Serikali yataja sababu kutojenga stendi Ngara, kugawa ardhi Hifadhi ya Isalalo

Dodoma. Serikali imekiri stendi ya mabasi katika wilaya ya Ngara, Mkoa wa Kagera haitoshelezi mahitaji ya huduma kwa mji huo ambao unaendelea kukua.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Reuben Kwagilwa alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Ngara (CCM), Dotto Bahemu.

Katika swali lake, Bahemu ameuliza ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Stendi ya Ngara mjini ambayo anasema ni mji usio na stendi ya kutosha kwa hadhi yake.

Katika swali la nyongeza, mbunge huyo ameuliza ni kwa nini Serikali isiwe na mkakati madhubuti katika ujenzi wa stendi katika mji huo ambao unapakana na nchi jirani za Burundi na Ruanda lakini katika maeneo yake ikiwemo na mji wa Rusumo hakuna stendi zenye hadhi badala yake mabasi yanasimama na kuegesha maeneo ya kwenye korido.

Naibu Waziri amesema Halmashauri ya Wilaya ya Ngara inayo stendi ndogo inayotumika kwa sasa ambayo haikidhi mahitaji ya huduma za usafiri kwa Mji wa Ngara unaoendelea kukua.

“Kwa kuwa eneo la stendi iliyopo sasa halitoshelezi ujenzi wa stendi ya kisasa, Halmashauri inaendelea na taratibu za tathmini ili kutwaa eneo lingine kwa ajili ya ujenzi wa stendi ya kisasa,” amesema Naibu Waziri.

Amesema katika bajeti ya mwaka 2026/27, Halmashauri imepanga kutenga Sh150 milioni kutoka kwenye mapato ya ndani kwa ajili ya kulipa fidia ya eneo hilo ili ujenzi uanze haraka.

Kwagilwa amesema mara baada ya kukamilika kwa taratibu za utwaaji wa eneo, Halmashauri itajumuisha mradi wa ujenzi wa Stendi ya Ngara Mjini katika mipango na bajeti zake ili kuanza utekelezaji wa ujenzi huo, kulingana na hali ya upatikanaji wa fedha.

Katika hali ya haraka, amemuagiza Mkurugenzi wa Wilaya ya Ngara kufanya tathimini ya haraka katika maeneo hayo kwani yana umuhimu wake na katika hilo ni lazima aje na mipango madhubuti yenye kutoa majibu.

Katika hatua nyingine, Serikali imesema haina mpango wa kugawa au kumega Hifadhi ya Msitu Isalalo kwa matumizi ya kibinadamu, ikisisitiza hifadhi hiyo ilianzishwa mahsusi kwa ajili ya uhifadhi wa mazingira, vyanzo vya maji na udhibiti wa athari za mabadiliko ya tabianchi.

Badala yake, imewashauri wananchi wanaozunguka hifadhi hiyo kuzingatia Mipango ya Matumizi bora ya Ardhi katika maeneo yao, huku wakiruhusiwa kufanya shughuli zisizokinzana na uhifadhi wa mazingira, ikiwemo ufugaji nyuki, ili waweze kunufaika kiuchumi bila kuathiri mazingira.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Hassan Chande wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbozi, Onesmo Mnkondya, aliyehoji mpango wa Serikali kuwapatia kipande cha ardhi wananchi wanaozunguka hifadhi ndogo ya Isalalo inayosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Hassan Chande 

Chande amesema Hifadhi ya Msitu Isalalo ina umuhimu mkubwa wa kiikolojia, ikiwemo kuhifadhi vyanzo vya maji, mimea na wanyama, kulinda udongo na kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Amesema hifadhi hiyo imezungukwa na vijiji vitano ambavyo ni Itentula na Hamwelo vilivyopo Kata ya Itaka, pamoja na vijiji vya Nambizo, Ipapa na Utambalila vilivyopo Kata ya Nambizo, hali inayoongeza umuhimu wa kuilinda ili kuendelea kutoa huduma muhimu za kiikolojia kwa jamii zinazozunguka eneo hilo.

“Kwa sasa Serikali haina mpango wowote wa kumega au kubadili matumizi ya hifadhi hiyo kwa shughuli za kibinadamu,” amesema Naibu Waziri huyo akisisitiza uamuzi huo unalenga kulinda maslahi ya kizazi cha sasa na kijacho.

Hata hivyo, amesema Serikali inaruhusu wananchi kuendesha shughuli ambazo hazikinzani na uhifadhi wa mazingira ndani ya hifadhi hiyo, ikiwemo ufugaji nyuki, shughuli ambayo tayari baadhi ya wananchi wameanza kuifanya kwa mafanikio.

Katika swali la nyongeza la Mbunge huyo wa Mbozi alihoji wananchi wanaozunguka hifadhi hiyo wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa ardhi, akidai kuwa hifadhi hiyo haina hadhi wala wanyamapori wakubwa, huku akitolea mfano kuwa hata sungura hawapo, hivyo akahoji kwa nini wananchi wasipewe sehemu ya ardhi hiyo ili kuendeleza kilimo cha kibiashara.

Akijibu hoja hiyo, Naibu Waziri amewataka wananchi kuwa na subira, akieleza suala hilo linahitaji kufanyiwa tathmini ya kitaalamu, lakini kwa sasa Serikali inaona ni vigumu kumega au kubadili matumizi ya eneo hilo.

Hifadhi ya Msitu Isalalo ipo katika Mkoa wa Songwe, wilayani Mbozi, na Serikali imesisitiza kuwa itaendelea kulinda rasilimali za asili huku ikihamasisha ushiriki wa wananchi katika shughuli rafiki za uhifadhi kwa manufaa ya sasa na ya baadaye.