Leo naendelea na mfululizo wa makala za historia ya Katiba ya Tanzania, tulioanza wiki iliyopita kwa kuangazia katiba nne za mwanzo: Katiba ya Uhuru ya mwaka 1961, Katiba ya Jamhuri ya mwaka 1962, Katiba ya Muungano ya mwaka 1964, pamoja na Katiba ya Mpito ya mwaka 1965.
Katika makala hii, ninaichambua Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ambayo ndiyo Katiba ya kwanza ya kudumu ya taifa letu.
Katiba ya mwaka 1977 ni Katiba ya tano katika historia ya Tanzania. Hata hivyo, kama zilivyokuwa katiba zilizotangulia, nayo pia haikutungwa kwa ushiriki wa wananchi. Ilitungwa kupitia Tume ya Rais Julius Nyerere, wakati Tanzania ikiwa chini ya mfumo wa chama kimoja.
Katika kipindi hicho, chama ndicho kilichokuwa na mamlaka makuu ya kuongoza Serikali. Rais Nyerere, ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha TANU, aliteua wajumbe 20 wa Tume hiyo 10 kutoka Tanzania Bara na 10 kutoka Zanzibar, ikiongozwa na Sheikh Thabit Kombo Jecha, huku Katibu wake akiwa Pius Msekwa.
Tume hiyo iliandaa Katiba ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilichoundwa baada ya kuunganishwa kwa Tanu na Afro-Shirazi Party (ASP) tarehe 5 Februari 1977.
Katiba ya CCM ndiyo iliyogeuzwa kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Katiba hiyo ilijengwa juu ya misingi mikuu mitatu: urais wenye mamlaka makubwa (urais wa kifalme), mfumo wa chama kimoja cha siasa, na muundo wa serikali mbili uliokuwa na mwelekeo wa serikali moja.
Katiba hiyo ilipitishwa na Bunge la CCM lililojigeuza kuwa Bunge Maalum la Katiba, na kuipitisha ndani ya muda mfupi wa takribani dakika 30 tu.
Kwa msingi huo, ni wazi kuwa katiba zote tano zilizowahi kutumika nchini hazikushirikisha wananchi moja kwa moja.
Jaribio la kwanza la kuwashirikisha wananchi lilifanyika kupitia Tume ya Jaji Joseph Warioba na Bunge Maalum la Katiba, lakini mchakato huo haukukamilika.
Hivyo basi, mchakato mpya unaoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuelekea kupata Katiba Mpya, unaotarajiwa kuwashirikisha wananchi kikamilifu, unaleta matumaini mapya. Endapo mchakato huo utafanikiwa na Katiba Mpya kupatikana, basi hiyo itakuwa Katiba ya kwanza ya kweli ya wananchi wa Tanzania.
Kwa mantiki hiyo, inapendekezwa kwamba Katiba hiyo iitwe ‘Katiba ya Samia,’ hasa ikizingatiwa kuwa Katiba ya Warioba haikufanikiwa kupatikana.
Katiba ni nini? Katiba ni mkataba wa kijamii kati ya watawala na watawaliwa. Ni mamlaka kuu ya nchi inayopaswa kuheshimiwa na kila mtu bila ubaguzi.
Nchini Tanzania, hakuna mtu aliye juu ya Katiba. Ndiyo maana viongozi wote, wanapochaguliwa au kuteuliwa, huapa kiapo cha utii kwa Katiba, kuilinda, kuiheshimu, kuitetea na kuitekeleza.
Katiba ina kazi gani? Katiba ndiyo msingi mkuu na mwongozo wa uendeshaji wa nchi. Sheria zote, kanuni zote na taratibu zote za utawala lazima zitokane na Katiba na zilingane nayo. Katiba ya Tanzania imejengwa juu ya misingi mikuu minne: uhuru, haki, udugu na amani. Misingi hii inaweza kudumishwa kikamilifu katika jamii ya kidemokrasia, yenye Bunge linalowakilisha wananchi, Mahakama huru inayotoa haki bila woga wala upendeleo na Serikali inayowajibika kwa wananchi.
Katiba ni ya nani? Katiba ni mali ya wananchi. Ni Katiba ya watu, iliyotungwa kwa niaba yao kwa lengo la kujenga jamii yenye haki, uhuru, mshikamano na amani.
Kwa mujibu wa Katiba, jambo muhimu zaidi katika Taifa ni watu wenyewe. Watanzania ndiyo wenye Katiba, na wao ndiyo walioweka misingi yake mikuu. Uhuru na haki ni nguzo kuu za Katiba; bila uhuru hakuna haki, na bila haki hakuna amani ya kweli.
Katika uendeshaji wa nchi, kuna mihimili mitatu ya dola: Serikali, Bunge na Mahakama. Ili mihimili hii ifanye kazi kwa mujibu wa Katiba, nafasi ya wanasheria ni muhimu sana.
Hata hivyo, licha ya viongozi kuapa kuilinda Katiba, baadhi yao huitekeleza bila uelewa wa kina. Matokeo yake ni kuikanyaga na kuivunja Katiba bila wao kutambua. Hali hiyo inaonekana katika mihimili yote mitatu.
Serikali hutunga miswada ya sheria inayokwenda kinyume na Katiba, Bunge hupitisha sheria hizo batili na Mahakama, ambayo ndiyo yenye jukumu la kutafsiri Katiba hushindwa kuchukua hatua stahiki, hali inayosababisha Katiba kuvunjwa waziwazi.
Ujio wa Katiba Mpya una nafasi ya kuondoa mapungufu haya yote. Endapo mchakato huo utafanikiwa, Rais Samia Suluhu Hassan ataingia katika historia kama Rais wa kwanza wa Tanzania kuwapatia wananchi Katiba yao halisi.
