Samia ainadi Tanzania jukwaa la uwekezaji duniani

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania imepanda nafasi tisa katika orodha ya mataifa yanayotajwa kuwa vituo bora vya uwekezaji duniani, huku akiwaalika wawekezaji kuwekeza nchini.

Samia ametoa kauli hiyo usiku wa kumkia Februari 4, 2026, alipozungumza katika uzinduzi wa Jukwaa la Uwekezaji Duniani kwa upande wa Afrika (GAIS), linalofanyika Dubai, katika Taifa la Falme za Kiarabu.

Amesema kupanda kwa nafasi hiyo ni matokeo ya mabadiliko ya kimkakati yaliyofanywa na Serikali katika kuboresha mazingira ya biashara, miundombinu, na uaminifu wa taasisi za umma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza katika mjadala wa Jukwaa la Serikali za Dunia (WGS2026), leo Februari 4, 2026 Madinat Jumeirah, Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Rais amesema Serikali ya Tanzania imejikita katika kujenga misingi imara inayowawezesha wawekezaji kufanya biashara kwa uhakika na kwa gharama nafuu, akitaja miundombinu ya kisasa kuwa nguzo kuu ya safari hiyo.

“Kwa ujumla, Tanzania tayari imejenga uti wa mgongo wa ukuzaji biashara,” amesema Rais Samia, akibainisha uwekezaji umeelekezwa katika reli ya kisasa na maboresho ya bandari.

Amesema miundombinu hiyo inalenga si tu kuhudumia soko la ndani, bali pia kuifanya Tanzania kuwa lango muhimu la biashara kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, jambo linaloongeza mvuto wake kwa wawekezaji wa kimataifa.

Mbali na miundombinu, Rais Samia amesema Serikali imeandaa maeneo maalumu ya kiuchumi yaliyobuniwa mahsusi kwa ajili ya wawekezaji, yakitoa vivutio mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa ardhi ya uwekezaji, punguzo la kodi, na huduma zote muhimu kupitia kituo cha huduma za pamoja.

Amesema mfumo huo unalenga kuondoa urasimu, kupunguza muda wa kupata vibali, na kuhakikisha michakato ya uwekezaji inakuwa rahisi, ya haraka, na inayotabirika.

Rais Samia ameongeza kuwa moja ya sababu kubwa zinazoiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya ushindani wa kimataifa ni msimamo wa Serikali wa kutimiza ahadi zake.

“Wawekezaji wa sasa hawatazami fursa pekee, bali wanatafuta uaminifu wa taasisi, sera zinazotabirika, na mshirika anayetimiza ahadi zake,” amesema, akisisitiza kuwa Tanzania imejizatiti kuwa mshirika wa aina hiyo.

Amesema Serikali inatambua umuhimu wa kujenga uhusiano wa uwekezaji unaozingatia heshima, uwajibikaji, na ustawi wa pamoja, badala ya mahusiano ya muda mfupi yasiyo na mwelekeo wa maendeleo ya muda mrefu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan (wa pili kushoto) akishiriki mjadala katika Jukwaa la Serikali za Dunia (WGS2026), leo Februari 4, 2026 Madinat Jumeirah, Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Katika hotuba yake, Rais Samia amelitaja Jukwaa la Uwekezaji Duniani kama ishara ya mabadiliko ya kimkakati katika namna nchi zinavyoshirikiana kiuchumi, likihama kutoka utegemezi wa misaada na kuelekea kukuza uwekezaji unaovutia mitaji mikubwa ya kimataifa.

Amesema jukwaa hilo linawakilisha mabadiliko kutoka ushirikiano usio na mshikamano kwenda ushirikiano ulioratibiwa, kutoka miradi ya kawaida hadi miradi iliyopangwa kitaalamu inayoweza kuvutia taasisi kubwa za kifedha na kuendana na vipaumbele vya kitaifa.

“Hili ndilo jukwaa mahsusi linalohitajika barani Afrika kwa ajili ya kukusanya mitaji ya kimataifa kwa ukubwa,” amesema Rais Samia, akibainisha kuwa Tanzania iko tayari kushiriki kikamilifu katika mwelekeo huo.