Musoma. Polisi Mkoa wa Mara inawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kuiba gari la wagonjwa (ambulance) kisha kulibadilisha na kuwa gari la biashara ya kubeba watalii.
Watuhumiwa hao wakazi wa Tarime mkoani Mara na jijini Arusha wanatuhumiwa kuiba gari hilo mali ya Halmashauri ya Manispaa ya Musoma mkoani Mara iliyokuwa ikitoa huduma hospitali ya manispaa hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo amesema kwenye taarifa yake kwa vyombo vya habari Februari 3, 2026 kuwa gari hilo liliibwa Oktoba 25, 2025 likiwa limeegeshwa kwenye Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma mita chache kutoka ilipo hospitali ya manispaa hiyo.
Gari la wagonjwa la hospitali ya Manispaa ya Musoma kabla halijabadilishwa mwonekano na kuwa la kubeba watalii.
“Baada ya kupata taarifa tulianza uchunguzi na upelelezi na katika uchunguzi wetu tulikamata watu wengi wakiwamo watumishi wa Serikali, lakini baada ya uchunguzi tumebaini kuwa wahusika ni hawa wanne tuliobaki nao,” amesema.
Hata hivyo, Kamanda Lutumo hakuwa tayari kutaja kazi za watuhumiwa hao kwa madai kufanya hivyo kutavuruga masuala mengine kwenye kesi hiyo. Taarifa zinadai miongoni mwa watuhumiwa hao wapo pia watumishi wa Serikali.
Amewataja watuhumiwa hao ni Goodluck Chacha (26) mkazi wa mjini Tarime, Karume Kimwel (26) mkazi wa Morombo Arusha, Said Ramadhani (39) mkazi wa Engosengyu Arusha na Elias Lyimo (53) mkazi wa Arusha.
Kamanda Lutumo amesema gari hilo aina ya Landcruiser lilipatikana jijini Arusha likiwa kwenye hatua za mwisho kubadilishwa ili liweze kutumika kama gari la kubeba watalii.
Amesema gari hilo liliibwa siku hiyo katika maegesho hayo usiku kisha watuhumiwa kulisafirisha hadi jijini Arusha ambapo waliendelea na utaratibu wao wa kulibadilisha kabla hawajatiwa mbaroni kutokana na ushirikiano ambao vyombo vya usalama ulipata kutoka kwa wananchi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo akionyesha gari la wagonjwa la hospitali ya Manispaa ya Musoma baada ya kuibiwa na kubadilishwa mwonekano.
Amesema uchunguzi tayari umekamilika, watuhumiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani muda wowote kuanzia sasa.
Hata hivyo, zipo taarifa zinadai watuhumiwa hao ni sehemu ya mtandao wa watu wanaojihusisha na wizi wa magari ya wagonjwa kutoka katika halmashauri mbalimbali nchini kisha kuzibadili na kuwa magari ya kubeba watalii.
Alipoulizwa kuhusu mtandao huo Kamanda Lutumo hakuwa tayari kuzungumza kwa maelezo kuwa, taarifa zaidi kuhusu maeneo mengine zitataolewa na viongozi wa maeneo husika.
“Mimi nazungumzia mkoa wangu wa Mara, huko kwingine pia watazungumza wakiwa tayari wamekamilisha mambo yao, kwasasa naomba nizungumzie ambulance hii moja iliyoibwa hapa Manispaa,” amesema.
Gari la wagonjwa la hospitali ya Manispaa ya Musoma baada ya kubadilishwa mwonekano.
Kuna taarifa za kuwepo kwa wizi wa magari ya wagonjwa, hadi sasa inadaiwa magari zaidi ya 10 yameibwa kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Wakizungumza kuhusu suala hilo baadhi ya wakazi wa Musoma wamesema licha ya watuhumiwa kuchukuliwa hatua lakini pia kitengo cha ulinzi cha manispaa hiyo kinapaswa kuwajibishwa.
David Obure amesema kitengo hicho kimeonesha uzembe wa hali ya juu kuruhusu wizi wa aina hiyo kufanyika.
“Mbali na watuhumiwa kukamatwa lakini pia kitengo cha ulinzi katika manispaa kinapaswa kutizamwa kwa umakini sana ni ajabu sana mtu kutoka nje kuingia ndani ya uzio wa manispaa tena kupitia getini na kuondoka na gari bila kushtukiwa wala kukamatwa,hii ni ajabu,” amesema.
Ismail Mbura amesema kitendo hicho kinaonesha namna gani mali za umma hazipo salama katika halmashauri hiyo.
“Kama gari inaweza kupita getini bila mwizi kukamatwa vipi kuhusu vitu vidogo vidogo ambavyo mtu anaweza kuweka kwenye mkoba au begi dogo,hii ni hatari sana,” amesema.
Katika hatua nyingine, jeshi hilo limefanikisha kutaifishwa kwa gari aina ya Toyota Hilux baada ya kukamatwa likiwa linasafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi.
“Dereva wa gari hili Abdallah Hussein (30), mkazi wa Mtaa wa Kambarage mkoani Shinyanga alikamatwa na mirungi yenye uzito wa kilogramu 67 wilayani Bunda akiwa anasafirisha dawa hizo kwenda Shinyanga,”amesema.
Aidha katika msako uliofanyika Januari mwaka huu jeshi hilo pia limewakamata watuhumiwa 190 kwa tuhuma za kupatikana na bangi kilogramu 30, pombe aina ya gongo lita 2,464 pamoja na mitambo minne ya kutengeneza gongo.
Kamanda Lutumo amesema majalada ya kesi hizo yapo katika hatua mbalimbali ya kisheria huku mengine yakiwa yamefikishwa mahakamani kwa hatua zingine.
