Na. Philipo Hassan – Dodoma
Menejimenti ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) ikiongozwa na Mjumbe wa Bodi ya TANAPA Dkt. Robert Fyumagwa na Naibu Kamishna wa Uhifadhi, Massana Mwishawa leo Februari 4, 2026 imefanya ziara katika Maabara ya Uchunguzi wa DNA za Wanyamapori iliyopo chini ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali iliyopo Jijini Dodoma.
Timu ya TANAPA ilipokelewa na Daniel Ndiyo, Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) aliewakaribisha kwa niaba ya Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko ambapo, ziara ya TANAPA inalenga kujifunza namna maabara hiyo inavyofanya kazi kama wadau muhimu katika masuala ya uchunguzi wa kisayansi wa wanyamapori.
Aidha, Daniel alieleza kuwa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) kupitia Maabara ya Uchunguzi wa vinasaba (DNA) za Wanyamapori inatoa msaada wa kitaalamu na kisayansi katika kuimarisha utekelezaji wa sheria mbalimbali ambapo ni pamoja na sheria ya uhifadhi wa wanyamapori”
Naye, Dkt. Fidelis Bugoye, Meneja wa Maabara ya Sayansi Jinai Baiolojia na Vinasaba alitoa wasilisho kuhusu namna maabara ya mkemia mkuu inavyofanya kazi kwa kueleza kuwa “tunasimamia uratibu wa shughuli za uchunguzi, msaada wa kiufundi, pamoja na upokeaji, uhifadhi na uchambuzi wa vielelezo vinavyotumika kama ushahidi katika kesi za uhalifu wa wanyamapori.”
Akizungumza katika ziara hiyo, Dkt. Robert Fyumagwa aliipongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi na kutumia vifaa vya tekinolojia ya kisasa na kufikia kutoa matokeo ndani ya siku 35.
“Tunawapongeza sana kwa kuendelea kufanya kazi nzuri inayosaidia katika utoaji wa ushahidi wa makosa ya kijinai (ujangili wa wanyamapori), kwa mwaka jana 2025 mliweza kuchakata jumla ya Sampuli 183 na kuzitolea ushahidi wa kitaalam katika mahakama” alieleza Dkt. Fyumagwa.
Lengo la TANAPA kutembelea ofisi hiyo ni kuimarisha uwezo wa Shirika katika utekelezaji wa sheria za uhifadhi kwa kujifunza mbinu za kisasa za uchunguzi wa kisayansi, ukusanyaji na uhifadhi wa vielelezo, pamoja na matumizi ya teknolojia ya DNA katika kudhibiti uhalifu wa wanyamapori, sambamba na kuimarisha ushirikiano wa kitaalamu, kujenga uwezo wa rasilimali watu, na kuboresha mikakati ya kulinda bioanuwai na kukabiliana na biashara haramu ya wanyamapori.
Ziara hiyo iliambatana na kutembelea Maabara ya Vinasaba vya Wanyamapori “Wildlife DNA Laboratory” ambapo maabara hiyo ina jukumu la uchambuzi wa vinasaba “DNA” vya wanyamapori, kutoa ushahidi wa kisayansi kwa kesi za ujangili, kutoa mafunzo juu ya ukusanyaji na uhifadhi wa sampuli, kuhifadhi na kusimamia kanzidata ya vinasaba (Genetic Database) na Kusaidia ushirikiano kati ya Taasisi mbalimbali za Serikali.




