KIKOSI cha Singida Black Stars, kimeiwahi CR Belouizdad Zanzibar tayari kwa ajili ya mechi ya tano ya Kombe la Shirikisho Afrika kundi C inayotarajiwa kuchezwa Februari 8, mwaka huu huku Kocha David Ouma akipiga hesabu kali za kufuzu robo fainali.
Singida Black Stars imewasili Dar es Salaam alfajiri ya jana Jumanne ikitokea Congo Brazzaville ilipokwenda kucheza dhidi ya AS Otoho na kufungwa 2-1.
Baada ya mapumziko ya saa chache, ikaanza safari kwenda Zanzibar tayari kuikabili CR Belouizdad.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ouma amesema wameamua kuunga moja kwa moja kwenda Zanzibar kwa lengo la kupata muda wa kujiandaa vizuri wakiwa huko kabla ya kumkabili mpinzani wao ambaye wamemtaja kuwa siyo rahisi lakini wamejiandaa kupambania pointi tatu muhimu.
“Tuna mechi ngumu Jumapili dhidi ya CR Belouizdad ambao wanakuja kucheza na sisi wakiwa na kumbukumbu nzuri ya kutufunga mabao mawili wakiwa kwao na sisi tuna matarajio makubwa ya kushinda nyumbani.
“Hautakuwa mchezo rahisi, tunakutana na timu bora ambayo ina uzoefu na mashindano lakini hilo haliondoi sisi kuwa bora na kupambania pointi tatu ili kufikia malengo ya kutinga hatua inayofuata,” amesema Ouma.
Ouma amesema wanahitaji pointi zote sita kwenye mechi mbili zilizobaki, hivyo kila mchezo kwao ni fainali kwani wanatamani kuona hawadondoshi pointi hata moja.
Singida Black Stars ili ifuzu robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu, inatakiwa ishinde mechi zake mbili zilizobaki dhidi ya Belouzdad (nyumbani) na Stellenbosch (ugenini) na kuombea AS Otoho isipate pointi sita kwenye mechi mbili ilizobakiza.
