NIKWAMBIE MAMA: Wabunge wapya waielewe Serikali

Binadamu wanavutiwa sana na vitu vilivyo tofauti. Kama nguo nzima ikiwa nyeupe lakini ikapata doa dogo la rangi, macho ya wote yataangukia kwenye doa hilo.

Inawezekana hiyo ni silika ya kawaida ya binadamu, pengine anataka kujiridhisha iwapo doa hilo ni urembo au uchafu. Wasanii huwa wanaelekezwa kuvaa mavazi yanayotofautiana rangi na jukwaa ili macho ya mashabiki wao yaangukie kwao.

Wakati naingia kwenye kidato cha kwanza, nilikuwa na umbo dogo sana. Nilikuwa tofauti sana na wanafunzi wote wageni, pamoja na wale waliohamia kwenye vidato vya pili, tatu na nne. Lakini mimi nilitafsiriwa moja kwa moja kuwa “Form Less” (form one) kutokana na umbo langu.

Hivyo nikawa kivutio kwa wanafunzi wa kidato cha pili waliokuwa na kiu ya kuwapata wadogo zao wa kuwatuma sokoni.

Kumbukumbu hii inajirudia baada ya kusikiliza sehemu ya Bunge la 13 linaloendelea huko Dodoma. Nimegundua kuwa kama mimi nilivyotambulika kuwa mgeni shuleni, ndivyo inawezekana kuwatambua wabunge wapya bungeni.

Si kwa sababu ya maumbo au mavazi yao, bali kwa namna wanavyotumia muda mrefu kujieleza kuliko kuchangia mada. Wakati mwingine mbunge anajisahau na kuelekea kumshukuru kila aliyefanikisha kuingia kwake mjengoni.

Bunge lilikuwa likichangia mada kuhusu hotuba ya kwanza ya Rais bungeni. Badala ya kuchangia, wabunge hasa wale wapya walijikita kuelezea utekelezaji wa miradi ya Serikali.

Ilikuwa ni zaidi ya hotuba za mawaziri. Mwenyekiti wa kikao hicho alikuwa na kazi ya ziada kuwaelekeza wabunge hao namna ya kuchangia mada. Ilifika mahala akasema: “Taratibu tu nadhani mtazoea”.

Mbunge aliutumia muda wake wote kutoa ushuhuda huku akikiri kuwa muda wake wa kuongea ungali mfupi.

Lakini pamoja na ufupi wa muda, mbunge huyo hakujifunza namna ya kuutumia, zaidi alijipa kazi ya kukanusha maneno ya mtaani yanayobeza uwezo wa Serikali.

Naweza kabisa kusema kuwa wabunge wengi wanatumia nguvu nyingi katika mambo yasiyoisaidia Serikali yao.

Wabunge wanapaswa kuelewa kuwa kazi yao kubwa ni kuisaidia Serikali kufanya kazi kwa usahihi. Wapo watu wengine wakiwemo wapambe wanaodhani kusifia ndio kusaidia.

Hivyo badala ya kuyaondoa madoa yaliyo juu ya kanzu ya bosi wao, wao humsifia huku wakimziba macho asiyaone. Hii ni hatari kubwa kwa sababu watu watapaza sauti. Kelele zao zitasababisha bosi azibwe masikio ili asisikie.

Hatuwalaumu wale wanaopiga kelele kwani nao wapo kwa sababu maalum. Kama nikikumbuka vizuri, mzazi hamalizi maneno wakati akimpongeza mwanaye aliyeongoza ufaulu wa darasani. Pamoja na kumpongeza, hataacha kumkosoa kwenye maswali aliyokosa. Zamani alikuwepo mwalimu ambaye hakuwahi kumpa mwanafunzi alama zote hata kama alipata zote. Mwisho wake ulikuwa asilimia 99.9.

Wahenga walituasa tukubali kukosolewa na hata wendawazimu. Ukishagundua kuwa ushauri wao hautatuingiza mtegoni, basi si vibaya kuwafurahisha kwa sababu nchi hii ina wendawazimu wengi kuliko unaowaona.

Ni bora kupatia kwa bahati kuliko kukosea isivyo bahati. Wakati mwingine kichaa anayekuokoa na hatari ana faida kuliko mwanazuoni anayekulengesha shimoni.

Serikali inatambua kuwa haiwezekani kumridhisha kila mtu kwa asilimia zote. Inajua kuwa yapo maeneo korofi ambayo haijafanikiwa kuyakwamua. Pia inatambua uwepo wa watu wanaokosoa hata mafanikio.

Lakini kwa kuwa inaamini kwenye michakato, basi inaongeza jitihada za kupunguza matatizo na malalamiko angalau wote wawe salama. Hata China na Marekani hawajaweza kutatua kero za watu wao wote.

Kama tunaelewa vizuri dhima ya Serikali, inafanya kazi usiku na mchana ili kuondoa kero zote za wananchi.

Asitokee mtu akadhani kuwa Watanzania wote wamepata maji, umeme na barabara za kiwango cha lami kama alivyopata yeye. Serikali ipo mbioni kumaliza kero za wananchi wote kwa ujumla wao.

Tatizo la Mtanzania mmoja wa kule Mtwara ni tatizo la Tanzania; linaihusu Serikali kuanzia kwenye ngazi ya mtaa mpaka Taifa.

Kila mmoja akizingatia kuwa Taifa linaanza na yeye, atagundua kuwa anasubiriwa na majukumu mapya kila anapotimiza yale ya awali. Yeyote ambaye amemaliza na hana majukumu ni yule aliyefikwa na umauti.

Kadhalika Serikali baada ya kufanikiwa kutoa ruzuku ya mbolea kwa mkulima, bado inaangalia uwezekano wa kumwezesha mkulima huyu kwa “ndege nyuki” za kuhudumia shamba lake. Baadaye hata kumsafirishia mazao yake kwa Bombadia kwenda duniani.

Lakini yote haya hayawezi kufanikiwa bila michango ya wabunge. Serikali haiwezi kuwa na macho ya kuona kila jimbo la nchi, hivyo mbunge huwa daraja kati ya mwananchi na Serikali yake. Baadhi ya wabunge wanakumbuka jinsi walivyokosana na wapiga kura wao kwa kuwaacha na kuidandia Serikali.

Ni vizuri kutoa sifa kwa Serikali kutokana na mazuri yanayotendeka Kitaifa. Lakini sifa zisizidi kiasi cha Mwenyekiti au Spika kuingilia kati, maana haya ni matumizi mabaya ya muda wa kuchangia hoja.

Unaweza kudhani kuwa wapo wanaojifagilia njia za kupanda chati, lakini huwezi kukagua unadhifu wako ukiwa vitani. Fanya vizuri kazi ya wananchi na baraka zitakumwagikia hadi uzichoke.