Makonda: Wananchi changamkieni fursa za miradi ya maendeleo

Arusha. Mbunge wa Arusha Mjini, Paul Makonda, amewataka wananchi wa Arusha Mjini kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazotokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali, ukiwemo ujenzi wa stendi ya kisasa ya mabasi inayojengwa katika Kata ya Olasiti, maarufu kama Bondeni City.

Makonda, ambaye pia ni Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, ametoa wito huo leo Februari 3, 2026, wakati wa ziara maalumu ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa stendi hiyo, akisema mradi huo ni miongoni mwa miradi mikubwa zaidi Afrika Mashariki, unaotarajiwa kuleta mapinduzi ya kiuchumi kwa wakazi wa Arusha.

Akizungumza na wananchi na wadau wa mradi huo, Makonda amesema kukamilika kwa stendi hiyo kutafungua fursa nyingi za ajira na biashara, hususan katika ujenzi na uendeshaji wa vizimba, maduka, na huduma mbalimbali za kibiashara.

“Serikali haiwaletei noti mfukoni, bali inafanya kazi ya kufungua fursa za kiuchumi. Miradi hii inasogezwa karibu na wananchi ili muweze kuzitumia kujiongezea kipato.

“Anzeni sasa kuzungumza na wataalamu wa mipango miji, shikeni ardhi katika maeneo haya, na anzeni ujenzi kwa maandalizi ya kufanya biashara,” amesema Makonda.

Aidha, amemtaka mkandarasi wa mradi huo kuhakikisha anakamilisha ujenzi kwa wakati uliopangwa, akisisitiza kuwa stendi hiyo ni sehemu ya maandalizi ya kuimarisha usafiri wa watalii na maandalizi ya Tanzania kuelekea mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

“Tumeweka mpango wa reli ya kisasa kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kupita hapa ili abiria washuke hapa na kuendelea na shughuli zao mbalimbali, hivyo mkandarasi hakikisha hutuangushi,” amesema.

Awali, mshauri elekezi wa mradi huo, John Benedict, amesema kukamilika kwa stendi hiyo kutapunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa magari katikati ya Jiji la Arusha, sambamba na kuboresha huduma za usafiri wa umma.

Ameeleza kuwa sehemu ya mradi huo, unaogharimu zaidi ya Sh14 bilioni, unatekelezwa ndani ya kipindi cha miezi 18 na unatarajiwa kukamilika Mei 2026 kama ilivyopangwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla, amesema atahakikisha anaufuatilia mradi huo kwa karibu kwa kufanya ziara za mara kwa mara ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na bila vikwazo vyovyote.

Amesema Serikali ya mkoa itaendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa viwango vilivyokusudiwa na kuleta tija kwa wananchi wa Arusha na Taifa kwa ujumla.

Mradi wa ujenzi wa stendi mpya ya mabasi jijini Arusha ni sehemu ya mpango wa TACTIC, unaotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa kushirikiana na Serikali Kuu pamoja na Benki ya Dunia (WB).

Mradi huo una thamani ya Sh51.56 bilioni, ukihusisha ujenzi wa masoko ya Kilombero na Mrombo pamoja na uboreshaji wa barabara zenye urefu wa zaidi ya kilomita 18.

Ujenzi wa stendi hiyo ulianza Juni 2025 na unatarajiwa kukamilika Mei mwaka huu, na utakuwa na uwezo wa kuhudumia mabasi zaidi ya 400 kwa siku, ikiwa na miundombinu ya kisasa ikiwemo maduka, ofisi, vyumba vya kupumzika, vyoo vya kisasa, na mfumo wa ulinzi kupitia ukuta na kamera za CCTV.