DC ITUNDA APONGEZA JITIHADA ZA RAIS SAMIA MAGEUZI YA KIDIGITALI MAHAKAMANI

📍Azindua wiki ya Sheria Mbeya 

NA MWANDISHI WETU, MBEYA

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Mhe. Solomon Itunda, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utashi wake wa kisiasa na uwekezaji mkubwa uliowezesha mapinduzi ya kidijitali ndani ya Muhimili wa Mahakama, hatua inayorahisisha upatikanaji wa haki kwa wananchi.

Mhe. Itunda ametoa pongezi hizo wakati akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Beno Malisa, katika uzinduzi wa Wiki ya Sheria mkoani hapa.

Alisema kuwa uboreshaji wa miundombinu na mifumo ya kisasa ya TEHAMA ni matokeo ya fedha nyingi ambazo Rais Samia amekuwa akizielekeza mahakamani ili kuleta ufanisi, uwazi na uwajibikaji.

Akielezea ufanisi huo, Mhe. Itunda amebainisha kuwa kupitia utekelezaji wa maono ya Rais Samia, Mahakama imeweza kuongeza kasi ya kusikiliza na kumaliza mashauri kwa wakati, jambo linalopunguza kero kwa wananchi na kuimarisha utawala wa sheria nchini.

“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuipa kipaumbele Sekta ya Sheria. Si tu kwa upande wa majengo na teknolojia, bali pia kwa kuidhinisha ajira za watumishi wa mahakama ambazo zimekuja kuongeza nguvu kazi na kupunguza mrundikano wa kesi,” alisema Mhe. Itunda.

Aidha, Mhe. Itunda alitoa wito kwa watumishi wa mahakama na wadau wa sheria kutumia maboresho hayo yaliyowekwa na serikali kutenda haki kwa kuzingatia maadili na hofu ya Mungu. 

Alisisitiza kuwa uwekezaji huu wa serikali lazima uende sambamba na uadilifu wa hali ya juu kwa maamuzi yenye tija kwa jamii.

Mkuu huyo wa wilaya alihitimisha kwa kusema kuwa Wiki ya Sheria ni wakati muhimu wa kutathmini jinsi nchi inavyopiga hatua chini ya uongozi wa Rais Samia katika kujenga Taifa linaloheshimu haki na wajibu wa kila raia.