Siasa ni jukwaa la kuchuma pesa kwa njia ya mkato, bila kuvuja jasho. Unaweza kubadili sentensi hiyo utakavyo, lakini maana itabaki hiyo. Ukosefu wa uadilifu ndani ya jumuiya ya wanasiasa, ni tatizo la kimsingi.
Wananchi hawajui ya ndani kuhusu wanasiasa. Matokeo yake hudanganyika kulingana na mambo ya juujuu. Mzuri mdomoni, anaweza kuonekana shujaa, mtetezi wa haki za watu, kumbe maisha yake yamezungukwa tamaa na ufisadi.
Kiongozi aliyeondolewa ofisini kwa ukosefu wa uadilifu, baada ya kubainika ameingiziwa fedha chafu kwenye akaunti yake binafsi, miaka 11 baadaye anaimbwa kuwa ni jasiri na mtetezi wa raia.
Wananchi wanasaka faraja. Wakosefu wa uadilifu wanatambua hilo, wanacheza na fursa. Wanajua wananchi wanataka kusikia nini ili wapumue. Ndicho wanakizungumza. Matokeo yake, wananchi wanawaimba na kuwasherehekea kama wakombozi.
Yupo mtu niliona mitandaoni anaitwa shujaa, kwamba yeye hapokei hongo. Ni mwanasiasa wa upinzani, kiongozi wa kitaifa. Dhahiri, wananchi wameweka matumaini yao kwake. Je, ni kweli ni mwadilifu? La hasha! Wananchi hawamjui.
Mtu ambaye aliumwa, akashindwa kujigharamia matibabu. Akapelekwa nje ya nchi kwa msaada, ambao anaona aibu kuusema hadharani. Anarejea nchini, ananunua gari la Sh250 milioni. Usafi wa mtu huyo unatokea wapi?
Wenzake wanamshitukia, migogoro inaanza ndani ya chama. Mgogoro siyo kwa nini mwenzao amekosa uadilifu, bali kwa nini anakula peke yake. Misuguano mingi ndani ya vyama, kusemana na kushushana hadhi, chanzo chake kikubwa ni wivu wa kuzidiana urefu wa kamba. Anayekula zaidi, lazima anyooshewe kodole.
Ajabu, anayenyoosha kidole naye si msafi, isipokuwa amezidiwa na mwenzake ambaye kamba yake ya ulaji ni ndefu. Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ingefanya kazi sawasawa kuchunguza na kukagua maisha ya wanasiasa, wananchi wangewajua vizuri wanasiasa wao mashujaa.
Unaweza kumwona mwanasiasa anapaza sauti, ukadhani anatetea umma. Kumbe anashughulika na masilahi. Ama anatisha ili aitwe pembeni apozwe, au anatumikia kibunda alichopewa na watu wenye masilahi ya jambo husika. Ni siasa za kitapeli. Takukuru inawalea wanasiasa wa aina hii kwa kutowashughulikia inavyotakiwa.
Ajabu ya wanasiasa! Kila mwanasiasa atatamba kuwa hapokei rushwa, atasema yeye ni msafi. Shida kubwa siyo wanasiasa wala tamaa, ukweli ni kuwa wingi wa fedha ambazo zinamwagwa ndani ya mzingo wa kisiasa Ndiyo shida kubwa.
Binadamu mmoja ndani ya watu milioni, ndiye anaweza kuwa na msimamo wa kudumu wa kugomea fedha chafu. Wengine watapokea siku ya kwanza wanayopewa, wachache watakataa kwa mtindo wa sitaki nataka, kisha watalegeza na kupokea. Hivyo, vita yoyote baina ya fedha chafu ni mapambano ya mtu mmoja dhidi ya watu milioni. Je, peke yako utashinda?
Mei 2, 2024, Uwanja wa Mwembetogwa, Iringa, Makamu Mwenyekiti Chadema, Tanzania Bara, Tundu Lissu, alizungumza kwa hisia kuwa kuna fedha nyingi zimeingizwa kwenye uchaguzi wa chama hicho. Aliwatahadharisha wanachama kuwa macho dhidi ya fedha hizo ambazo yeye alidai anajua zilipotoka.
