Uber yasitisha tena huduma Tanzania, Latra yasema…

Dar es Salaam. Kampuni ya Uber, ambayo hutoa huduma ya usafiri ya teksi kwa njia ya mtandao, kwa mara nyingine imetangaza kusitisha shughuli zake nchini Tanzania kuanzia Januari 31, 2026 kutokana na changamoto za kibiashara.

Mara ya kwanza, kampuni hiyo ilisitisha utoaji wa huduma Aprili 2022 hadi Januari 2023 kwa sababu kama hizo.

Leo Jumanne, Februari 3, 2026, akizungumza na Mwananchi, Ofisa Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mahusiano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra), Salum Pazzy, amesema taarifa zilizokuwa zikisambaa kuwa Uber imejiondoa nchini ni sahihi na wamepokea barua rasmi.

“Ni kweli kumekuwa na taarifa mbalimbali za Uber kujiondoa nchini, na sisi mamlaka ya udhibiti tunathibitisha kampuni hiyo imesitisha huduma kwa muda, si kujiondoa moja kwa moja,” amesema Pazzy.

Amesema Latra imepokea barua ya kampuni hiyo, iliyoandikwa Januari 30, 2026, kutoka ofisi za Uber BV zilizopo Amsterdam, Uholanzi, ikieleza uamuzi wa kusitisha huduma kwa muda katika soko la Tanzania.

Kwa mujibu wa Pazzy, sababu kuu ya hatua hiyo ni changamoto wanazokutana nazo katika uendeshaji wa biashara zao hapa nchini, akisisitiza kuwa hali hiyo si jambo geni katika sekta ya biashara.

“Kwa kampuni zinazofanya biashara, kuna nyakati hukutana na changamoto za uendeshaji, na wakati mwingine hulazimika kusitisha huduma kwa muda ili kujipanga upya. Hili si jambo la ajabu,” amesema.

Amesema wana matumaini Uber inaweza kurejea kutoa huduma zake nchini siku za usoni baada ya kujipanga upya.

Hata hivyo, Kifungu cha 6(a) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini Sura ya 413, kimeipa Latra wajibu wa kuhamasisha ushindani wenye ufanisi miongoni mwa watoa huduma zinazodhibitiwa.

Hatua hiyo ya Uber, Pazzy amewatoa hofu wadau wa usafiri wa teksi mtandaoni na wananchi kwa ujumla, akisema soko hilo linaendelea kufanya vizuri kutokana na uwepo wa kampuni nyingine nyingi za ndani na nje ya nchi zinazotoa huduma kwa ufanisi.

Amesema kutokana na ubora wa soko hilo, iliwahi kutangazwa tuzo ya kampuni bora ya teksi mtandaoni kwa kutoa huduma salama na bora, iliyotolewa mwaka 2025 na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, wakati wa maadhimisho ya kwanza ya Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini.

Latra imesisitiza iko tayari kushirikiana na Uber endapo kampuni hiyo itaamua kurejea nchini, pamoja na kuhakikisha mazingira ya uwekezaji na utoaji wa huduma yanaendelea kuwa rafiki kwa wadau wote wa sekta ya usafiri.

“Hii inaonesha wazi kuwa soko la teksi mtandaoni nchini linaendelea vizuri, hivyo hakuna sababu ya wananchi au madereva kuwa na hofu,” amesema.

Mbali na hilo, Pazzy amesema kumekuwepo na malalamiko kuhusu teksi mtandao kutoka kwa baadhi ya madereva, ambayo mamlaka hiyo imewashauri yawasilishwe rasmi ili yafanyiwe kazi.

“Maofisa wa Latra, ikiwemo wa mkoa wa Dar es Salaam, wamekuwa wakishiriki vikao na madereva wa teksi mtandaoni kusikiliza changamoto zao na kutafuta ufumbuzi.”

Dereva wa teksi mtandao, Richard Massawe, amesema kusitishwa kwa Uber haitawaathiri kwa sababu walikuwa wanapata pesa kidogo zaidi kuliko kampuni nyingine.