kwa madereva, makondakta na mafundi, huku wananchi wakinufaika na huduma za usafiri wa uhakika, salama na wa gharama nafuu, na Serikali ikikusanya mapato kupitia kodi na tozo mbalimbali.

“Mzee Hood na mwenzake walikuwa viongozi wa hekima na busara. Hawakupenda migogoro na Serikali, bali walipendelea mazungumzo kama njia bora ya kutatua changamoto za sekta,” amesema Priscus John, Katibu Mkuu wa sasa wa Taboa.

Kwa mujibu wa maelezo ya John, sekta ya usafirishaji nchini imepoteza nguzo mbili muhimu za kiuchumi kutokana na vifo vyao, akisema pengo lao halitazibika kirahisi.

Amesema mzee Hood alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa mabasi ya kisasa ya Marcopolo Scania yanayofanya safari za masafa marefu, na alikuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Taboa.

Amesema katika kipindi chote cha uongozi wake, Hood alihimiza wamiliki wa mabasi kushirikiana na Serikali badala ya kuchukua misimamo mikali kama migomo, akiamini mazungumzo yana tija zaidi kwa ukuaji wa biashara.

Kwa upande wa Hamdani, John amesema alikuwa miongoni mwa wawekezaji waliodumisha huduma za usafirishaji katika nyakati ngumu, hasa katika njia za vumbi kabla ya miundombinu ya barabara kuboreshwa.

“Alifanya kazi katika mazingira magumu. Njia nyingi zilikuwa hazijajengwa kwa lami, lakini aliendelea kutoa huduma hadi barabara zilipoboreshwa,” amesema.

Akikumbuka mazingira waliyofanyia kazi, John amesema kipindi hicho nchi ilikuwa na kilomita chache za barabara za lami na uhaba mkubwa wa maduka ya vipuri.

“Ilikuwa kawaida basi kuharibika na kifaa cha kurekebisha kupatikana umbali wa zaidi ya kilomita 100. Wakati mwingine unakaa barabarani siku nzima. Walifanya kazi kwa jasho na damu,” amesema.

Amesema wawili hao waliwekeza mabilioni ya fedha katika ununuzi wa mabasi na waliweza kuhimili soko kwa muda mrefu, jambo adimu katika sekta hiyo ambayo imekuwa ikikabiliwa na changamoto za kiafya kwa wamiliki wake, ikiwemo presha na kisukari.

“Unaponunua basi la Sh600 milioni unaambiwa faida ni kubwa, lakini uhalisia wa soko ni tofauti kabisa. Sekta hii ina changamoto nyingi zisizoonekana juu juu,” amesema.

John amesema wawili hao walikuwa mstari wa mbele kupinga sera na sheria walizoziona kandamizi kwa wamiliki wa vyombo vya usafirishaji, huku wakisisitiza utoaji wa huduma bora, salama na zinazolingana na gharama halisi za uendeshaji.

“Walikuwa wakisisitiza kuwa mapato yaendane na ubora wa huduma. Walikuwa na mchango mkubwa kwa Serikali na sekta nzima ya usafirishaji,” amesema.

Amesema Hamdani alikuwa nembo ya uchumi wa usafirishaji mkoani Tabora, akimiliki mabasi mengi yaliyokuwa yakihudumia ruti mbalimbali kutoka mkoani humo kwenda mikoa mingine.

John amesema sekta ya usafirishaji wa abiria ni ngumu na yenye hatari kubwa za kifedha, hali inayosababisha kampuni nyingi kufilisika ndani ya muda mfupi. Hata hivyo, Hood na Hamdani waliweza kuhimili ushindani na changamoto za soko kwa zaidi ya miaka 25.

“Walikuwa na uzoefu mkubwa na wameacha elimu muhimu kwa kizazi cha sasa cha wawekezaji. Ingawa pengo lao halitazibika, upande wa NBS kuna vijana wengi waliobaki na kampuni inaendelea kufanya vizuri,” amesema.

Amesema Hood, baada ya miaka ya uwekezaji mkubwa katika mabasi, alipunguza shughuli zake katika sekta hiyo na kuelekeza mitaji katika maeneo mengine ya kiuchumi.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), Habibu Suluo, amesema taasisi hiyo imepokea kwa huzuni taarifa za vifo vya wamiliki hao wakongwe wa mabasi nchini na kwamba ni pigo kwa sekta ya usafiri na maendeleo ya uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Amesema wawekezaji hao walitoa mchango mkubwa katika kukuza sekta ya usafirishaji wa abiria, hususan kwa kuimarisha huduma za usafiri, kutoa ajira kwa maelfu ya Watanzania na kuchangia mapato ya Serikali kupitia kodi na tozo mbalimbali.

Amesema kupitia uwekezaji wao, sekta ya usafiri iliwezeshwa kuwa kichocheo muhimu cha shughuli za kiuchumi katika mikoa waliyohudumia.

“Sio familia pekee zilizopoteza, bali Taifa lote limepoteza. Latra tumepoteza, na wadau wa uchukuzi wamepoteza hazina kubwa ya uzoefu, uadilifu na uwekezaji wa wazee hawa,” amesema Suluo.

Amesema mchango wao umeacha alama muhimu katika historia ya maendeleo ya sekta ya usafiri nchini, huku Latra ikiendelea kuenzi mchango wa wawekezaji hao kwa kuimarisha mazingira rafiki ya kiuchumi na kisheria yatakayochochea uwekezaji endelevu katika sekta ya usafiri.

“Tumepoteza waasisi hawa, lakini uwekezaji waliouacha utaendelea kwa kuwa ni kampuni. Hivyo pengo ni kuwapoteza wao binafsi, na tunatarajia uongozi wa kampuni zao utaendeleza uwekezaji waliouacha,” amesema.