Polisi Arusha yazungumzia Mbwambo wa fedha za Lissu

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi mkoani Arusha linaendelea kumshikilia kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Fredrick Mbwambo, kwa tuhuma za wizi wa fedha zilizochangwa kwa ajili ya kumsaidia mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu.

Mbwambo alikamatwa siku nane zilizopita baada ya jeshi hilo kupokea malalamiko kutoka kwa kaka yake Lissu, Alute Mughwai, aliyebaini wizi wa fedha hizo zilizokuwa zimechangwa kwa ajili ya mdogo wake.

Wiki iliyopita, Vincent Mughwai (mdogo wake Lissu) aliiambia Mwananchi kuwa harambee ya kumchangia Lissu ilifanywa na vijana na marafiki wa Chadema,  ikiongozwa na Mbwambo.

Mwananchi ilipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo, Januari 30, 2026, kujua kinachoendelea, alisema bado wanaendelea kulifuatilia suala hilo.

Leo, Jumanne Februari 3, 2026, Mwananchi ilipofuatilia tena suala hilo, Kamanda Masejo alijibu kupitia ujumbe mfupi: “Uchunguzi unakamilishwa.”

Alipoulizwa kama Mbwambo ameachiwa kwa dhamana, amejibu: “Bado tunaye”.

Chanzo cha kuaminika kiliidokeza Mwananchi wiki iliyopita kuwa mchakato wa kampeni ya kuhamasisha mchango wa Lissu, uliopewa jina la ‘Funga mwaka na Tundu Lissu’, uliendeshwa na Mbwambo na makada wengine wa Chadema, majina yamehifadhiwa (wanaoishi nchi jirani).

Taarifa zinadai kuwa makada walifanya kampeni ya uhamasisho kupitia makundi ya mitandao ya kijamii katika wiki ya mwisho wa Desemba 2025 na kwamba usiku wa Desemba 31, siku ya mwisho ya kuchangisha, liliwekwa tangazo kuwa zimepatikana Sh26 milioni, lakini uhalisia ilikuwa Sh41 milioni.

Baada ya hapo, Mughwai alikabidhiwa Sh22 milioni, na kuelezwa alipata wasiwasi na kwenda kujiridhisha kupitia taarifa za miamala na kubaini kiwango kilichopatikana ni zaidi ya alichokabidhiwa.

Pazia la mchango huo lilipofungwa, inadaiwa Sh6 milioni zilitumwa kwenda nchi jirani (Nairobi, Kenya) kupitia namba ya wakala, wakati Sh2 milioni zikitumwa kupitia namba ya mkononi ya mtandao mmoja wa Tanzania.

Katika taarifa yake Januari 27, 2026, Kamanda Masejo alisema: “Ufuatiliaji wa awali umeonesha kuwa ukusanyaji huo wa fedha ulikuwa ukifanywa kupitia namba mbili za simu za kampuni tofauti. Inadaiwa zilihamishiwa kwenye namba hizo mbili, moja ikiwa ni ya kampuni ya Tanzania na nyingine ni ya kampuni ya simu ya nchi jirani.”

Inadaiwa Sh700,000 zilitumwa kwa namba hiyo hiyo iliyopokea awali Sh2 milioni, lakini baada ya jambo hilo kufika Jeshi la Polisi, Sh2 milioni zilirudishwa kwenye akaunti ya Mughwai.

Aidha, inadaiwa Sh3 milioni zilitumwa kwenye namba nyingine ya Kitanzania. Hiyo ni baadhi ya miamala mikubwa iliyofanywa katika mgawanyo wa fedha za mchango wa Lissu, ikichepushwa kutoka kwenye namba maalumu zilizosajiliwa kwa jina la Mughwai.

Wakati huohuo, uongozi wa Chadema ulitoa ufafanuzi kuwa mchango wa Lissu uliratibiwa kupitia namba ya simu ya kaka yake (Mughwai), na upokeaji wa michango haukufanywa na sekretarieti ya Taifa au kiongozi yeyote wa chama hicho.

Kauli hiyo inafanana na ile iliyotolewa na familia ya Lissu, iliyotaka viongozi wa juu wa Chadema wasihusishwe katika sakata hilo, bali ni makada wachache walioenda kinyume na makubaliano.

“Kumekuwepo na taarifa za upotoshwaji zinazosambazwa na watu wasiokitakia mema (Chadema), zikiwahusisha viongozi wa chama na kashfa zinazohusisha madai ya michango iliyoendeshwa hivi karibuni mtandaoni kumchangia Lissu.

“Tunawaomba Watanzania na dunia nzima kupuuza taarifa potofu zinazosambazwa kwa lengo la kuchafua taswira ya chama na viongozi wake,” alieleza Brenda Rupia, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, kupitia taarifa yake kwa umma iliyotolewa Januari 29, 2026.

Kwa mujibu wa Rupia, Chadema ni taasisi inayooongozwa kwa misingi ya uadilifu, uwazi, na maadili. Hairuhusu matumizi ya jina la chama au viongozi wake kufanikisha vitendo vinavyokiuka sheria na taratibu zilizopo.