Dodoma. Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomu (IAEA) Kanda ya Afrika limeiagiza Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa kujiandaa kutoa huduma za matibabu ya saratani kwa wagonjwa kutoka mataifa mengine, baada ya kuridhishwa na miundombinu na maandalizi yanayoendelea katika hospitali hiyo.
Maelekezo hayo yametolewa baada ya kukubalika kwa mazingira na miundombinu inayojengwa mahsusi kwa ajili ya utoaji wa huduma za saratani ndani ya jengo jipya linalotarajiwa kuzinduliwa Septemba mwaka huu.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa mradi huo leo Jumanne, Februari 3, 2026, Mkurugenzi wa IAEA Kanda ya Afrika, Gashaw Wolde, amesema licha ya jengo hilo kutokamilika, maandalizi yaliyofanyika yanaonesha kuwepo kwa mipango mikubwa na ya muda mrefu katika utoaji wa huduma za saratani.
Kauli hiyo inakuja wiki mbili baada ya Waziri wa Afya na Usafi wa Mazingira wa Malawi, Madalitso Baloyi, kutangaza kuwa wananchi wa nchi hiyo sasa wanaweza kupata huduma za matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi nchini Tanzania, hususan katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, baada ya wataalamu wa nchi hiyo kujiridhisha kuwa huduma zinazotolewa zinakidhi viwango vinavyohitajika.
“Mawazo ni mazuri, ubunifu ni wa hali ya juu. Asanteni sana Tanzania. Napenda kusisitiza kuwa maandalizi haya yasihusishe kutibu Watanzania pekee, bali hospitali hii iwe kitovu cha kupokea wagonjwa kutoka mataifa jirani. Jambo la msingi ni kuwekeza zaidi katika rasilimali watu,” amesema Wolde.
Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dk Henry Humba, amesema hospitali hiyo imejenga jengo la kisasa lenye thamani ya Sh30.2 bilioni, linatarajiwa kukamilika Agosti mwaka huu na kuanza rasmi kutoa huduma za matibabu ya saratani ifikapo Septemba.
Dk Humba ameongeza kuwa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomu Kanda ya Afrika limekuwa mshirika muhimu tangu hatua za awali za ubunifu wa mradi huo, likitoa mchango mkubwa ikiwemo kusomesha madaktari na kuwajengea uwezo watoa huduma za afya.
“Hata hivyo, tunahitaji fedha za haraka kiasi cha Sh12 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vitakavyofungwa ndani ya jengo hilo ili kuwezesha utoaji wa huduma za kisasa zaidi. Pamoja na changamoto hiyo, tupo tayari kupokea wagonjwa kutoka nje ya nchi kama tulivyoelekezwa,” amesema Dk Humba.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC), Profesa Najat Mohammed, amesema maandalizi ya ujenzi na kuanza kwa huduma za saratani na mionzi yanaendelea vizuri, huku akibainisha kuwa huduma hizo zinatarajiwa kuanza mwaka huu ili kuwapunguzia wananchi gharama na usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu hayo.
Kwa sasa, hospitali zinazotoa huduma za matibabu ya saratani nchini ni Taasisi ya Saratani Ocean Road, jijini Dar es Salaam, Hospitali ya Bugando mkoani Mwanza, Hospitali ya KCMC mkoani Kilimanjaro, huku maandalizi ya kuanza kutoa huduma hizo yakiendelea katika Hospitali ya Benjamin Mkapa na Hospitali ya Rufaa ya Mbeya.
