Libya. Mwanamapinduzi Seif al-Islam Gadhafi, ambaye ni mtoto wa rais wa zamani wa Libya Moammar Gadhafi, imeripotiwa ameuawa katika mji wa Zintan.
Mtandao wa Africa News umeeleza kuwa, maofisa usalama wa Libya wamethibitisha kutokea mauaji ya Seif jana Jumanne Februari 3, 2026.
Mazingira ya kifo chake hayajatangazwa rasmi, lakini vyombo vya habari vya Libya vimeripoti kuwa inadaiwa aliuawa na watu wenye silaha nyumbani kwake.
Mtoto huyo wa kiongozi huyo wa zamani alizaliwa Juni 1972, alipata shahada ya uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha London School of Economics, na alitambulika kama sura ya mageuzi ya utawala wa Gadhafi.
Rais huyo wa zamani, Moammar Gadhafi alipinduliwa madarakani mwaka 2011 kupitia uasi wa wananchi ulioungwa mkono na majeshi ya Nato, baada ya kutawala kwa zaidi ya miaka 40.
Aliuawa mwaka huohuo katikati ya mapigano yaliyoibuka, ambayo baadaye yaligeuka kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Miaka ya hivi karibuni Seif alikamatwa alipokuwa akijaribu kukimbilia nchini Niger. Hata hivyo, wanamgambo walimwachilia huru Juni 2017 na tangu wakati huo alikuwa akiishi Zintan.
Mahakama ya Libya ilimhukumu kwa kosa la kuchochea vurugu na kuwaua waandamanaji na ikamhukumu adhabu ya kifo bila yeye kuwepo mahakamani mwaka 2015.
Pia, Seif alikuwa anatafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa tuhuma za uhalifu dhidi ya binadamu zinazohusiana na uasi wa mwaka 2011.