Hapa mjadala haikuwa Lissu kukishambulia chama chake na kuonesha udhaifu kwamba wao ndani kwa ndani hawawezi kudhibiti rushwa, mpaka anaamua kupaza sauti kwenye kadamnasi. Hoja ni namna ambavyo fedha zimeendelea kuwa tishio kwenye siasa, mithili ya mapambano dhidi ya dawa ya kulevya, yanavyopita katikati ya majaribu makubwa mno; fedha.
Je, fedha imeanza kuyumbisha siasa leo? Muongo mmoja unaondoka unafuata mwingine, karne kwa karne, milenia hadi milenia. Bara kwa bara, nchi baada ya nchi, wimbo haubadiliki kuwa fedha zimekuwa zikiziweka siasa katikati ya majaribu. Kila mtu hapokei pesa chafu ila zinapokelewa. Ajabu, anayefoka kuhusu rushwa, naye ana bei yake. Akishaonwa, ananyamaza.
Ghafla, wanasiasa hawapimani kwa utumishi wao kwa umma, bali wanashindana kwa wanavyomiliki. Vipimo hivyo ndivyo husababisha wivu na husuda. Yupo atakayesimama kulaani mwenzake kupokea fedha, kumbe haumizwi kwa uadilifu, bali husuda ya kukosa mwenzake kupata, au wivu wa kuzidiwa umiliki wa vitu. Chanzo ni siasa kukithiri mabilioni.
Mapitio ya kitabu, “Drug Politics: Dirty Money and Democracies” – “Siasa za Dawa: Fedha Chafu na Demokrasia”, kilichotoka mwaka 1999, mwandishi David Jordan, anaeleza jinsi ambavyo dawa za kulevya zinavyolindwa kiutamaduni na kisiasa duniani kote, halafu athari ya biashara hiyo kifedha, kisayansi, kijamii na kisiasa, inadidimiza demokrasia.
Jordan, amejenga hoja zake kupitia mifano ya nchi za Amerika Kusini, Mexico, Urusi na Marekani. Kwamba tatizo la dawa za kulevya siyo uuzaji na ununuaji, bali mabilioni ya dola yaliyopo kwenye mzunguko wa biashara hiyo. Rejea swali; nani aliyewahi kuanzisha vita dhidi ya fedha akafanikiwa?
Kama alivyosema Jordan, jielekeze kwenye hoja ya Lissu; tatizo siyo wanaotoa fedha na wanaopokea, shida ya siasa ipo kwenye mabilioni yaliyopo katikati ya mzingo wa kisiasa. Ajabu zaidi, siasa si biashara wala huduma yenye kuhitaji malipo, bali utumishi.
Kikubwa ambacho mwanasiasa anaweza kupata ni mshahara ambao kwa wastani ni milioni chache. Hata hivyo, uwepo wa mabilioni kwenye mzingo wa kisiasa, husababisha siasa kugeuka fursa ya utajiri. Na huo ni mtego mkubwa unaoiweka demokrasia njiapanda.
Ni vigumu kuishinda biashara ya dawa za kulevya kwa sababu ya fedha. Ustawi wa demokrasia upo majaribuni kisa ni pesa. Wasafi wa jana, leo ni wachafu, fedha imewachafua. Wachafu wanageuka wasafi, fedha inawasafisha. Ushindi wa siasa safi na demokrasia, utategemea ushindi wa kuyaondoa mabilioni kwenye mzingo wa siasa. Nani anaweza kushinda vita dhidi ya fedha?
Rejea vita dhidi ya pesa taslimu (War on Cash), mataifa makubwa yamefeli. Uhitaji mkubwa wa fedha taslimu, umesababisha ishindikane kupunguza uchapaji wa noti. Maana mzunguko wa fedha taslimu ni mkubwa na una siasa nyingi za kifedha, ikiwemo mipango ya kiharamia, hasa utakatishaji fedha (money laundering).
Kama Takukuru itaweza kushughulika na rushwa za kisiasa, itakuwa rahisi kudhibiti rushwa ndani ya ofisi za Serikali. Wananchi watawajua wachafu wanaowahadaa kuwa ni wasafi. Utapeli wa kisiasa utapungua, kama si kuondoka kabisa.
