Pedro ashusha pumzi akimtaja Buba Morocco

BAADA ya Yanga kumtambulisha winga mpya, Buba Jammeh, kuwa usajili wa mwisho kikosini hapo kabla ya dirisha dogo halijafungwa Januari 30, 2026, hivi sasa mashabiki wa timu hiyo wanamsubiri kwa hamu kumuona uwanjani.

Wakati hamu ya mashabiki ikiwa juu, kocha wa kikosi hicho, Pedro Goncalves amefichua taarifa za staa huyo, akisema jamaa akiwahi tu basi kikosi chake kitakuwa tishio zaidi kwenye mechi zake.

Winga huyo raia wa Gambia mwenye umri wa miaka 24, hadi anayejiunga na Yanga, ameitumikia Interclube katika michezo saba yote ikiwa ya Ligi Kuu Angola na kufunga bao moja.

PEDR 01

Akizungumza na Mwanaspoti, Pedro amesema Jammeh ni mchezaji ambaye anakuja kutokana na mapendekezo yake akimfahamu kwa misimu mitatu aliyokuwa anacheza soka Angola alikokuwa anafundisha timu ya taifa hilo.

Pedro amesema Jammeh ni winga wa kisasa mwenye kasi na ufundi wa kutosha ambapo alikuwa anataka mchezaji wa namna hiyo kukipa makali zaidi kikosi chake na sasa uongozi wa timu hiyo umefanikisha kumleta.

“Ninamfahamu Jammeh vizuri sana, ni mchezaji kutoka Gambia ambaye amecheza misimu mitatu mpaka minne kule Angola, ni mchezaji mwenye kasi kubwa uwanjani, ana ufundi wa kutosha na utulivu wa akili,” amesema Pedro.

PEDR 02

“Ninaamini kwa timu ambayo tunayo atatusaidia sana, kuna kitu kikubwa atatuongezea kwenye ubora ambao tunao akiunganika na wenzake ambao atawakuta hapa. Ni usajili mzuri naweza kusema hivyo kwa sasa.”

Pedro aliongeza kuwa, hivi sasa uongozi wa klabu hiyo unapambana kukamilisha kila kitu juu ya usajili wake na ujio wake na anatamani kama atapatikana mapema wanaweza kuangalia ubora wake na kumtumia dhidi ya FAR Rabat.

Jammeh amefunga hesabu za usajili ndani ya Yanga kipindi cha dirisha dogo msimu huu lililofungwa Januari 30, 2026 akiwa mchezaji wa sita mpya kutambulishwa baada ya Emmanuel Mwanengo, Mohamed Damaro, Allan Okello, Laurindo Dilson ‘Depu’ na Hussein Masalanga.

PEDR 03

Pia Jammeh amehitimisha idadi ya wachezaji 12 wa kimataifa ndani ya Yanga wanaotakiwa kikanuni. Wengine ni Djigui Diarra, Kouassi Attohoula Yao, Frank Assinki, Chadrack Boka, Duke Abuya, Maxi Nzengeli, Pacome Zouzoua, Prince Dube, Lasine Kouma, Allan Okello na Dilson Aurélio ‘Depu’.

Yanga imeondoka nchini jana ikiifuata FAR Rabat ya Morocco, timu hizo zitacheza mchezo wa tano wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Jumamosi Februari 7 mwaka huu, jijini Rabat ambapo mabingwa hao wa Tanzania wanauita kama fainali ikisaka nafasi ya kwenda robo fainali.

PEDR 04

“Kuna mambo yamesalia ambayo uongozi unapambana kuyakamilisha, itakuwa safi kama yakimalizikika mapema na tukimpata (Jammeh) kabla ya kucheza na FAR Rabat lakini tutaangalia utayari wake kama tutaona yuko kwenye utimamu mzuri wa mwili.

“Tunaweza kuwa na mabadiliko kidogo kwenye muundo wa timu kwa kuwa tuna kikosi kipana, kama ambavyo nilikwambia huu mchezo kwetu ni fainali, tunataka kupata uhakika wa kufuzu kupitia mechi hii, hatuna kingine zaidi ya kwenda kutafuta ushindi huko.”

Wakati Pedro akisema hayo, taarifa mpya kutoka Yanga ni kwamba kikosi kikitua nchini Morocco kitamkuta Jammeh ameshafika akitokea Angola, hivyo anaweza kutumika wikiendi hii endapo benchi la ufundi litaridhishwa na utimamu wake wa mwili.