POLISI MWANZA YAKANUSHA TAARIFA ZA UWEPO WA VIKUNDI VYA KIHALIFU NA UASI

:::::::::::

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limetoa wito kwa wananchi kupuuza taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zenye kichwa cha habari kinachoeleza kuwa “kundi la uasi laibuka Mwanza, Polisi waonekana mitaani.”

Kulingana na Taarifa ya Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Wilbrod Mutafungwa amesema taarifa hizo ni za upotoshaji zikiwa na lengo la kuleta taharuki kwa jamii, kwani wahalifu wa matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii wamekuwa wakichukua picha za askari na vitendea kazi vyao kisha kutengeneza maudhui yenye lengo la kuzua taharuki, kuchonganisha na kupandikiza chuki. 

“Jeshi la Polisi linawasisitiza wananchi kuendelea kuwapuuza watu kama hao wanaosambaza taarifa zenye nia ovu na badala yake wafuatilie na kupata taarifa zenye ukweli na usahihi kutoka kwenye mamlaka zenye jukumu la kufanya hivyo.” Amesema Kamanda Mutafungwa.

Aidha, Jeshi la Polisi limesema linaendelea kuwafuatilia kwa karibu watu wote wanaoandaa na kusambaza taarifa za uongo, uchonganishi na zenye kupandikiza chuki kwa jamii kwani ni kinyume cha sheria za nchi. 

Katika hatua nyingine Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limesema hali ya usalama katika Mkoa wa Mwanza ni shwari na wananchi wanaendelea na shughuli zao za kila siku za kujitafutia kipato katika mazingira ya amani, utulivu na usalama huku askari Polisi nao wakiendelea kutimiza majukumu yao ya kulinda maisha ya watu na mali zao kwa ushirikiano mkubwa na wananchi na vyombo vingine vya usalama.